Ujumbe wa Bodi ya Nishati Vijijini ukikagua utekelezaji wa miradi ya umeme vijijini katika Kijiji cha Igalula wilayani Uyui, Mkoa wa Tabora
Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini (REB) Wakili Julius Kalolo (kushoto) akizungumza na Mwenyekiti wa Kijiji cha Igalula wilayani Uyui, Mkoa wa Tabora Athumani Ramadhani, wakati wa ziara ya Bodi hiyo mkoani humo, Septemba 8, 2021 kukagua maendeleo ya utekelezaji wa miradi ya umeme vijijini.
Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini (REB) Wakili Julius Kalolo (katikati) na Ujumbe wake, wakikagua maendeleo ya utekelezaji wa miradi ya umeme vijijini katika kijiji cha Igalula, wilayani Uyui, Mkoa wa Tabora wakati wa ziara ya Bodi mkoani humo,
Mwenyekiti wa Kijiji cha Kigwa wilayani Uyui, Mkoa wa Tabora, Hussein Kigwa (wa pili-kushoto) akizungumza na Ujumbe wa Bodi ya Nishati Vijijini (REB) wakati wa ziara ya Bodi kukagua maendeleo ya utekelezaji wa miradi ya umeme vijijini, Septemba 8, 2021. Kulia ni Mwenyekiti wa Bodi, Wakili Julius Kalolo na kushoto ni Mjumbe wa Bodi, Oswald Urassa.
Mjumbe wa Bodi ya Nishati Vijijini (REB), Oswald Urassa akishuhudia vibarua wa Mkandarasi Kampuni ya Sengerema Engineering Group Limited, anayetekeleza Mradi wa Umeme wa Ujazilizi wilayani Uyui, Mkoa wa Tabora, wakiendelea na kazi ya kutandaza miundombinu husika katika kijiji cha Kigwa. Bodi ilikuwa katika ziara ya kazi.
Ujumbe wa Bodi ya Nishati Vijijini ukikagua utekelezaji wa miradi ya umeme vijijini katika Kijiji cha Kigwa, wilayani Uyui, Mkoa wa Tabora.
Msimamizi wa Miradi ya Umeme Vijijini Kanda ya Magharibi, Mhandisi Oscar Migani akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa miradi hiyo katika Kanda yake kwa Ujumbe wa Bodi ya Nishati Vijijini (hawapo pichani), wakati wa ziara ya Bodi mkoani Tabora.
Kutoka kushoto ni Mjumbe wa Bodi ya Nishati Vijijini (REB) Oswald Urassa, Mwenyekiti wa Bodi, Wakili Julius Kalolo na Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Amos Maganga, wakiwa kwenye kikao pamoja na Wakandarasi wanaotekeleza miradi ya umeme vijijini, Mkoa wa Tabora, Septemba 8, 2021. Bodi ilikuwa katika ziara ya kazi.
……………………………………………………………………
Veronica Simba – Tabora
Serikali imewataka Wakandarasi wanaotekeleza miradi ya umeme vijijini nchini kote kuheshimu makubaliano ya utendaji kazi yaliyoafikiwa baina ya pande hizo mbili kupitia mikataba waliyosaini.
Wito huo ulitolewa na Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini (REB), Wakili Julius Kalolo wakati akizungumza na Wakandarasi wanaotekeleza miradi hiyo Mkoa wa Tabora, Septemba 8 mwaka huu.
Kikao hicho kilikuwa ni sehemu ya ziara ya Bodi mkoani humo kukagua maendeleo ya utekelezaji wa miradi ya umeme vijijini.
Wakili Kalolo aliyasema hayo baada ya kupokea taarifa ya utekelezaji wa miradi husika iliyobainisha kuwa baadhi ya Wakandarasi wanasuasua hivyo kuchelewesha kukamilika kwake, jambo lililo kinyume na mikataba yao ya kazi.
Akisisitiza, alisema Serikali kamwe haitamvumilia Mkandarasi yeyote mwenye utendaji kazi duni unaokwamisha miradi hiyo na kuwakosesha wananchi fursa ya kuboresha maisha yao kutokana na nishati ya umeme.
“Kitendo cha kukwamisha kwa kuchelewesha Mradi au kwa namna nyingine yoyote ni uhujumu uchumi. Naomba muelewe Serikali haitakubali hivyo hatutasita kuchukua hatua kwa yeyote atakayekwenda kinyume na Mkataba,” alisisitiza.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, Mjumbe wa Bodi Oswald Urassa na Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Amos Maganga walitoa onyo kwa Wakandarasi wanaozembea kuheshimu Serikali ya Tanzania kwani iko thabiti na haina mzaha katika kusimamia miradi ya kuwaletea maendeleo wananchi.
Katika hatua nyingine, Ujumbe huo wa Bodi ulitembelea maeneo mbalimbali mkoani humo ambako utekelezaji wa miradi ya umeme unaendelea na kuzungumza na viongozi wa vijiji na vitongoji ili kusikia maoni yao.
Akitoa maoni kwa Bodi, Mwenyekiti wa Kijiji cha Igalula wilayani Uyui, Athumani Ramadhani alisema wananchi katika eneo hilo wameupokea Mradi wa Umeme Vijijini kwa furaha na matumaini.
“Wananchi wameanzisha miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo mashine za kusaga. Pia tunashukuru maana umeme huu haukatiki-katiki. Ombi langu kwa Serikali wananchi wote wafikishiwe nishati hii,” alisema.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kijiji cha Kigwa wilayani Uyui, Hussein Maganga aliishukuru Serikali kwa kubuni miradi ya umeme vijijini akiielezea kuwa imekuwa yenye manufaa makubwa kwa wananchi kwani imechangia kuboresha maisha yao.
Bodi ya Nishati Vijijini inaendelea na ziara katika Mikoa mbalimbali nchini kukagua maendeleo ya utekelezaji wa miradi ya umeme vijijini.
Bodi hiyo ikiwa mkoani Mwanza Septemba 6 mwaka huu, iliagiza Mkandarasi Sagemcom anayetekeleza Mradi wa Ujazilizi Fungu la Pili A, kuandikiwa barua ya kumtaka akamilishe kazi kwa wakati vinginevyo hatua za kuvunja Mkataba wake zitachukuliwa.
Post a Comment