***********************
Na Mwandiahi Wetu
Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Hassan Abbasi amesema Wizara rasmi inaanzisha Mfuko wa Maendeleo ya Utamaduni na Sanaa ambao utapitishwa kupitia Bajeti ya mwaka ujao wa Fedha wa 2021/2022.
Mfuko huo utakuwa maalum kwa ajili ya kusaidia wasanii kupata mitaji ambayo itawasaidia kufanya kazi zao za Sanaa kwa ufanisi na tija kwa taifa pamoja na kuwapatia mafunzo ya kuwaongezea uwezo wao wa kiutendaji.
“Bajeti ya Serikali kwa mara ya kwanza inakwenda kutenga fedha kwa ajili ya Mfuko huo ambao utakuwa mkombozi mkubwa kwa wasanii wetu, kwani wataweza kupata mitaji kwa ajili ya kufanya kazi zao za Sanaa na Kupata mafunzo ya kuongezeana uwezo” amesema Dkt. Abbasi.
Dkt. Abbasi amesema hayo wakati wa Iftari maalum ya wadau wa Habari na DSTV iliyoandaliwa na kampuni ya Multichoice Tanzania na kupewa jina la Media Showcase iliyofanyika Mei 6, 2021 Jijini Dodoma alipomuwakilisha Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Innocent Bashungwa.
Ameongeza kuwa Kampuni ya Multichoice Tanzania imefanya kazi kubwa sana na Wizara ya Habari inawashukuru kwa mchango wao ikizingatiwa ni wadau muhimu wa kimkakati kwa maendeleo endelevu ya nchi.
‘’Nawapongeza Multichoice Tanzania kwa uwekezaji mkubwa mlioufanya kwenye sekta ya Habari, nyinyi ndio baba wa teknolojia ya Televisheni nchini, kwenye eneo hili mmekuwa viongozi wazuri, mmeonesha njia kwa wengine, nawapongeza kwa kuanzisha filamu zenye maudhui ya kitanzania na zinafuatiliwa sana’’ aliongeza Dkt. Abbasi.
Dkt. Abbasi amesema Serikali itaendelea kuwaunga mkono na kuwaombea muendelee kuwekeza kwenye sekta za Wizara na kuwaahidi kuzitatua changamoto wanazopitia ikiwezekana kuzimaliza kabisa ili waendelee kufanya kazi zao.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Multichoice Tanzania Balozi Ami Mpungwe wakati akimkaribisha Mgeni rasmi Dkt. Abbasi amesema Kampuni ya Multichoice imeajiri vijana wengi Tanzania na imekuwa chanzo kizuri cha kukuza sekta ya Sanaa hapa nchini na amewaomba wadau wa Sekta ya Sanaa kuendelea kushirikiana na Multichoice ili kukuza Sanaa nchini na kuleta maendeleo.
Ameongeza kuwa vijana wengi wamekuwa wakijiunga na Chuo cha Mafunzo ya Filamu cha Akademia ya Filamu ya MultiChoice cha nchini Kenya hatua inayowasaidia kuwaongezea ujunzi ambapo wengi wamepata ajira na wamepata nafasi ya kushirikiana na waongoza filamu wakubwa kutoka nje ya Tanzania.
Shughuli hiyo Iftari maalum pia imehudhuriwa na baadhi ya Wabunge pamoja na wasanii mbalimbali wa filamu kutoka Multichoice Tanzania wanaoigiza filamu za Jua Kali, Huba na Pazia.
Post a Comment