Featured

    Featured Posts

KANISA HALISI LA MUNGU BABA JUMAPILI HII 'KUANIKA HADHARANI MBIVU NA MBICHI' KUHUSU KALENDA SAHIHI, KUZINDUA MAJIRA NA WAKATI KABLA UHARIBIFU

Na CCM Blog, Tegeta
Hapana shaka kupanga muda, siku, mwezi, au mwaka ni jambo la lazima kwa mtu au Taifa lolote ili kufanikisha kwa uhakika malengo ya kimaisha yakiwemo ya kimaendeleo.

Ni kutokana na sababu hiyo, ndiyo maana kukawepo kitu kinachoitwa Kalenda ambayo mtu au Taifa huifuata ili kujua kipi kitangulie kufanyika na kipi kifanyike baadaye kwa kuwa zipo shughuli ambazo huhitaji kufanywa katika muda au majira maalum.


Hata hivyo jambo hili jema la kuwepo Kalenda maalum limekuwa na mkanganyiko ya ipi hasa ambayo ni Kalenda halisi inayofaa kufuatwa Duniani. Bila shaka mkanganyiko huu umetokana na mila na desturi za kawaida na za kiimani za watu na mataifa mbalimbali, hali ambayo imesababisha sasa kuwepo kalenda kadhaa wa kadhaa zinazotofautiana katika kujua ni siku ipi ya kwanza katika wiki na iitweje?

Mkanganyiko huu unaotokana na utofauti wa kinadharia ya chimbuko la Dunia ndiyo uliosababisha, baadhi ya watu au mataifa Duniani kutofautiana siku za mwanzo na mwisho wa wiki, mwezi na mwaka jambo ambalo limesababisha wakati wengine wanatambua kuwa siku fulani ni ya mapumziko ya kazi wengine wanaiona siku hiyo hiyo ni siku ya kazi na wanayo ya kwao ya mapumziko!

Katika dhana ya nadharia, kuna makundi makuu mawili ya nadharia zinazoelezea chimbuko la dunia ambapo kundi la kwanza ni la wayakinifu (materialists) linaloamini kuwa, dunia na vyote vilivyomo, vilitokea kutokana na migusano au mimeguko ya mada, mabadiliko ya viumbe, nakadhalika, kundi hili hujumuisha wanasayansi na wanafalsafa mbalimbali, hili ni kundi la wanauhalisia.

Kundi la pili ni la wadhanifu (idealists), linaloamini kuwa, dunia na vyote vilivyomo ni matokeo ya kazi ya Mwenyezi Mungu ambapo inasadikiwa kuwa Wakristo, Waislamu na Wayahudi wote duniani, wanaunga mkono nadharia hii kwa kuamini kuwa, dunia na vyote vilivyomo, viliumbwa na Mwenyezi Mungu kwa muda wa wiki moja, siku sita za kazi na moja ya mapumziko.

Kwa kuwa nadharia zote hizi (udhanifu na uyakinifu), hutumika katika kufanyia tafiti mbalimbali, hivyo napendekeza kutumia kundi la pili la nadharia ya udhanifu, kujadili kwa  ufupi historia ya kalenda ya siku za wiki kama inavyoonyeshwa na kundi hili la nadharia tangu uumbaji hadi sasa.

Mwanzo wa Kalenda ya Siku za Wiki
Kwa mujibu wa nadharia ya uumbaji, dini kubwa duniani kama vile Ukristo, Uislamu, Ahmadiyya, na Uyahudi kwa asilimia kubwa zinaamini kuwa dunia na vyote visivyoonekana na vinavyoonekana juu ya uso wa dunia vilitokana na uumbaji wa Mungu.

