…………………………………………………………………………………………………..
Na.Alex Sonna,Dodoma.
Serikali imepanga kuhamasisha sekta binafsi kuanzisha vituo vya kutoa huduma za kukodisha zana za kilimo ili kupunguza matumizi ya jembe la mkono kutoa asilimia 53 za sasa hadi kufikia asilimia 10 ifikapo 2025.
Hayo yamebainishwa leo Machi,31,2021 Bungeni jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Kilimo Hussein Bashe wakati akijibu swali la Msingi la Mbunge wa Nkasi Kaskazini Mhe.Aida Joseph Khenani aliyehoji kuhusu Utaratibu unaotumika kuwakopesha matrekta wakulima unawasababishia hasara kwa kuwa wanatozwa riba kubwa Je, kwa nini Serikali isibadili utaratibu unaotumika sasa kuwakopesha wakulima matrekta ili kuleta tija.
Akijibu Swali hilo ,Naibu Waziri Bashe amesema , Benki ya Maendeleo ya Kilimo imetoa mikopo ya matrekta makubwa 62 yenye thamani ya shilingi bilioni 5.6 na katika kuongeza matumizi ya zana bora za kilimo na kuongeza tija katika kilimo, Serikali imepanga kuhamasisha sekta binafsi kuanzisha vituo vya kutoa huduma za kukodisha zana za kilimo kwa lengo la kusogeza huduma ya upatikanaji wa zana za kilimo kwa wakulima na kupunguza matumizi ya jembe la mkono kutoka asilimia 53% za sasa hadi kufikia asilimia 10 % ifikapo 2025.
Aidha, Naibu Waziri Bashe amebainisha kuwa Katika mwaka 2020/2021 hadi Mwezi Februari, 2021 Mfuko wa Taifa wa Pembejeo umetoa mikopo yenye thamani ya Shilingi Milioni 959.5 kati ya mikopo hiyo, mikopo ya matrekta makubwa 16 yenye thamani ya shlingi Milioni 729.5 imetolewa.
Hata hivyo Naibu Waziri Bashe amesema baadhi ya wakulima hushindwa kupata mikopo ya pembejeo kutokana na riba kubwa na masharti mengine yanayotolewa na watoa huduma hivyo kutokana na changamoto hizo, Serikali kupitia Wizara ya Kilimo imeanza kuwatambua watoa huduma wote wanaotoa mikopo ya pembejeo za kilimo ikiwemo matrekta ili kujua aina ya huduma na mikopo inayotolewa kwa wakulima katika kusaidia kutambua changamoto zilizopo na kuzipatia ufumbuzi .
Post a Comment