Na Albano Midelo, Ofisa Habari Ruvuma
Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Christina Mndeme amesema mkoa huo ulipokea zaidi ya Sh. Bilioni 9 (Sh. 9,205,781,600.28), kwa ajili ya kutekeleza sera ya utoaji elimu bila malipo katika kipindi cha mwaka mmoja kati ya Desemba 2019 na Novemba 2020.
Christina amesema fedha hizo zimesaidia kuongeza kiwango cha uandikishaji na mahudhurio ya wanafunzi katika shule za msingi na sekondari pamoja na kuongezeka upatikanaji wa vitabu vya kiada na ziada.
“Utekelezaji wa sera hii umeweza kuleta unafuu kwa wazazi na walezi katika kugharamia gharama za elimu kwa watoto wao’’, alisisitiza Mndeme.
Amesema, Mkoa umeendelea kuimarisha utoaji wa elimu katika ngazi zote na kwamba Mkoa wa Ruvuma umepata mafanikio makubwa baada ya serikali kujenga vyuo viwili vipya vya ufundi stadi VETA na kuufanya Mkoa kuwa na vyuo vitatu vya VETA.
Christina amesema hivi sasa mkoa unaweka msukumo mkubwa katika utoaji wa taaluma bora kwa kuwashirikisha wadau wote wa elimu ili kuhakikisha kila mdau anashiriki kufanikisha tendo la ufundishaji,ujifunzaji na mahudhurio ya wanafunzi shuleni.
“Kwa niaba ya wananchi, naishukuru serikali ya Awamu ya Tano chini ya uongozi wa Rais wetu Dk. John Magufuli kwa kuendelea kufanya elimu kuwa kipaumbele ambapo serikali imeamua kila Mkoa, ukiwemo Mkoa wetu kujenga shule moja ya sekondari ya wasichana ya kitaifa’’, alisema Christina.
Mkoa wa Ruvuma una jumla ya shule za msingi 808 kati ya hizo, shule za serikali ni 778 na za binafsi 30, pia Mkoa una shule za sekondari 206 kati ya hizo za serikali ni 150 na za binafsi 56.
Post a Comment