Featured

    Featured Posts

WANAWAKE TWPC- ULINGO WAMTAKA NDUGAI AMUOMBE RADHI RAIS SAMIA NA WANAWAKE WOTE, WASEMA KAULI YAKE NI YA KIBAGUZI DHIDI YA WANAWAKE.

Mwenyekiti wa TWPC-Ulingo Mama Anna Abdallah

 

Na Bashir Nkoromo, CCM Blog
Wanawake zaidi ya 20 kutoka Asasi ya Wanawake wenye Itikadi tofauti za Kisiasa (TWPC-Ulingo), wamejitokeza leo na kumtaka Spika Job Ndugai, kumuomba radhi Rais Samia Suluhu Hassan na Wanawake wote kwa maneno aliyoyatoa hivi karibuni ambayo Wanawake hao wamesema ni ya kibaguzi na kejeli dhidi ya wanawake.

Pamoja na kumtaka Spika Ndugai kumuomba radhiSamia na Wanawake, Wanawake hao kutoka TWPC- Ulingo. wamekiombaa Chama Cha Mapinduzi (CCM), kuchukua hatua dhidi ya mwanachama wake huyo, wakisema  mbali na kauli hiyo kuwabagua wanawake, pia amemvunjia heshima Mkuu wa nchi Rais Samia Suluhu Hassan.

Kauli hizo imetolewa na Mwenyekiti wa TWPC-Ulingo Anna Abdallah, wakati wanawake hao zaidi ya 20 walipokutana leo katika Hoteli ya Travertine, Magomeni Jijini Dar es Salaam kujadili kadhia hiyo dhidi ya Spika Ndugai na kutoa tamko lao.

"Ni wajibu wa yetu kumtetea mwanamke yeyote nchini bila kujali cheo wala chama chake na nimefurahi sana kwamba Ulingo inakutana kueleza masikitiko yake kwa kauli zilizotolewa na ndugu Ndugai hivi karibuni, akilaumu Rais wa nchi kwenda kukopa, eti anasema tozo zingetosha,” akasema Mama Abdallah.

Anna Abdallah akasema Spika Ndugai alitamka kwamba "Mama kaenda kukopa" badala ya kusema Rais, kauli ambayo alisema inamvunjia heshima Mkuu wa nchi, hivyo anapaswa kujitokeza kumuomba radhi Rais Samia na wanawake wote.

“Aliyekwenda kukopa ni Rais na iliyokopa ni nchi sio Mama, yeye mwenyewe (Spika Ndugai) aliwahi kutuambia hapendi kusikia tukisema maneno "Rais Mwanamke", sasa kwa nini Rais amekwenda kukopa yeye anasema "Mama kaenda kukopa?,” alihoji na kuongeza kuwa kauli hiyo ya Spika Ndugai inadhihirisha ni kwa namna gani asivyoheshimu wanawake, ilhali wao wanaheshimu.

“Na tamko lake la kusema "mwaka 2025" mimi sijalielewa na naomba kabisa CCM ikinyamaza isimchukulie hatua, kumjadili kwa kweli tutaona ina upendeleo, mbona wengine wanaitwa?,” alisema na kuhoji.

Mama Anna Abdallah ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Wadhamini la CCM, ameiomba Kamati ya Usalama na Maadili ya Chama imuite ili akajieleze na hatua stahiki zichukuliwe, badala ya kunyamaza kwa kuwa nguvu na nafasi aliyonayo sasa inatokana na kadi ya CCM hivyo kuchukuliwa hatua kwake, kutamfanya asiitumie vibaya nafasi yake, kwa kuwa siyo mara yake ya kwanza kutoa kauli za namna hiyo.

Kwa upande wake, Mratibu wa Asasi hiyo, Dk. Ave Maria Semakafu, alisema pamoja na ndoto ya kuwa na Rais mwanamke kutimia, lakini kumejitokeza vitendo vya kibaguzi dhidi yake.

“Tumekuwa tukishuhudia Rais wetu kila atakapohutubia wanatokea baadhi ya watu na kuanza kumjibu mitaani, tumetafakari tukaona mbona katika awamu nyingine hawa watu waliheshimu inakuaje wanajitokeza katika awamu hii?,” alisema na kuongeza kuwa kitendo hicho ni unyanyasaji wa kijinsia na kinamvuta mwanamke chini aonekane ameshindwa kuongoza vyema.