Kwa mujibu wa taarifa zilizopo, kwa upande wa dini ya Ubudha na Uhindu wao baadhi ya madhehebu yao, wanaamini 'uibukaji' na baadhi wanaamini 'uumbaji', Kwa kufuata nadharia hii ya uumbaji, historia inaonesha kwamba mfumo wa Kalenda ya siku saba za wiki, uliasisiwa na Mwenyezi Mungu baada ya kuiumba dunia na kuwapa wanadamu wa kale walioishi ili wauendeleze.

Bila shaka, haukuwa mfumo wa Kalenda kama ulivyo kwa siku za leo, bali ulikuwa ni utaratibu ambao jamii za kale zikiwa kwenye makazi yake, zilikuwa na utaratibu huo wa kusoma majira ya siku. Siku za wiki hazikuwa na majina rasmi isipokuwa siku moja kama utakavyoona mbele.

Inaaminika kwamba kabla ya maandishi kugunduliwa watu hao wa kale, walitumia jua, mwezi na nyota katika kusoma majira ya siku, utaratibu ambao uliendelea kwa kipindi kirefu katika jamii nyingi za wanadamu hadi maandishi yalipogunduliwa.

Kalenda ya Wasuma na Waakadi
Inaaminika kuwa jamii za mwanzo kutumia kalenda ya siku za wiki, zilikuwa ni jamii za watu wa Mesopotamia waitwao Wasuma na Waakadi ambao waliishi Kaskazini na Kusini mwa mito ya Tigrisi/Hidekeli na Frati katika nchi ijulikanayo kwa sasa Iraki mnamo miaka ya 4000 K.K. baada ya gharika ya Nuhu.

Jamii hizi za Wasuma na Waakadi zilijulikana kwa jina maarafu la mji wa sehemu waliyokuwa wanaishi  wa Babeli na hivyo jamii hizo kujulikana kama Wababeli ambao waliishi kwenye nyumba za udongo zilizokuwa zimejengwa karibu na mahekalu chini ya utawala wa Makuhani (viongozi wa dini).

Wababeli walikuwa wakitumia kalenda ya Biblia ambayo ni Kalenda ya siku saba (7) za wiki ikianzia siku ya kwanza ya wiki ambapo hadi kufikia karne ya 6 K.K. mpaka karne ya 4 B.K. mataifa mengi yaliyofuata baada ya Wababeli, (isipokuwa machache kama vile Ugiriki, Uturuki, Ashuru, Misri n.k.), yalikuwa na mifumo na kalenda ya siku za wiki tofauti na ilivyokuwa kwa Wababeli.

Kwa mfano, mataifa mengine kama vile Wamaya walikuwa na wiki za siku 13 hadi 20, Wamisiri walikuwa na siku za wiki 10, Wajapani na Wakorea walikuwa na siku za wiki 10, Waakani (Nigeria) walikuwa na siku 6 za wiki, Wayaveni (Indonesia) walikuwa na siku 5 za wiki.

Mkanganyiko huo wa kalenda tofautitofauti za siku za wiki kwa mataifa hayo, ulikuja kufanyiwa marekebisho na dola ya Rumi ilipoitawala dunia kuanzia mwaka 68 K.K hadi mwaka 538 B.K. Ndani ya kipindi hicho mnamo mwaka 321 B.K. chini ya utawala wa Mfalme Constantino I, mfumo wa siku 7 za wiki kama ulivyokuwa kwa Wababeli, ulirejeshwa tena.

Kalenda ya Wiki ya Warumi
Rumi ilipoitawala dunia, mifumo na taratibu za kalenda za siku za wiki za Babeli vilirejeshwa. Idadi ya siku za wiki ilikuwa ni ileile ya zamani, japo kwa kipindi hicho, siku zilipewa majina ya mkopo.

Pamoja na mvuto wa Rumi kwa mataifa mengi yaliyokuwa chini yake kufuata utaratibu huo wa kalenda ya siku saba za wiki, baadhi ya mataifa mengine yaliendelea na kalenda zao hadi mwanzoni mwa karine 20 B.K,  Mfano, Umoja (wa zamani) wa nchi za Kisovieti ulikuwa na kalenda tofauti ya siku za wiki, China na Japani zilikuwa na siku 10 za wiki.

