Ikulu, Dar es Salasm.
Rais Samia Suluhu Hassan amewaagiza Wakuu wa mikoa, Katibu Mkuu na Watendaji Wakuu wa Taasisi mbalimbali aliowateua Mei 15, 2021 mambo makuu muhimu ya kushughulikia katika utendaji kazi wao.
Rais Samia ametoa maagizo hayo wakati wa kikao cha kazi na Wakuu wote wa Mikoa, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Watendaji Wakuu wa Taasisi za Serikali, kuwapa maelekezo wanayopaswa kuyazingatia katika utendaji wao wa kazi kwa kuzingatia sheria na utu, baada ya kuwaapisha leo, Ikulu jijini Dar es Salaam.
Katika kikao hicho cha Kazi, Rais amewataka Wakuu wote wa mikoa kuhakikisha Mikoa yao inakuwa salama, wanatenda haki kwa wananchi, wana simamia ukusanyaji wa mapato na kuhakikisha wanafuatilia utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Rais amewataka pia kuhakikisha wanasimamia ujenzi wa viwanda na uanzishwaji wa maeneo maalum ya viwanda (industrial parks) na kuwahamasisha wawekezaji kuwekeza katika fursa mbalimbali zilizopo katika Mikoa hiyo.
Upande wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Joseph Edward Sokione Rais amemtaka kuhakikisha anasimamia uimarishaji wa uhusiano na ushirikiano wa Tanzania na nchi mbalimbali duniani na kuhakikisha watumishi wa Wizara hiyo wanafanya kazi kwa kuzingatia weledi wa masuala ya diplomasia.
Kwa upande wa Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kuoambana na Rushwa (TAKUKURU) Kamishina wa Polisi (CP) Salum Rashid Hamduni na Mkurugenzi wa Mashtaka Sylivester Anthony Mwakitalu, amewataka kutekeleza majukumu yao kwa haki na kuhakikisha wanapunguza msongamano wa mahabusu waliowekwa rumande bila sababu za msingi.
Akitoaa maelekezo ya kazi Mkurugenzi Mtendaji wa Wakala wa Mabasi yaendayo Haraka (DART) Dk. Edwin Mhede, Rais amemtaka kusimamia vizuri wakala hiyo ili kuongeza ufanisi katika mradi wa mabasi yaendayo haraka kwa kuongeza idadi ya mabasi, kutengeneza yaliyoharibika na kusimamia ujenzi wa miundombinu ili kuwaondolea adha ya usafiri wananchi.
Wakuu wa Mikoa walioapishwa ni 10 ambao ni Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam Amos Gabriel Makalla, Mkuu wa mkoa wa Songwe Omary Tembeta Mgumba, Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Stephen Nzohabonayo Kagaigai na Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Balozi Brig. Jen. Wilbert Augustine Ibuge.
Wengingine mikoa yao ikiwa kwenye mabano ni, Charles Makongoro Nyerere (Manyara), Mej. Jen. Charles Mang’era Mbuge (Kagera), David Kafulila (Simiyu), Rosemary Staki Senyamule (Geita), Mwanamvua Hoza Mrindoko (Katavi) na Queen Cuthberti Sendiga ( Iringa).
Mbali na Wakuu wa mikoa, wengine walioapishwa ni Nenelwa Joyce Mwihambi ameapishwa kuwa Katibu wa Bunge, Balozi Joseph Edward Sokoine kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Kamishina wa Polisi Salum Rashid Hamduni kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU).
Wengine ni Sylivester Anthony Mwakitalu kuwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), Joseph Sebastian Pande kuwa Naibu Mkurugenzi wa Mashtaka (DDPP) na Neema Mpembe Mwakalyelye ameapishwa kuwa Naibu Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU.
Hafla hiyo imehudhuriwa pia na Wakuu wa Mikoa wengine 16 ambao tayari walikwishakula kiapo cha Ukuu wa Mkoa waliokuwa wakiuhudumu kabla ya uteuzi mpya, Makatibu Tawala wa Mikoa, Wawakilishi wa Wakuu wa Wilaya na wawakilishi wa Makatibu Tawala wa Wilaya.
Viongozi wakuu waliohuxhuria hafla ya kuapishwa kwa viongozi hao Ikulu Jijini Dar es Salaam ni Makamu wa Rais Dk. Philip Isdor Mpango, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa Majaliwa, Spika wa Bunge Job Yustino Ndugai, Jaji Mkuu Prof. Ibrahim Hamis Juma.
Pia wamehudhuria Mawaziri na Naibu Mawaziri, Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama, Makatibu Wakuu na Naibu Makatibu Wakuu, viongozi wa Dini, Viongozi wa Siasa na viongozi wa idara na taasisi mbalimbali za Serikali.
Rais Samia Suluhu Hassan akimuapisha Amoss Makalla kuwa Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Katika hafla ya Uapisho liyofanyika leo, Ikulu jijini Dar es Salaam. Picha nyingi za uapisho huo, Bofya👉 HAPA
Post a Comment