Dk. Ave Maria alibainisha kwamba, si rahisi kuacha kukemea kauli ya Spika Ndugai, kwa kuwa inatishia wanawake wengine wanaotamani kuwa viongozi baadaye na kusema huku akieleea kusikitishwa kwake na kauli ya kiongozi huyo, akisema hakatazwi kuwa na mtazamo tofauti lakini alipaswa kutumia maneno na jukwaa sahihi kueleza hayo badala ya kusahidia ubaguzi.

Alieleza kwamba si mara ya kwanza kwa Ndugai kutoa kauli za namna hiyo kwani aliwahi kusema "si lazima kwa wanawake kujinadi kila siku kwamba wanaweza kuongoza".

“Tulitaka kumjibu lakini tukasema labda kateleza ulimi, lakini mwendelezo wa matendo yake na ushiriki wake unatutia shaka na hofu na hii kauli yake ya juzi kusema kwamba "tutaona hiyo 2025", ni lugha ya vitisho.

“Tuko hapa kulaani kauli yake hiyo ya kibaguzi na yenye vitisho, sisi tunaweza kutokana na historia yetu ya malezi, lakini akitokea kiongozi wa muhimili anaturudisha nyuma inatukera,” alisema.

Alisema kuanzia leo asasi hiyo itamjibu kiongozi ama mtu mwingine yeyote atakayedhalilisha viongozi wanawake.

Disemba 27, mwaka huu katika Mkutano wa pili wa Wana Kikundi cha Mikalile Ye Wanyausi wa Jamii ya Wagogo jijini Dodoma, Spika Ndugai, alinukuliwa akisema "Juzi Mama ameenda kukopa sh. trilioni 1.3”.

Alisema kipi bora kati ya Watanzania katika miaka 60 ya uhuru kuendelea kukopa na kuwa na madeni au wabanane kujenga wenyewe bila madeni.

“Ni lini sisi tutafanya wenyewe na kwa namna gani? Tutembeze bakuli ndio heshima? Tukishakopa tunapiga makofi, sisi wa kukopa kila siku? Tukasema pitisha tozo anayetaka asiyetaka, pitisha tozo lazima tuanze kujenga wenyewe, nani atatufanyia, yuko wapi huyo mjomba, tukapitisha.

“Sasa 2025 mtaamua mkitoa waliopo sawa, waje watakaokuwa kazi yao kwenda kukopa, endapo hiyo nayo ni namna ya kuongoza nchi, hivi sasa deni letu ni trilioni 70. Hivi ninyi wasomi hiyo ni afya kwa taifa? Kuna siku nchi itapigwa mnada hii,” alinukuliwa Ndugai akisema.

Kufuatia kauli hizo, siku moja baadaye wakati wa utiaji saini Mkataba wa Ujenzi wa Mradi wa Reli ya Kisasa kutoka Tabora hadi Makutupora, Rais Samia alisema ni ngumu kutekeleza miradi ya maendeleo haraka bila kukopa.

Rais alisema katika ulimwengu, hakuna nchi isiyokopa kwani ndiyo njia rahisi na ya haraka ya kutekeleza miradi yenye manufaa kwa wananchi.

“Mradi wa matrilioni utakusanyaje za kwako, lakini kopa tekeleza nenda kalipe na wakopwaji wanakupa muda miaka 20. Ni kujua tu kujadiliana tumekopa mkopo nafuu miaka 20 unatudhuru nini? kukopa kunaharakisha maendeleo,” aliweka wazi Rais Samia

Mratibu wa Asasi ya TWPC- Ulindo, Dk. Ave Maria Semakafu,akiungumza, leo.
author

Author Name

Author Description!

Get Free Email Updates to your Inbox!

Post a Comment

www.CodeNirvana.in

Magazeti Ya Leo

Copyright © Magazeti ya Leo, Habari Leo Tanzania, Mwananchi, Michuzi, mwanaspoti, nipashe, Udaku | Designed By Code Nirvana