Na Bashir Nkoromo, CCM Blog
Mkuu wa Wilaya ya Ubungo jijini Dar es Salaam Kisare Makori, amewaagiza Watendaji wa Mitaa katika Wilaya hiyo, kwamba kuanzia sasa waanze kazi ya kufanya utambuzi wa majengo na mabango ya matangazo katika mitaa yao na kuwataka hadi ifikapo tarehe 27 mwezi huu wawe wamekamilisha kazi hiyo.
Amesema, lengo la kufanya utambuzi huo ni kutekeleza agizo la Serikali la kuwataka Watendaji wote wa mitaa kusimamia ukusanyaji kodi za majengo na mabango katika maeneo yao, hivyo lengo la kufanywa utambuzi huo ni kuhakikisha kuwa kazi ya ukusanyaji kodi kutoka vyanzo hivyo itafanyika kwa usahihi.
Makori alisema hayo, leo katika kikao chake na Watendaji wa Kata na Mitaa, Wenyeviti wa Mitaa, Wakuu wa Idara na Wakuu wa Vitengo, kilichofanyika katika Ukumbi wa Little Flower, Mbezi Wilayani humo Jijini Dar es Salaam, na kuhudhuriwa na Mkurugenzi wa Manispaa ya Ubungo Beatrice Dominc, Katibu Tawala wa Wilaya hiyo James Mkumbo na Viongozi wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya.
Akitoa ufafanuzi, Makori alisema, mambo ya kuzingatia katika utambuzi huo kwa upande wa majengo, ni kuainisha aina ya jengo na kama ni ghorofa litajwe ni la ghorofa ngapi, Jina kamili la mmiliki au msimamizi wa jengo husika na namba za simu za msimamizi au mmiliki wa jengo na kwa upande wa mabango ni kupata jina la Taasisi, Kampuni au mmiliki wa bango husika katika mtaa.
"Natanguliza kuwaambia kabisa, utoaji wa taarifa zisizo sahihi kunaweza kukuingiza katika matatizo makubwa kwa mujibu wa sheria, kwa hiyo ni wajibu kwa kila mtendaji kuhakikisha anachukua taarifa hizo za utambuzi kwa usahihi mkubwa. Namba za simu hakikisha ni namba 'functional', siyo unachukua namba ambayo ikipigwa inasema..., hiyo hapana", alisisitiza Makori.
Alisema, baada ya ukusanyaji wa taarifa za utambuzi, Watendaji wazipeke taarifa hizo kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Wilaya hiyo kabla ya tarehe 27 mwezi huu ambayo nidiyo siku ya mwisho, na kuongeza kuwa kazi hiyo ni lazima ifanywe kwa ushirikiano na viongozi wa ngazi zote wakiwemo Wenyeviti wa mitaa.
Makori alifafanua zaidi kwamba wakati wa kukusanya taarifa za kuanisha, taarifa za majengo na mabango zisichanganywe pamoja, badala yake taarifa za mabango zile na kabrasha lake na zile za majengo pia ziwe na kabrasha lake.
"Mwaka jana Tanzania iliingia katika Uchumi wa Kati, sasa kama mnavyojua matokeo haya yana faida na athari zake, hapa athari yake ni kwamba nchi ikiingia uchumi wa kati kuna aina ya misaada ambayo haipati kutoka Taasisi za Kifedha za Kimataifa, kwa hiyo pamoja na kuingia uchumi wa akati bado kuna mapengo ambayo Serikali lazima tuyafanyie kazi ili maendeleo yaonekane... Na kama mnavyojua Serikali haina Biashara zaidi ya kukusanya kodi", alisema Makori mwanzoni mwa hotuba yake akizungumza kwenye kikao hicho.
Alisema, Serikali imetoa maelekezo ya watendaji kukusanya kodi za majengo na mabango, kwa kuwa sasa ukusanyaji wa kodi za vyanzo hivyo umerejeshwa chini ya Halmashauri husika tofauti na awali ambapo ukusanyaji huo ulikuwa chini ya Serikali Kuu.