Na ilipofika mwishoni mwa karne ya 20, mataifa karibu yote duniani, yalikuwa yakitumia utaratibu wa siku 7 za wiki, ambao uliokuwa ni matokeo ya jitihada zaidi za wafalme wengine wa Kirumi waliofuata baada ya Constantino.

Urejeshaji wa kalenda ya siku 7 za wiki uliofanywa na mfalme Costantino I, haukuwa tofauti na kalenda ile ya Wagiriki. Wagiriki waliziita siku za wiki kwa kutumia majina ya sayari, ambazo kwa Wagiriki, ilikuwa ni miungu iliyoabudiwa, japo ilipewa hadhi tofauti.

Kwa Wagiriki siku za wiki zilijulikana kama ‘siku za miungu’ (theon hemerai -days of the gods). Majina ya siku za wiki yalitolewa kwa kufuata hadhi za miungu yao, kuanzia mungu mkuu kuelekea mungu mdogo, Siku ya kwanza ya wiki, ilipewa hadhi ya jina la mungu mkuu wa Kigiriki. Siku ya mwisho ya wiki, ilipewa jina la mungu wao mdogo.

Mungu mkuu wa Wagiriki alikuwa ni sayari jua ambaye alipewa hadhi ya siku ya kwanza ya wiki: hemera heli(o)u: siku ya jua, Siku ya pili ya wiki waliita kwa jina la mungu wao anayefuata baada ya jua –sayari mwezi hemera selenes – day of the moon: siku ya mwezi. Siku ya tatu ya wiki iliitwa hemera Areos/ Tiw/Tyr – day of Ares: siku ya mungu wa vita.

Siku ya nne iliitwa hemera Hermu 'day of Hermes' yaani siku ya mungu hermes, mungu wa biashara, Siku ya tano iliitwa, hemera Dios  'day of Zeus' yaani siku ya mungu wa anga au mbingu (ngurumo), Siku ya sita iliitwa hemera Aphrodites 'day of Aphrodite' yaani siku ya mungu wa mapenzi na urembo na siku ya saba iliitwa hemera Khronu 'day of Cronus' ikiwa na mana ya  siku ya mungu wa kilimo na aliyekuwa mtawala wa ulimwengu wote kabla ya kuondolewa na mungu zeus.

Kwa upande wa Warumi, wao walizitafsiri maana za majina ya siku za wiki kutoka kwa Wagiriki. Majina yaliyotafsiriwa kutoka lugha ya Kigiriki kwenda Kilatini yalianza kwa mpangilio na mtiririko uleule wa lugha chanzi – Kigiriki.

Siku ya kwanza ya wiki kwa Kilatini ilitafsiriwa kwa jina la sayari jua – dies solis ( Sunday), Siku ya pili ya wiki ilitafsiriwa kwa jina la sayari mwezi dies lunae (> Monday). Siku ya tatu iliitwa siku ya sayari Mirihi – dies Martis: (Tuesday), Siku ya nne iliitwa siku ya sayari Utaridi – dies Mercurii (Wednesday), Siku ya tano iliitwa kwa jina la sayari Mshtarii – dies Jovis (Thursday), Siku ya sita iliitwa kwa jina la sayari Zuhura – dies Veneris (Friday), na siku ya saba iliitwa kwa jina la sayari Zohali – dies Saturni-(Sartuday).

Aidha, lugha zenye uhusiano na lugha ya Waingereza (Anglo-Saxon languages) nao waliiga mfumo wa uandishi wa majina ya siku za wiki kutoka kwa Warumi kama walivyofanya Warumi kutoka kwa Wagiriki. Waingereza na lugha zingine zenye uhusiano na Kiingereza nao walichukua majina ya siku za wiki kama yalivyo na kuyatafsiri yote kuanzia siku ya kwanza ya wiki hadi siku ya saba, Maana za majina ya siku za wiki kwa Kiingereza zilikuwa sawa kabisa na zile maana za majina hayo kwenye lugha ya Kigiriki na Kilatini.

