Na Jacqueline Liana, Mbeya
KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Komredi Daniel Chongolo, amesema uongozi siyo fasheni bali ni dhamana ya kushugulika kutafuta ufumbuzi wa matatizo ya wananchi.
Amesema hayo Julai 13, 2021, alipokuwa akihitimisha ziara ya kikazi katika wilaya zote za mkoa huo; kuhamasisha uhai wa chama katika ngazi ya shina na kukagua utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya CCM ya 2020-2021.
Akizungumza na viongozi na watendaji wa chama na serikali pamoja na wazee wa jijini Mbeya, katika ukumbi wa Benjamin Mkapa, mkoani hapa, Komredi Chongolo amesema uongozi ni dhamana inayoambatana na kutafuta ufumbuzi wa matatizo yanayowakabili wananchi.
Komredi Chongolo amesema kazi ya kiongozi siyo vikao na sifa ya kuitwa komredi, bali kuhangaika kutatua shida zinazowakumba watu katika maeneo yao ya uongozi.
"Viongozi wengi wanaona uongozi ni kama fasheni, ukipewa dhamana ya uongozi ni lazima utenge muda wa kushughulikia dhamana yako," alisema.
Amesema wananchi wanachotaka ni kupata huduma bora na siyo maneno.
Katika ziara hiyo, Komredi Chongolo, amesema licha ya sera na ilani kueleza kwamba watoto chini ya miaka mitano na wajawazito watapata matibabu bure, lakini wanatozwa fedha.
"Wanaofanya hivi wanakigombanisha chama na wananchi, na sisi hatuko tayari kuona chama chetu kikigombanishwa na wananchi, " ameonya Chongolo.
Katibu mkuu amesema kwamba, kama kuna sababu za msingi za watoto hao na wajawazito kutozwa pesa wanapoenda kupata matibabu katika zahanati, vituo vya afya na hospitali, hapana budi itamkwe
bayana.
"Hili tutalisimamia bila haya", alisema na kuongeza kwamba, tatizo lingine ni ukosefu wa dawa katika taasisi hizo za tiba, licha ya serikali kutoa mamilioni ya fedha ya kununua dawa.
"Tumeahidi (katika ilani) tunapeleka dawa katika kila zahanati, vituo vya afya, hospitali, lakini dawa hakuna, kuna mchwa wanaotafuna fedha za umma," alisema Komredi Chongolo.
Alisema viongozi katika ngazi zote za CCM, ni lazima na siyo hiyari, kusimamia utekelezaji wa ilani kwa sababu wao ndiyo wamiliki na watumishi wa umma watekelezaji.
Komredi Chongolo amesema, ilani isipotekelezwa watakaoulizwa ni CCM siyo wataalamu walio katika utumishi wa umma.
Komredi Chongolo amesema tatizo la ukosefu wa dawa likiachwa pasipo 'mchwa' kushughulikiwa, linaweza kusababisha uvunaji wa mabua katika uchaguzi mkuu ujao, na CCM hakiko tayari kwa hilo kutokea.
"Kuna mchwa wanaotafuna fedha, tukicheka na nyani tutavuna mabua, hatuwezi kuliacha hili kama lilivyo," Chongolo amesisitiza.
Nchini kote, ameagiza kamati za siasa za ngazi zote za chama kutembelea miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika maeneo yao.
Amefafanua kwamba kufanya hivyo kutawezesha kutambua mapema kasoro badala ya kuzijua wakati mradi umekamilika chini ya kiwango na fedha zimeliwa.
"Tusijitenganishe na miradi yetu wenyeviti na kamati za siasa, lazima mkague miradi, siyo hiyari ni lazima. Msipokuwa macho tutawakosesha haki wananchi," alielekeza Komredi Chongolo.
Komredi Chongolo amesema kwamba viongozi bora ni wale wenye kupata uchungu wanapoona wale wanaowaongoza.
"Tunataka viongozi wenye uchungu na matatizo ya wananchi, siyo wenye uchungu na mifuko yao," amesema.
Kuanzia Julai 6 hadi 13, 2021, Katibu Mkuu Chongolo, akiwa amefuatana na wajumbe wa sekretarieti ya CCM taifa, Kanali mstaafu Ngemela Lubinga, Komredi Shaka Hamdu Shaka na Komredi Kenani Kihongosi, wamefanya ziara katika mikoa ya nyanda za juu kusini; Rukwa, Songwe na Mbeya.
Post a Comment