…………………………………………………………………..
Na Gabriella Kibua wa Lukwangule
Dar es Salaam: RAIS Mstaafu wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete ataungana na ujumbe wa Shirika la Mapinduzi ya Kijani Afrika (AGRA) kutembelea nchi za Uganda, Zambia na Msumbiji katika kuamsha utashi wa kisiasa miongoni mwa viongozi ili kuboresha kilimo cha biashara chenye tija.
Aidha kuboreshwa kwa kilimo hicho kutasaidia kuwapo kwa usalama wa chakula na kuongeza pato la kaya.
Hayo yameelezwa mwishoni mwa wiki baada ya ujumbe wa AGRA ukiongozwa na Waziri Mkuu Mstaafu wa Ethiopia na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa AGRA, Hailemariam Dessalegn, kumtembele Rais Mstaafu katika taasisi yake ( Jakaya Mrisho Kikwete Foundation -JMKF) iliyopo mkoani Dar es Salaam.
Katika mazungumzo hayo, Rais Kikwete alitaka kusaidiwa kwa wajasiriamali ambao ni muhimu katika kufanikisha viwanda vya mnyororo wa kilimo nchini.
“Ili kuwepo na mabadiliko ya kilimo ni muhimu kwa viwanda vidogo kufahamu soko lao vyema na wao kuwekwa mstari wa mbele katika kubadili kilimo,” alisema Kikwete, ambaye pia ni mjumbe wa bodi ya AGRA chini ya uenyekiti wa Dessalegn.
Mkutano huo wa mwishoni mwa wiki pia ulihudhuriwa na Waziri wa Kilimo Profesa Adolf Faustine Mkenda, Waziri wa Biashara na Viwanda Profesa Kitila Mkumbo.
Profesa Mkumbo katika mazungumzo hayo alielezea vipaumbele vya wizara yake katika kuongeza tija kwenye kilimo na kushukuru AGRA kwa kushawishi kuondolewa kwa Kodi ya Thamani (VAT) kwa baadhi ya zana za utunzaji wa mazao baada ya mavuno.
Dessalegn na ujumbe wake uliwasili nchini Ijumaa kwa ziara ya siku tano ambapo anatarajiw akukutana na Rais Samia Suluhu Hassan kwa mazungumzo kuhusu mfumo wa chakula.
Mazungumzo hayo ni muhimu wakati bara la Afrika linajiandaa kuwasilisha taarifa yake katika mkutano wa mifumo ya chakula wa Umoja wa Mataifa baadaye mwaka huu.
Post a Comment