Bila ya kupoteza maana za msingi, Waingereza waliyatafsiri majina ya siku za wiki, Kuanzia kwa Wagiriki, mtiririko ulikuwa kama ifuatavyo; Mpangilio na Maana za Majina ya Siku Saba za wiki Kigiriki – Kiingereza Kigiriki Kilatini Kiingereza Fasili yake; 1. hemera heli(o)u, dies solis, Sunday (sun day), siku ya mungu jua, 2. hemera selenes, dies lunae, Monday (moon day) siku ya mungu mwezi, 3. hemera Areos, dies Martis, Tuesday(Tiu or Tīw day), siku ya mungu wa vita, 4. hemera Hermu, dies Mercurii, Wednesday (Woden day), siku ya mungu mlinzi/kiongozi, 5. hemera Dios, dies Jovis, Thursday(Thor day), siku ya mungu wa ngurumo, 6. hemera Aphrodites, dies Veneris, Friday (Freia/frigus.. day) siku ya mungu frigga (mahaba), 7. hemera Khronu, dies Saturni, Sartuday(saturn day) siku ya mungu mtawala/kilimo.

Hivyo basi, pamoja na majina ya siku kubadilika kutoka kwa Wagiriki hadi kufikia kundi la lugha zenye uhusiano na Kiingereza (Anglo-Saxon languages), maana za majina hayo hazikubadilika mpaka leo.

Aidha, katika kamusi na insaiklopidia (agh. za zamani) za Kiingereza bado mpangilio na maana za majina ya siku za wiki havijabadilishwa. Bado siku ya kwanza ya wiki ni Sunday (Jumapili ya leo) na siku ya saba ni Sartuday (kwa leo Jumamosi).

Kalenda ya Wiki ya Wayahudi
Kalenda ya siku ya Wayahudi ilikuwa ikianzia machweo na kuishia machweo ya siku inayofuata. Mfumo huu wa majira ya siku ulikuwa na historia ndefu ya utamaduni wa jamii za kale za Mesopotamia, ambayo hapo zamani, ilijulikana kama Uru ya Ukalidayo.  Kalenda ya Wayahudi ni kalenda yenye historia iliyokuwa ikitumiwa na taifa la Wayahudi, kwa kufuata taratibu na misingi ya Myahudi wa kwanza – Mzee Ibrahimu.

Kalenda hiyo ilikuwa ni kalenda ya siku saba za wiki, Kwa vile ilikuwa ni mwendelezo wa kalenda ya jamii za Mesopotamia, katika kalenda ya Wayahudi, siku za wiki hazikuwa na majina isipokuwa siku moja -Shabbath. Siku zingine, ziliitwa majina kwa kuanzia na neno “yom” (wingi yamim) lenye maana ya “siku” likifuatiwa na namba kadinali za Kiebrania Rishon (~ kwanza), ~Sheni (-a pili) hadi siku ya sita, Siku ya saba iliitwa ‘shabbat’ (Sabato) kwa Kiebrania’ lenye maana ya mapumziko.

Hivyo, Kalenda ya siku za wiki kwa Kiyahudi ilikuwa ikisomeka kama ifuatavyo; Kiebrania Fasili (maana). Yom Reeshone (Rishon) – (Sunday) Siku ya kwanza ya wiki Yom Shaynee (Sheni) – (Monday) Siku ya pili ya wiki Yom Shlee´shee (Shelishi) – (Tuesday) Siku ya tatu ya wiki Yom Revee´ee (Revi’i) – (Wednesdy) Siku ya nne ya wiki Yom Khah´mee ´shee (Chamishi) – (Thursday) Siku ya tano ya wiki Yom Ha ´shee´shee (Shishi) – (Friday) Siku ya sita ya wiki Shabbat – (Saturday) Mapumziko (Sabato).