MALALAMIKO YA MAPATO NA MATUMIZI
Akizungumzia kadhia ya baadhi ya watendaji wa Serikali za Mitaa, Mkuu wa Wilaya aliagiza Watendaji wa kila mtaa lazima wahakikishe kuanzia sasa wanajenga utarajibu wa kusoma taarifa za mapato na matumizi kwenye vikao kila baada ya miezi miwili.
"Kumekuwepo na malalamiko kwa watendaji kutosoma taarifa za mapato na matumizi, sasa nawagiza fanyeni hivyo kila baada ya miezi miwili. mjanua mnapofanya tabia hii ya kutosoma taarifa kwenye vikao mnasababisha mashaka ambayo pengine hata hayapo", alisema Makori.
Mkuu huyo wa wilaya alisema ni lazima Watendaji na Wenyeviti wafanye kazi kwa pamoja, lakini wapo ambao wamekuwa wakivutana lasababu kubwa ikiwa ni maslahi binasi.
"Kutokana na sababu za maslahi binafsi unakuta kuna kusigana kwa taarifa za mapato na matumizi kati ya Mwenyekiti na Mtendaji, sasa mimi nasema achaneni na mabo binafsi, fanyeni mambo yanayohusu wananchi ambayo ndiyo mkazi uliyopewa unayolipwa mshahara", alisema Makori na kuwataka Wenyeviti wanapoona mambo hayako sawa wasibaki kulalamika badala yake waitishe vikao.
Mkuu huyo wa Wilaya pia alizungumzia suala la Viongozi wa mitaa kuhakikisha wanasimama imara katika kuhakikisha hakuna ujenzi holela unaofanyika katika mitaa yao.
Kuhusu ulinzi Shirikishi, Mkuu huyo wa Wilaya alionyesha kukerwa kutokana na mitaa kadhaa katika Kata za Wilayani Ubungo kutokuwa na ulinzi Shirikishi jambo ambalo alisema limesababisha mitaa kadhaa kuwa na uharifu wa kutisha, akiyataja baadhi ya maeneo kuwa ni mtaa wa kinzudi, Goba na Muungano.
Kufuatia hali hiyo Mkuu huyo wa Wilaya amewaagiza Maafisa tarafa kuhakikisha hadi ifikapo Jumanne Wiki ijayo (siku 14), mitaa isiyo na ulinzi shirikishi iwe nao.
Akizungumzia suala la usafi, Mkuu wa Wilaya alisema, kwa sasa Ubungo kwa ujumla ipo vizuri katika suala la usafi lakini akasema pamoja na hali hiyo kuna baadhi ya mitaa bado inaendekeza uchafu, na hivyo akaagiza Wenyeviti na Watendaji wa mitaa kuhakikisha wanasimamia kikamilifu suala la usafi katika maeneo yao.
Baadhi ya Watendaji wa Kata, Wenyeviti wa Mitaa, wakuu wa Idara, Wakuu wa Vitengo, wakiwa kwenye kikao hicho kilichofanyika katika Ukumbi wa Little Folower, Mbezi Wilayani humo Jijini Dar es SalaamMkuu wa Wilaya ya Ubungo Kisare makori na meza kuu wakiwa wamesimama na Watendaji wa Kata, Wenyeviti wa Mitaa, wakuu wa Idara, Wakuu wa Vitengo, kukumbuka watumishi wengine waliofariki dunia hivi karibuni kabla ya kuendelea na kikao hicho kilichofanyika katika Ukumbi wa Little Folower, Mbezi Wilayani humo Jijini Dar es Salaam
Wakuu wa Ulinzi na Usalama wakiwa kwenye kikao hicho
Mkuu wa Tehama Ubungo, Sophia Kayambwa akijieleza kwa Mkuu wa Wilaya kuhusu mtaa wa Kinzudi kukosa mashine ya kupokelea malipo ya serikali. Akasema mashine iliyokuwepo imeharibika betri na chaja kwa siku kadhaa na vifaa hivyo imekuwa vigumu kupatikana, jambo ambalo lilimstua Mkuu wa Wilaya kwa kuwa hali hiyo inaikosesha fedha serikali. Hivyo akaamuru mashine itafutwe na kupatikana haraka.
Mkuu wa Wilaya Makori Kisare akijibu baadhi ya maswali ya wajumbe mwishoni mwa kikao hicho
Post a Comment