Mbunge wa jimbo la Ilemela Mhe Dkt Angeline Mabula akiwa amembeba mtoto wa kituo cha kulelea watoto wadogo cha Forever Angels kilichopo kata ya Pasiansi,
Mbunge wa Jimbo la Ilemela akiwa katika picha na watoto wanaolelewa katika kituo cha watoto yatima cha Hisani kilichopo kata ya Buswelu
Mbunge wa Jimbo la Ilemela Mhe Dkt Angeline Mabula akiwa katika picha ya pamoja na watoto wanaolelewa katika kituo cha watoto cha Fenelisco kilichopo kata ya Ilemela,
………………………………………………………………………………………..
Wananchi wa Jimbo la Ilemela wametakiwa kumuenzi aliyekuwa Rais wa awamu ya tano Hayati Dkt John Pombe Joseph Magufuli kwa kufanya kazi kwa bidii, kudumisha amani, upendo na mshikamano huku wakimuombea na kumpa ushirikiano Rais wa sasa wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hasan ili aweze kuwatumikia vyema sanjari na kuendelea na ujenzi wa miradi mikubwa ya maendeleo na ya kimkakati.
Rai hiyo imetolewa na Mbunge wa Jimbo la Ilemela ambae pia ni Naibu Waziri wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe Dkt Angeline Mabula akisheherekea siku kuu ya kufufuka kwa Yesu Kristo maarufu kama Pasaka kwa kutembelea vituo vya malezi ya watoto Yatima na wale wenye hali duni za kimaisha vilivyomo ndani ya jimbo lake kikiwemo kituo cha Hisani kilichopo kata ya Buswelu, Forever Angels kata ya Pasiansi, Mtoto Afrika kata ya Buswelu, Fonelisco kata ya Ilemela na Foundation Karibu Tanzania cha kata ya Ibungilo ambapo mbali na kuwapongeza waanzilishi wa vituo hivyo na kuwashukuru kwa huduma wanayoitoa katika kuwasaidia watoto hao akawataka kutambua na kuenzi mchango wa Serikali na viongozi wake katika kuwaletea maendeleo ikiwemo utoaji wa elimu bure kwa watoto wanaosoma shule za msingi mpaka sekondari kidato cha nne jambo ambalo lilikuwa likichangia watoto wengi masikini kukosa huduma hiyo muhimu kwa msingi wa maisha yao
‘.. Bahati mbaya mwaka huu tunasheherekea Pasaka bila JPM, Lakini niwahakikishie Wa Tanzania bado tuko salama chini ya uongozi wa Rais Mhe Samia Suluhu, Tunachotakiwa kufanya ni kuzidi kuwaombea viongozi wetu, Na kubwa zaidi ni kuchapa kazi ..’ Alisema
Aidha Mhe Dkt Mabula akawataka watoto hao kushika neno la Mungu hasa ile Zaburi 23 huku akiwaahidi kuwatembelea tena na kutatua kero na changamoto zinazowakabili
Kwa upande wake mlezi na msimamizi wa kituo cha watoto yatima cha Hisani kilichopo kata ya Buswelu, Bwana Frednand Fredrick akampongeza mbunge huyo kwa kutenga muda wake na kuamua kusheherekea siku kuu ya Pasaka pamoja nao huku akimshukuru kwa zawadi aliyoitoa kwa watoto wa kituo chake sanjari na kuwataka viongozi wengine na jamii kwa ujumla kuiga mfano huo
Nae mtoto mwenye ulemavu wa ngozi Nuru Samuel anaelelewa katika kituo cha Hisani na Majaliwa Fredy anaelelewa kituo cha Fonelisco kwa nyakati tofauti wamezungumzia juu ya imani yao kwa Serikali katika kutatua kero zinazowakabili watoto wanaoishi katika mazingira magumu sanjari na kumshukuru Mbunge Dkt Angeline Mabula kwa kuwakumbuka na kujitoa kwake kwaajili ya jamii inayomzunguka
Post a Comment