Siku ya kwanza ya wiki ilikuwa ni Yom Reeshone (Sunday), ambayo kwa leo inaitwa Jumapili katika Kalenda ya Kiswahili. Hali kadhalika, siku iliyofuata iliitwa siku ya pili na kuendelea hadi siku ya sita Yom Ha ´shee´shee (Friday) ambayo kwa leo ni siku ya Ijumaa.

Siku ilikuwa ikianza jioni hadi jioni ya siku inayofuata. Kutokana na mabadiliko ya majira, baadhi ya siku, hazikuwa na saa sawa na siku zingine ndani ya wiki na hivyo kuleta tofauti ya urefu kati ya mwaka mmoja na mwingine.

Kalenda ya Wiki ya Kiarabu
Kalenda ya Kiarabu ilianza wakati wa Hija. Kalenda hii, ilianzishwa kwa kufuata kalenda ya mzunguko wa mwezi (lunar calendar) kuanzia mwishoni mwa mwezi kuelekea mwanzoni mwa mwezi wa Hija. Ilikuwa ni Kalenda iliyoanza siku ya kwanza ya mwezi wa MuHarram, katika mwaka wa Hijrah; kipindi cha tarehe za Hija –Anno Hegirae, ambayo ilianzia tarehe 16, Julai, 622 B.K. (1 A.H), Hiki kilikuwa ni kipindi  Mtume Mohamed (s.w.s.) alichohama kutoka Makka kwenda Madina.

Aidha katika lugha ya Kiarabu, utamkaji wa majina ya siku, ulifuata mfumo huohuo wa lugha za kale za kimesopotamia ambao ulikuwa na misingi ya nasaba za lugha ya Kiebrania.  Utamkaji wa jina la siku ulitanguliwa na neno la Kiebrania ‘yom’ kwa Kiarabu “yawm” (wingi ayyām) lililokuwa likimaanisha ‘siku’.

Imegundulika kwamba, katika kalenda ya Kiarabu, majina yote ya siku za wiki, yaliandikwa kwa kutumia namba za kadinali zikitanguliwa na neno “yawm”. Mfumo na mpangilio wa majina ya siku ulikuwa sawa na ule uliokuwa ukitumiwa na Wayahudi.

Mpangailio na maana za majina ya siku ya wiki kwa Kiarabu vilionekana kama ifuatavyo;  Yawm Al-Aad – (Sunday) Siku ya kwanza Jumapili, Yawm Al-Ithnayn- (Monday) Siku ya pili Jumatatu,  Yawm Ath-Thulaathaaʼ – (Tuesday) Siku ya tatu Jumanne, Yawm Al-Arba’aa’ – (Wednesday) Siku ya nne Jumatano, Yawm Al-Khamīs –(Thursday) Siku ya tano Alhamisi. Yawm Al-Jumu’ah – (Friday) Siku ya sita Ijumaa, Yawm As-Sabt – (Saturday) Siku ya Sabato Jumamosi (mapumziko),

Inaonekana kuwa, kalenda ya Kiarabu, ilitumia mfumo na mpangilio wa majina ya siku sawa na ule wa Wababeli na Wayahudi. Aidha, ikumbukwe kwamba, hadi kufikia mwaka 1582 B.K., kalenda ya siku saba za wiki kwa Warumi (chini ya utawala wa Gregori I) ilikuwa ikitumiwa na mataifa mengi sana duniani. Hadi sasa, mataifa mengi, yamekuwa na mfumo wa siku saba za wiki, sawa na ilivyokuwa hapo zamani kabla na baada ya kugunduliwa kwa maandishi.

