Shirikisho la Vyama vya Magonjwa Yasiyoambukiza (TANCDA) linampongeza kwa dhati Raisi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama Samia Suluhu Hassani kwa kuweka kwenye vipaumbele vya serikali yake vita dhidi ya Magonjwa Yasiyo ya kuambukiza (NCDs).
Pia tunampongeza kwa kutambua madhila yanayowapata wagonjwa wengi wa NCDs na kuahidi kuimarisha mifuko ya bima ya afya ili itoe bima kwa Watanzania wote, jambo ambalo limekuwa ni kilio cha shirikisho kwa muda mrefu sasa.
Akihutubia Bunge la 12 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mjini Dodoma Aprili 22, mwaka huu, Rais Samia alisema Serikali yake itaweka nguvu katika kinga na tiba yakiwemo magonjwa yasiyoambukiza, ambayo yanasababisha vifo vingi na kugharimu Serikali fedha nyingi.
Sambamba na mpango huo alisema Serikali itaimarisha pia huduma za matibabu ya kibingwa na kuzipeleka huduma hizi kwenye Hospitali za Rufaa za Mikoa.
Alisema Serikali itaimarisha utoaji wa huduma za matibabu kwa wazee na kuweka mipango maalum kuhudumia makundi yenye magonjwa adimu.
Tafiti za kisayansi zinaonesha kuwa mwaka 2016, watu milioni 42, sawa na asilimia 71 ya vifo vyote duniani, walipoteza maisha kutokana na magonjwa yasiyoambukiza na pia asilimia 75 ya vifo vyote vinavyohusu watu wenye umri kati ya miaka 30 hadi 70
Magonjwa yasiyoambukiza ni magonjwa yasiyo na vimelea vinavyoweza kusambazwa kutoka kwa wanaougua kwenda kwa wengine mfano magonjwa ya moyo na mishipa ya damu, saratani, magonjwa sugu ya njia ya hewa, kisukari, kuoza meno, magonjwa ya akili na mengineyo ya kurithi kama vile siko seli.
Kwa Tanzania inakadiriwa ya kuwa magonjwa haya yanasababisha asilimia 27 ya vifo vyote na tafiti za mwaka 2012 zinaonyesha kuwa kwa kila watu 100 wenye umri kuanzia miaka 25 na kuendelea; tisa wana kisukari, 26 wana shinikizo la damu, 25wana mafuta yaliyozidi kwenye damu na 34 wana uzito ulizidi.
Zipo sababu mbalimbali zinazosababisha magonjwa haya zikiwamo za kutozingatia mitindo bora wa maisha kama vile ulaji usiofaa, kutoshughulisha mwili, matumizi ya vilevi kupindukia na matumizi ya tumbaku
TANCDA inajikita zaidi katika kuelimisha jamii kufahamu magonjwa haya kwa sababu utafiti wetu unaonesha kuwa kila mtu akifahamu kinagaubaga magonjwa haya itakuwa rahisi kuyaepuka.
Vile vile, TANCDA inaelimisha na kuhimiza wale ambao tayari wanaugua magonjwa haya kuzingatia kanuni wanazoelekezwa na wataalamu wa afya ili kuyadhibiti na kuwafanya waishi maisha marefu.
Tunatambua wazi kuwa juhudi hizi za Mama Samia amekuwa akizitekeleza tangu akiwa Makamu wa Rais katika Serikali ya Awamu ya Tano. Nakumbuka mwaka 2016, alihamasisha wananchi kufanya mazoezi ya mara kwa mara ili kukabiliana na magonjwa haya yasiyoambukiza.
Kwa kutambua kwamba magonjwa haya yasiyoambukiza ni janga linaloiandama jamii, alitangaza kila Jumamosi ya pili ya mwezi iwe siku ya kitaifa ya mazoezi. Mara kadhaa kwa nyakati tofauti alikuwa akionesha kwa vitendo ufanyaji mazoezi.
TANCDA inamhakikishia Rais kuwa itaendelea kushirikiana na Serikali katika mkakakati huu kufanikisha mipango ya maendeleo ya kujenga jamii ya Watanzania wanaoishi maisha bora.
Post a Comment