********************
Na. Damian Kunambi, Njombe
Wakazi wa kitongoji cha Idusi kilichopo katika kata ya Nkomang’ombe wilayani Ludewa Mkoani Njombe wameiomba serikali kukipandisha hadhi kitongoji hicho na kuwa kijiji kwakuwa tayari kina wakazi wasiopungu 1612 sambamba na kuwa na eneo la kutosha kwaajili ya kuanzisha huduma mbalimbali.
Ombi hilo wameliwasilisha mbele ya mbunge wa jimbo la Ludewa Joseph Kamonga baada ya kufanya ziara katika kitongoji hicho na kupokea changamoto mbalimbali wanazo kabiliana nazo.
Wananchi hao wamedai kuwa maombi hayo wamekuwa wanayawasilisha kwa kipindi kirefu sasa lakini barua zao za maombi zimekuwa zikiwekwa kapuni pasipo sababu maalum.
Januari Mbawala ni mmoja kwa wananchi hao amesema kuwa kitongoji cha Idusi kina nguvu kazi za kutosha na wanahakika endapo kitongoji hicho kitapandishwa hadhi itakuwa ni rahisi kwao kupata huduma za kijamii kwa urahisi kwani kwa sasa huduma hizo wanazipata mbali.
Amesema wamekuwa wakitembea umbali mrefu kufuata huduma hizo kama zahanati, shule ambapo wanafunzi wanalazimika kutembea umbali wa km 15 hadi 20 kitu ambacho kinawachosha wanafunzi huku wajawazito wakijifungulia njiani.
“Sisi wananchi tumedhamilia kupata kijiji ili tuweze kuwa na maendeleo mpaka tunafikia hatua hii inamaana tayari tumesha jipima nguvu na uwezo na tukaona tunaweza hivyo serikali haina budi ya kulifanyia kazi ombi letu”, Alisema Mbawala.
Aidha kwa upande wa diwani wa kata hiyo John Maganga amesema ni kweli wananchi hao wanastaili kupata kijiji kwani wamekuwa wakipata tabu katika kufuata huduma mbalimbali hasa katika msimu wa mvua ambapo mto mchuchuma ukijaa basi hawawezi kuvuka upande wa pili kufuata huduma.
Amesema kuwa wananchi hao waliomba kupatiwa shule ya msingi na yeye alilifikisha suala hilo kwa afisa elimu na aliagiza ifanyike sensa ya watoto waliopo eneo hilo ambapo watoto wa darasa la kwanza mpaka la saba ni 153 na watoto miaka 0 hadi 6 wako 108.
” Mheshimiwa mbunge watu hawa wana haki ya kupewa kijiji na kujenga shule yao na zoezi hilo la ujenzi tayari wameshalianza na tofali wamefyatua za kutosha hivyo kama viongozi hatuna sababu ya kuzuia maendeleo yanayofanywa na wananchi hawa”, alisema Maganga.
Mbunge wa jimbo hilo Joseph Kamonga amesema anawaunga mkono wananchi hao katika hoja hiyo ya kupata kijiji na atawasaidia kufuatilia taratibu za kisheria zinazotakiwa kufuata katika kupata kijiji.
“Hoja hii ya kijiji naibeba na nitaiwasilisha kwa waziri wa Tamisemi Ummy Mwalimu ili aweze kutusaidia njia tunazotakiwa kutumia katika kupata kijiji na ninaamini suala hili litawezekana kwakuwa serikali ya rais Samia Suluhu ni sikivu na yenye kutekeza maendeleo”, Alisema Kamonga.
Ameongeza kuwa idadi ya watu inajitosheleza kujitegemea lakini pia madiwani wa kata tatu zinazopakana ambazo ni Nkomang’ombe, Luilo pamoja na iwela wanapaswa kukaa pamoja na kuwasilisha mawazo ya wananchi wao wa vitongoji vilivyo jirani na Idusi endapo watahitaji kuchanganywa na kufanya kijiji kikubwa
Post a Comment