Saa 8:33 mchana wa leo Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) lilitoa taarifa ya kusogeza mbele mechi kutoka Saa 11:00 jioni hadi Saa 1:00 usiku ikisema imepokea agizo la Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kufanya hivyo, japo haikutaja sababu.
Nusu saa baadaye Yanga SC wakatoa taarifa ya kupinga mabadiliko hayo wakisema yanakiuka kanuni inayotaka mchezo ubadilishwe muda sio chini ya Saa 24 kabla.
Yanga SC waliwasili Uwanja wa Mkapa Saa 9:30 na kufanya mazoezi ya kuamsha misuli kabla ya kurejea vyumbani kusubiri muda wa kuitwa na waamuzi kuingia uwanjani, lakini Saa 11:30 wakaondoka kurejea kambini kwao.
Baadaye Simba SC nao wakaingia uwanjani kufanya mazoezi pia kabla ya kurejea vyumbani na kisha nao kuondoka pia baada ya Saa ya Saa 1:15 usiku.
Maelfu ya mashabiki waliobaki uwanjani walianzisha vurugu kudai warejeshewe viingilio, kabla ya Polisi kutumia mabomu ya machozi kuwatawanya.
Huu ulikuwa mchezo huo marudiano wa msimu baada ya miamba hiyo kutoka sare ya 1-1 kwenye mechi ya kwanza Novemba 7, mwaka jana.
Mechi ya kwanza hapo hapo Benjamin Mkapa, Yanga SC walitangulia kwa bao la penalti la mshambuliaji Mghana, Michael Sarpong kipindi cha kwanza, kabla ya beki Mkenya, Joash Onyango kuisawazishia Simba mwishoni kipindi cha pili.
Post a Comment