Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisoma hotuba ya kuahirisha Bunge jijini Dodoma, Septemba 10, 2021. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali imeunda timu maalumu ili kuchunguza kupanda kwa bei ya mafuta kwa kuwa kitendo hicho kinawaumiza wananchi hususan wale wa hali ya chini.
Amesema Serikali imechukua uamuzi huo baada ya Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati nchini (EWURA) kutangaza bei mpya elekezi ya mafuta kwa mwezi Septemba ambapo ilionesha kupanda kwa bei za bidhaa hizo. EWURA ilitangaza bei hiyo tarehe 31 Agosti, 2021.
Amesema kufuatia tangazo hilo la kupanda kwa bei za bidhaa hizo, Septemba Mosi, 2021, Serikali ilisitisha bei mpya zilizotangazwa na EWURA ili kufanya mapitio ya kina ya kupanda huko kwa bei na siku iliyofuata iliunda timu ya uchunguzi.
“Pamoja na mambo mengine timu hiyo inafuatilia kupanda kwa bei za bidhaa za mafuta mara kwa mara hususani petroli, dizeli, mafuta ya taa na ndege na kisha itaishauri Serikali hatua stahiki za kuchukuliwa.”
Mbali na uchunguzi huo wa kupanda kwa bei, pia Mheshimiwa Majaliwa ameielekeza timu hiyo ijiridhishe kuhusu utitiri wa tozo uliokithiri kwenye bidhaa za mafuta na itoe mapendekezo ya namna nzuri ya kushughulikia suala hilo.
“Mheshimiwa Spika napenda kuliarifu Bunge lako tukufu kuwa timu hiyo tayari imeanza kutekeleza majukumu yake tangu tarehe 2 Septemba, 2021. Hali kadhalika, itakapokamilisha taarifa yake Serikali itatoa mwelekeo wa yale yatakayopendekezwa.”
Wakati huo huo, Waziri Mkuu amesema katika kukabiliana na uhaba wa vyumba vya madarasa kwa shule za sekondari, Serikali imetumia shilingi bilioni 33.73 kwa ajili ya kujenga maboma 2,699 kati ya maboma 4,539 ya vyumba vya madarasa kwenye maeneo mbalimbali nchini. Fedha hizo zinatokanana tozo ya miamala ya simu.
Mheshimiwa Majaliwa amesema katika mwaka 2021, makadirio yanaonesha kuwa wanafunzi 934,706 sawa na asilimia 83.68 ya wanafunzi 1,115,041 waliohitimu mtihani wa darasa la saba wanatarajiwa kujiunga na kidato cha kwanza ifikapo Januari, 2022.
“Mheshimiwa Spika nitumie fursa hii kuliarifu Bunge lako tukufu kwamba tayari Serikali imepeleka shilingi bilioni saba kwa ajili ya ukamilishaji wa maboma 560 ikiwa ni awamu ya kwanza. Aidha, maboma 1,840 yatakayogharimu shilingi bilioni 23 yatakamilishwa kupitia ruzuku ya Serikali Kuu.”
Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kurejea maelekezo aliyoyatoa wakati alipofungua mafunzo elekezi kwa Wakuu wa Mikoa na Makatibu Tawala wa Mikoa kwamba wahakikishe wanakamilisha kwa wakati miundombinu kwa ajili ya wanafunzi wa kidato cha kwanza.
Amesema lengo la Serikali ni kuona vijana wote waliofaulu kujiunga na kidato cha kwanza mwakani wanapokelewa na kuanza masomo yao kwa wakati. “Tangu kuanza kwa utekelezaji wa Sera ya Elimumsingi bila Ada kumekuwa na mwitikio mzuri wa mahudhurio ya wanafunzi na hivyo kuongeza idadi ya wahitimu katika mitihani ya kujipima na kumaliza elimu ya msingi.”
“Ongezeko hilo la idadi ya wahitimu, lilisababisha changamoto ya kutokuwepo kwa miundombinu ya elimu ya kutosha hususan madarasa ya kuweza kupokea wahitimu wa darasa la saba waliofaulu kujiunga na kidato cha kwanza.”
“Kufuatia hali hiyo, Serikali ilitoa maekelezo kwa watendaji wa Serikali za Mitaa kuhakikisha wanatumia takwimu zilizopo kupanga maoteo na kutenga fedha katika mipango na bajeti ya kila mwaka ili miundombinu ya elimu, samani na shule hitajika viwepo kwa wakati.”
Post a Comment