Kalenda ya Wiki ya Waswahili
Katika utamaduni wa Waswahili, majina ya siku yamekuwa na changamoto kubwa sana. Ikumbukwe kwamba, asili ya lugha ya Kiswahili ni lugha za kibantu; pamoja na kwamba kuna maneno kutoka lugha zingine za kigeni kama vile Kiingereza, Kijerumani, Kihindi, Kireno, Kiajemi, Kiarabu n.k. Lugha hizi pia zimekuwa na mchango mkubwa sana katika kuongeza idadi ya misamiati katika lugha ya Kiswahili kama ilivyo kawaida ya lugha zingine duniani.

Mpangilio na majina ya siku za wiki katika kalenda ya Waswahili, kwa mara ya kwanza uliasisiwa na wanaleksikografia wazungu mnamo miaka ya 1930. Wanaleksikografia hawa walikuwa ni miongoni mwa wajumbe wa kusanifu lugha ya Kiswahili katika kamati ya lugha ya Afrika ya Mashariki enzi za ukoloni.

Katika utafiti wa majina ya siku kwa lugha ya Kiswahili, maandishi awali yanaonesha kuwa, majina ya siku za wiki kwa Kiswahili hayaoneshi usuli wala chanzo halisi cha majina hayo.

Kamusi awali zilionekana kuorodhesha majina hayo bila ya kutoa maelezo ya kutosha ya kumsaidia msomaji. “Siku za wiki ni Jumamosi – Saturday, Jumapili –Sunday, Jumatatu – Monday, Jumanne –Tuesday, Jumatano – Wednesday, Alhamisi – Thursday – Ijumaa- Friday”.

Baadhi ya majina hayo, hayana maana bainifu na wala hayaoneshi usuli wake kiasi cha kuingizwa kwenye usanifu wa lugha ya maandishi. Aidha, taarifa za msingi za mtunga kamusi yeyote, daima hufanyiwa utafiti kutoka katika lugha ya maandishi kwa kiasi kikubwa, pamoja na kwamba, lugha ya mazungumzo nayo huwa na sehemu fulani kama vile katika masimulizi ya aina ya makala, hotuba na taarifa zilizokwishaandikwa kwa ufasaha na usanifu wa lugha yenyewe.

Lugha andishi hupewa kipaumbele zaidi kwa sababu, lugha hiyo huwa sanifu na kwa kiasi kikubwa, hufuata kanuni zote za kisarufi kuliko lugha ya mazungumzo. Misamiati mingi inayotumika katika lugha andishi, mara nyingi huandikwa kwa kuzingatia taratibu za usanifu wa lugha husika.

Kwa kufuata kanuni za uingizaji wa vidahizo katika kumusi, kuna maswali mengi yanayohitaji majibu kuhusu majina ya siku za wiki katika lugha ya Kiswahili, mpangilio wake pamoja na maana za majina hayo. Kwa mfano, chanzo cha neno ‘juma’ kwa majina hayo, linatokana na lugha ya Kiarabu “gum’ah” au “jum’ah” lenye maana ya jamaa/jamii au kusanyiko la watu wengi kwa ajili ya ibada.

Aidha, neno juma katika utamaduni wa Mswahili, humaanisha jina la mtu aghalabu mwanaume, Inaonekana kuwa, neno juma kupewa maana ya wiki (siku ya saba) liliwekwa bila kuzingatia misingi ya uandishi wa kamusi; kwa maana kwamba, msingi na maana ya neno hilo ni la mkopo, hivyo neno lolote linapokopwa kutoka lugha moja kwenda lugha nyingine halipaswi kubadilishiwa maana yake ya msingi.

Hii ni kwa sababu, neno hilo huandikwa kwa kuzingatia umbo na utamkaji wake wa asili japo hufanyiwa marekebisho kidogo ya umbo na matamshi katika lugha lengwa bila ya kuharibu maana yake ya asili, Hivyo basi, imethibitika kuwa, hakuna uhusiano wowote wa jina la siku kuambikwa neno au kiambishi awali ‘juma’ likifuatiwa na namba kadinali kama yalivyo baadhi ya majina ya siku katika lugha ya Kiswahili kwa sasa; Jumamosi, Jumapili, Jumatatu, Jumanne na Jumatano.

