Featured

    Featured Posts

GWAJIMA AIPONGEZA TAASISI YA MOYO (JKCI)

 
Na  Mwandishi Maalum –  Dar es Salaam

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Doroth Gwajima ameipongeza Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kuanzisha duka la dawa linalouza  dawa za kutibu magonjwa  mbalimbali na kuzitaka Hospitali zingine kuiga mfano huo.


Waziri Dkt. Gwajima amezitoa pongezi hizo  leo jijini Dar es Salaam wakati akizindua maktaba ya watoto wanaosumbuliwa na maradhi ya Moyo na saratani wanaotibiwa katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) na Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH).

Dkt. Gwajima alisema kuwepo kwa duka hilo la dawa kutawasaidia wagonjwa wanaotibiwa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI)  na Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI) badala ya kwenda kununua dawa nje ya Muhimbili watakwenda kuzinunua katika duka hilo.

“Kuna dawa ambazo hazipatikani ndani ya Hospitali , mgonjwa akiandikiwa dawa hizi na daktari analazimika kwenda kuzinunua nje ya Muhimbili . Kuwepo kwa duka hili kutawasaidia wagonjwa kupata dawa hizi ndani ya Muhimbili na kuweza kuokoa muda  wa kutembea kwenda kutafuta dawa”, alisisitiza Dkt. Gwajima.

Dkt. Gwajima pia aliipongeza compounding Unit ambao wanatengeneza dawa za watoto za moyo kutoka kidonge cha mtu mzima hadi kuwa kwenye matumizi ya watoto na kutengeneza vitakasa mikono “sanitizer” ambazo zinatumika katika Taasisi hiyo na zingine zinauzwa katika duka hilo la dawa.

“Hospitali zingine ziige mfano wa JKCI kwani kuwepo kwa duka la dawa ambalo mtu ananunua kwa kulipia na compounding unit ambao wanazalisha dawa na pamoja na vitakasa mikono kutasaidia Hospitali kuongeza kipato pamoja na kurahisisha upatikanaji wa dawa kwa wagonjwa”, alisisitiza Dkt. Gwajima.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI Prof. Mohamed Janabi alisema kabla ya kuanzishwa kwa duka hilo waliangalia ni aina gani za dawa ambazo hazipatikani MNH, JKCI na MOI na kuziweka katika duka hilo ili kuwarahisishia wagonjwa pamoja na watu wengie  kupata dawa hizo kirahisi.

“Dawa hizi pamoja na bidhaa zingine ambazo zinatakiwa kuuzwa katika duka la dawa zinauzwa kwa kulipia, mtu yeyote anafika katika duka hili na kununua dawa anazozitaka. Kuna dawa ambazo unanunua moja kwa moja bila ya kuandikiwa na daktari na kuna dawa ambazo unaandikiwa na daktari”, alisema Dkt. Janabi.

Akizungumzia kuhusu Compounding Unit Mkurugenzi wa Tiba Shirikishi  katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Delila Kimambo alisema imewasaidia katika upatikanaji wa dawa za moyo za watoto kwani dawa hizo hazipatikani kwenye soko la dawa nchini kutokana na dawa hizo kutozalishwa viwandani.

Dkt. Delila ambaye pia ni daktari bingwa wa magonjwa ya moyo alisema duka hilo la dawa limeanza kufanya kazi mwanzoni mwa mwezi Juni  na linahudumia zaidi ya watu 100 kwa siku.
author

Author Name

Author Description!

Get Free Email Updates to your Inbox!

Post a Comment

www.CodeNirvana.in

Magazeti Ya Leo

Copyright © Magazeti ya Leo, Habari Leo Tanzania, Mwananchi, Michuzi, mwanaspoti, nipashe, Udaku | Designed By Code Nirvana