Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dk Faustine Ndugulile akizungumza na watumishi wa wizara hiyo na wale wa Shirika la Posta nchini leo jijini Dodoma alipokua akifungua Baraza la 27 la Wafanyakazi wa Shirika hilo.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dkt. Zainab Chaula,akizungumza kabla ya kumkaribisha Waziri Dkt. Faustine Ndugulile wakati wa ufunguzi wa mkutano wa Baraza la wafanyakazi wa Shirika la Posta Tanzania, Dodoma
Posta Masta Mkuu wa Shirika la Posta Tanzania, Hassan Mwang’ombe akifafanua jambo kwa Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dkt. Faustine Ndugulile (aliyeketi katikati) wakati wa mkutano wa baraza la wafanyakazi wa Shirika hilo, Dodoma.
Baadhi ya wafanyakazi wa Shirika la Posta wakimsikiliza Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dk Faustine Ndugulile leo jijini Dodoma alipokua akifungua Baraza la 27 la Wafanyakazi wa Shirika hilo.
Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dk Faustine Ndugulile (mwenye tai nyekundu mbele) akiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa Wizara yake na Mameneja wa Posta kutoka Mikoa mbalimbali nchini.
…………………………………………………………………………………………………
Na.Alex Sonna,Dodoma
WAZIRI wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dk Faustine Ndugulile amemuagiza Posta Masta Mkuu nchini Hassan Mwang’ombe kuhakikisha anaimarisha kitengo chake cha ubunifu, utafiti na masoko ili kukuza mapato ya Shirika hilo na kuongeza ufanisi kazini.
Dk Ndugulile ameyasema hayo leo jijini Dodoma alipokua akifungua Baraza la 27 la Wafanyakazi wa Shirika la Posta nchini ambapo amewataka kuzingatia weledi na uzalendo kazini na yeyote ambaye ataenda kinyume na miongozo ya kazi basi hatosita kumchukulia hatua kali za kinidhamu.
Amesema anafurahi kuona Baraza hilo linaenda kujadili na kuweka mikakati ya pamoja ya namna gani wanaweza kusonga mbele huku akiwataka wawasilishe wizarani maazimio yote ambayo watayaazimia ili serikali iangalie namna ya kuyafanyia kazi.
Waziri Ndugulile amewataka watumishi wa Shirika hilo kongwe la Mawasiliano nchini kuacha kufanya kazi kwa mazoea huku akiwataka kuendana na kasi ya mabadiliko ya teknolojia ili kuwa wa kisasa zaidi.
” Nimeshapokea malalamiko yanayowahusu, Wizara hii ni mpya lakini taasisi zake za kisekta siyo mpya, niwatake muwe na mawazo mapya na fikra mpya ili tuweze kusonga mbele, tuongeze ubunifu, utafiti na masoko mapya tutumie rasilimali za Posta kufikia wananchi ni lazima tuingie kwenye ushindani tusibaki kung’ang’ania Telegram tu.
Mimi kama Waziri siwezi kukubali kufanya kazi za Mameneja wa Mikoa, ambaye atalala kwenye kituo chake cha kazi mimi nitambutua tu, hatutaki ufanyaji kazi wa mazoea tena, tumeaminiwa ni lazima tuitunze imani hiyo,” Amesema Dk Ndugulile.
Kwa upande wake Posta Masta Mkuu, Hassan Mwang’ombe amesema kupitia mkutano huo wa Baraza hilo
la Wafanyakazi watajadili mambo ya Msingi yenye tija kwenye Shirika lao na Taifa kwa ujumla.
” Kikao hiki ni muhimu sana kwetu, kitaleta uelewa wa pamoja na kitapunguza pia migogoro kazini, pia tumepanga kujadili maslahi ya wafanyakazi wetu na kuongeza nidhamu serikalini,” Amesema Mwang’ombe.
Post a Comment