Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan, leo Agosti 11, 2021 amekutana na kufanya mazungumzo na Uongozi wa Chama cha Majaji na Mahakimu Wanawake Tanzania (TAWJA), Ikulu Chamwino mkoani Dodoma.
Katika mazungumzo hayo, Mwenyekiti wa TAWJA Mhe. Jaji Joaquine De-Mello amempongeza Mhe. Rais Samia kwa kushika nafasi ya uongozi na kuwa Rais wa kwanza Mwanamke nchini Tanzania.
Mhe. Jaji De-Mello amesema Chama cha Majaji na Mahakimu wanawake Tanzania (TAWJA), kinafarijika na uongozi wake kutokana na mambo mbalimbali anayofanya ikiwa ni pamoja na kuzingatia usawa wa kijinsia kwa kuongeza idadi ya wanawake katika nafasi mbalimbali za uongozi.
Amesema TAWJA iko tayari kushirikiana na Serikali katika kusimamia haki pamoja na kuhakikisha Serikali inafikia lengo la usawa wa kijinsia wa 50 kwa 50 katika ngazi mbalimbali za uongozi.
Kwa upande wake Mhe. Rais Samia amekishukuru Chama cha Majaji na Mahakimu wanawake Tanzania (TAWJA) kwa kazi nzuri inayofanya na kuahidi kuendelea kushirikiana nao katika kutekeleza majukumu yao na amepokea changamoto zao na kuahidi kuzifanyia kazi.
Wakati huohuo, Mhe. Rais Samia amekutana na kufanya mazungumzo na uongozi wa wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), ambapo Rais wa Chama hicho Profesa Edward Hoseah amesema wameomba kukutana na Mhe. Rais ili kujitambulisha na kuelezea majukumu yao.
Profesa Hoseah amesema pamoja na mambo mengine, TLS ina jukumu la kumshauri Rais, Serikali, Bunge na Mahakama katika masuala mbalimbali ya sheria na utawala bora.
Aidha, Profesa Hoseah amemhakikishia Mhe. Rais Samia kuwa TLS iko tayari kuendelea kushirikiana na kuishauri Serikali katika masuala mbalimbali ya kisheria.
Kwa upande wake Mhe. Rais Samia ameishukuru na kuipongeza TLS kwa kazi nzuri inayofanya katika kutekeleza majukumu yake ikiwa ni pamoja na kuishauri Serikali.
Mhe. Rais ameihakikishia TLS ushirikiano wa kufanya nao kazi kwa karibu ili kuweza kutimiza majukumu yake pia amepokea changamoto zao mbalimbali.
Post a Comment