Featured

    Featured Posts

RAIS SAMIA AWATAKA DIASPORA KUJIANDIKISHA KWENYE BALOZI ZA TANZANIA KATIKA NCHI WANAMOISHI, AMALIZA ZIARA NCHINI BURUNDI

 Bujumbura, Burundi

Rais Samia Suluhu Hassan ametoa mwito kwa Watanzania wanaoishi nchi za nje (Diaspora), kujiandikisha kwenye Balozi za Tanzania huko wanakoishi ili iwe rahisi kwa Serikali kuwahudumia na kunufaika na fursa zinazopatikana nyumbani na pia kujiepusha na vitendo vya uhalifu kwa kuwa vinachafua jina la Tanzania


Taarifa ya Ikulu imesema, Rais Samia ameyasema hayo alipokutakana na kufanya mazungumzo na Jumuiya ya Watanzania wanaoishi nchini Burundi (JUTABU) ambapo amewashukuru kwa mapokezi mazuri tangu alipowasili nchini humo kufanya ziara ya siku mbili.


Ameipongeza Jumuiya hiyo kwa kushiriki katika shughuli mbalimbali za kijamii nchini Burundi na nchini Tanzania, ambapo JUTABU ilitoa mchango wa madawati  na kusaidia walioathiriwa wa tetemeko la ardhi mwaka 2016 na pia wakati wa kuzama kwa Meli ya Mv. Nyerere mwaka 2018.


Rais Samia amewaeleza Watanzania hao wanaoishi nchini Burundi kuwa hali ni shwari nchini Tanzania na wananchi wanaendelea na shughuli zao kama kawaida.


Amesema raia wanaoishi nje ya nchi kwa jina maarufu Diaspora ni kundi muhimu kutokana na mchango wao kwa nchi zao kama walivyo wao wanaoishi nchini Burundi na kwamba inakadiriwa kuwa, Watanzania wapatao milioni moja wanaishi katika nchi mbalimbali duniani.


Rais Samia amesema kwa mujibu wa Benki Kuu ya Tanzania, Diaspora wa Tanzania mwaka  2018 walituma nchini kiasi cha Dola za Marekani milioni 475.65, kutokana na umuhimu wao huo ndio maana Serikali imekuwa ikichukua hatua mbalimbali za kulinda na kutetea maslahi ya Watanzania waishio nje ikiwa ni pamoja na kuanzisha Kitengo cha Diaspora katika Wizara ya Mambo ya Nje.


Aidha Rais Samia amehutubia mkutano wa Jukwaa la Wafanyabiashara wa Tanzania na Burundi uliofanyika Jijini Bujumbura.


Akihutubia, Rais Samia amesema kufanyika kwa Kongamano hilo ni ishara tosha  ya kuimarika uhusiano mzuri uliopo  baina ya Tanzania na Burundi na kumuagiza Waziri wa Biashara na Uwekezaji Prof. Kitila Mkumbo kuhakikisha anashughulikia na kuondosha vikwazo vinavyokwamisha biashara kwa wafanyabiashara wa Tanzania na Burundi.


Rais Samia amemtaka Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Dkt. Leonard Chamuriho na Mkurugenzi wa Shirika la Reli Tanzania (TRC) Masanja Kadogosa kuhakikisha wanaboresha huduma za usafiri wa reli ili kuongeza usafirshaji wa bidhaa kwa Wafanyabiashara wa Burundi ili kuongeza idadi ya mizigo inayosafirishwa kwenda nchini Burundi.


Amesema takwimu zinaonyesha kuwa Kampuni 17 za Tanzania zimewekeza nchini Burundi katika sekta ya ujenzi, fedha, afya, usafirishaji na madini huku Kampuni 18 za Burundi zikiwa zimewekeza nchini Tanzania katika sekta mbalimbali.


Rais Samia amesema takwimu hizo zinaonyesha jinsi nchi mbili hizi zinavyofanya biashara kwa usawa ingawa jitihada zaidi zinahitajika kuwekeza katika maeneo mengi ambayo hayajafanyiwa kazi.


Aidha, Rais amesema ni lazima kutumia kikamilifu fursa za soko lililopo katika nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa kuzalisha bidhaa zilizoongezewa thamani.


Vilevile, ametaka kutumika kikamilifu fursa zilizopo kwenye sekta ya kilimo ili kuchochea upatikanaji wa ajira kwa vijana ambapo amesema Tanzania ina fursa nyingi ambazo wafanyabishara wa sekta binafsi wanaweza kuzitumia.


Amesema Tanzania ina takriban hekta milioni 44 za ardhi nzuri ambazo kati ya hizo hekta milioni 10 bado hazijatumiwa kikamilifu hivyo amewashauri Wafanyabiashara hao kutumia fursa ya hali ya hewa nzuri iliyopo nchini Tanzania kuwekeza katika kilimo.


Rais Samia amesema Serikali ya Tanzania imeendelea kuimarisha miundombinu ya Bandari ya Dar es Salaam, Kigoma, Kalema, Kasanga na Kabwe katika kurahisisha usafiri wa watu na bidhaa na kuwaomba wafanyabiashara nchini Burundi kuendelea kutumia Bandari za Tanzania kikamilifu.


Eneo jingine ambalo Burundi inaweza kulitumia ni huduma ya afya ambayo Tanzania imewekeza kwa kiwango kikubwa kwa kuwa na wataalam mahiri na vifaa vya kisasa, hususan vya matibabu ya moyo katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete iliyopo Jijini Dar es Salaam, hivyo amewaomba wananchi wa Burundi kuja Tanzania kupata huduma hizo.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan, akiagana na Viongozi mbalimali wa Serikali ya Burundi kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Melchior Ndadaye  Jijini Bujumbura Burundi baada ya kukamilisha ziara yake ya Kitaifa ya siku mbili Nchini humo, leo Julai 17,2021.
author

Author Name

Author Description!

Get Free Email Updates to your Inbox!

Post a Comment

www.CodeNirvana.in

Magazeti Ya Leo

Copyright © Magazeti ya Leo, Habari Leo Tanzania, Mwananchi, Michuzi, mwanaspoti, nipashe, Udaku | Designed By Code Nirvana