Featured

    Featured Posts

TAKUKURU YAMFIKISHA MWALIMU MKUU KIZIMBANI, KISA KULA SH. 2,000,000 ZA MOTISHA YA WALIMU WA SHULE YAKE, MWANZA

Picha ya Maktaba

Misungwi, Mwanza 

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) wilaya ya Misungwi mkoani Mwanza kwa kushirikiana na Ofisi ya Taifa ya Mashitaka imemfikisha mahakamani Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Mwanangwa Baraka Mwambipile Mwansasu (34) kujibu mashtaka ya rushwa kulingana na Kifungu cha 31 matumizi mabaya ya mamlaka.


Kwa mujibu wa Mwandishi wa Mtandao wa Dira Makini, hayo yamesemwa na Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mkoa wa Mwanza Frank Mkilanya ambaye Mtandao huo umekariri akisema kwamba  pia, Mwalimu Mkuu huyo ameshtakiwa kwa tuhuma ya kughushi nyaraka kinyume cha sheria.


Mwalimu Mkuu huyo alipandishwa kizimbani Februari 10, 2021, katika Mahakama ya Wilaya ya Misungwi na kufunguliwa kesi namba ECC. 1/2021 ili kujibu mashtaka yanayomkabili, na kwamba amepandishwa kizimbani kufuatia uchunguzi wa shauri hilo kukamilika. 


Imelezwa kwamba, Mwalimu Mkuu huyo akisomwa mashtaka na Mwendesha Mashtaka wa TAKUKURU Saida Salum mbele ya Hakimu Mkazi wa Makahama hiyo Erick Marley, ilidaiwa kwamba, mnamo mwaka 2018 shule ya Msingi Mwanangwa iliyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi mkoani Mwanza, iliingiziwa fedha kwenye akaunti ya shule na Wizara ya Elimu kiasi cha sh. 2,000,000 kwa ajili ya motisha kwa walimu kwa vile shule hiyo mwaka 2017 ilifanya vizuri katika mtihani wa darasa la saba.


Mwendesha Mashataka huyo alisema, uchunguzi wa TAKUKURU Wilaya ya Misungwi ulibaini kwamba, baada ya Wizara kuingiza fedha hizo, katika kipindi hicho cha mwaka 2018, Mwalimu Mkuu huyo aligushi muhtasari wa Kamati ya shule na kuuwasilisha kwa Afisa Elimu Kata pamoja na Afisa Elimu Msingi wa Halmashauri ya Misungwi kwa lengo la kuonesha kuwa kamati ya shule ilikaa na kuidhinisha kutolewa kwa fedha hizo kiasi cha Sh. 2,000,000 ili ziweze kutumika na  baada ya kutimiza lengo lake hilo huku akijua kuwa anachokifanya ni kosa kwa mujibu wa sheria za nchi, aliweza kutoa fedha hizo sh. 2,000,000 na kuzitumia kwa matumizi yake binafsi.


Kwa mujibu wa Mkuu huyo wa TAKUKURU mkoa wa Mwanza, Mwalimu Mkuu huyo baada ya kusomwewa mashtaka dhidi yake, alikana mashtaka yote manne na yupo nje kwa dhamana baada ya kutimiza masharti ya kuwa na wadhamini wawili na kila mmoja kusaini 'bondi' yenye thamani ya Sh. 1,000,000 na kesi hiyo itatajwa tena tarehe 25/02/2021 kwa ajili ya kusomewa maelezo ya awali.




author

Author Name

Author Description!

Get Free Email Updates to your Inbox!

Post a Comment

www.CodeNirvana.in

Magazeti Ya Leo

Copyright © Magazeti ya Leo, Habari Leo Tanzania, Mwananchi, Michuzi, mwanaspoti, nipashe, Udaku | Designed By Code Nirvana