CCM Blog, Dar es Salaam
Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinfuzi (CCM) Daniel Chongolo amemhakikishia Makamu Mwenyekiti wa CCM mstaafu Mzee Pius Msekwa kuwa Chama kipo salama chini ya Sekreterieti anayoiongoza.
Amesema, Katiba, Kanuni, taratibu na miongozo ya Chama iliyowekwa na Waasisi wa CCM itaendelea kuheshimiwa, kulindwa na kufuatwa, na kwamba Jahazi la CCM chini ya uongozi wake halitakwenda mrama.
Chongolo ameyasema hayo, leo Ofisini kwake, katika Ofisi Ndogo ya Makao Makuu ya CCM, Lumumba jijini Dar es Salaam, alipokutana na kuzungumza na Mzee Msekwa ambapo amemuahidi pia kwamba atakitumikia, kukisimamia na kukiimarisha zaidi Chama Cha Mapinduzi.
Katibu Mkuu mpya wa CCM ameeleza kuwa mafunzo ya uongozi, utawala na siasa aliyoyapata wakati wote akiwa mtumishi kwenye Chama na Serikalini yamemkomaza na kumuandaa vyema kwa nafasi aliyoteuliwa na Mwenyekiti wa CCM, Samia Suluhu Hassan.
Amemueleza Mzee Msekwa kuwa amejifunza mengi kutoka kwa Wazee wastaafu aliobahatika kufanya kazi chini yao, amejifunza Ujasiri, kujiamini na kupata upeo na maarifa ya kutosha.
"Nakushukuru sana Mzee Msekwa, wewe na viongozi wenzako wastaafu kwa jinsi mlivyonilea. Nimechota maarifa na kujifunza mengi kutoka kwenu na kuniandaa. Nichukue nafasi hii kukuhakikishia kwa fikra zile zile, nidhamu ile ile na misimamo inayozingatia mabadiliko ya nyakati CCM kitaendelea kubaki chama bora Barani Afrika "Alisema Chongolo.
Chongolo amesema licha ya kujifunza na kupata uzoefu wa kutosha ataendelea kujifunza zaidi na kwamba atakapokwama hatosita kukimbilia kwao kwa ushauri na elimu ya uongozi.
Kwa upande wake Mzee Msekwa alisema CCM hakijawahi kumkabidhi mwanachama wake yeyote dhamana ya kuongoza hata ofisi ya tawi ikiwa mtu au mwanachama huyo hatoshi na hana vigezo. Hivyo akamuhakikishia Chongolo kuwa Mwenyekiti wa CCM na wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa wamejiridhisha kuwa anatosha.
Mzee Msekwa amemshauri aonyeshe utiifu, nidhamu na kukisimamia chama kwa uamunifu na kupokea na kuzingatia maelekezo atakayopewa na Mwenyekiti na Vikao vya Chama.
"Una wajibu wa kuhakikisha Sekreterieti yako muda wote mnakuwa na msimamo wa pamoja. Una kazi ya kutekeleza maagizo aidha ya H/kuu ya Taifa au ya Kamati Kuu ya CCM na kutekeleza", alisema Mzee Msekwa.
Katibu Mkuu wa CCM Daniel Chongolo aki,u gumza na Makamu Mwenyekiti wa CCM mstaafu Mzee Pius Msekwa Ofisini kwake, leo.
Post a Comment