Tukirejea kuangalia maana ya neno ‘juma’, lenye maana ya -jamaa, jamii au kusanyiko la watu wengi; na kisha kuliambika neno -namba kadinali ili kuwa jina la siku, maana itakayopatikana kwa jina hilo la siku ni dhana tofauti na maana halisi ya jina la siku.

Kwa mfano neno ‘mosi’ likiambikwa ‘juma’ kama kiambishi awali, neno tutakalopata ni jumamosi, ambalo litakuwa na maana ya mwanaume mmoja anayeitwa Juma (mosi =moja na juma = jina la mtu mwanaume), Jamaa/jamii moja au kusanyiko moja la watu*. Jumapili, litakuwa na maana ya wanaume wawili wanaoitwa Juma, jamaa au jamii mbili au makusanyiko mawili ya watu*. Jumanne, Jumatano na kadhalika, maana hizo, hazipo kikamusi.

Ni ukweli usiopingika kwamba, maana halisi na za msingi kwa maneno Jumamosi, Jumapili, Jumatatu, Jumanne na Jumatano, hazipo kabisa katika muktadha sahihi wa matumizi yake kikamusi na hivyo kubakia kwenye matumizi yasiyo sahihi ya misamiati yenye maana tofauti na inavyotumika.

Changamoto nyingine kubwa ni kuhusu mpangilio wa siku za wiki katika lugha ya Kiswahili, ambao unaonekana kuwa na mkanganyiko kwa kiasi fulani. Jina la siku kwa Kiswahili, Mpangilio wake. Jumamosi Siku ya 1 ya wiki, Jumapili Siku ya 2 ya wiki, Jumatatu Siku ya 3 ya wiki, Jumanne Siku ya 4 ya wiki, Jumatano Siku ya 5 ya wiki, Alhamis Siku ya 6 ya wiki, Ijumaa Siku ya 7 ya wiki.

Huo ndiyo mpangilio wa siku za wiki katika kalenda ya Waswahili, Siku ya kwanza ya wiki, huanzia na Jumamosi na kuishia na Ijumaa. Mpangilio huu wa siku una changamoto nyingi, Miongoni mwa changamoto hizi ni pamoja na hizi zifuatazo; Kwanza, mapumziko ya mwishoni mwa wiki katika kalenda ya Waswahili, yako mwanzoni mwa wiki tofauti na kalenda zingine za mataifa mengine duniani kama tulivyoona huko nyuma.

Mpangilio huu uko tofauti sana na wanaleksikografia wengi duniani wanaounga mkono hoja ya kuwa na mapumziko baada ya kazi mwishoni mwa wiki tofauti na ilivyo katika kalenda ya wiki katika lugha ya Kiswahili.

Aidha, mtiririko huu, bado unawapa changamoto wataalamu na watumiaji wa kamusi za Kiswahili wanapokuwa na mitazamo kinzani ya mtiririko wa siku za wiki –siku ya kwanza hadi ya saba, Ni ipi siku ya kwanza, pili, tatu na hadi ya saba ya wiki katika utamaduni wa Mswahili? Mpaka sasa, kuna mvutano wa kimtiririko wa siku za wiki, japo majina na maana zenye ukakasi zikiendelea kubaki zilezile.

Pili, siku ya sita katika kalenda ya Waswahili ni Alhamisi. Neno alhamisi, linatokana na neno la Kiarabu, Al khamsah lenye maana ya ‘-a tano’. Swali la kujiuliza, mtu anawezaje kutoka siku ya tano – Jumatano na halafu akaenda siku hiyohiyo ya tano (Alhamisi) japo kwa jina tofauti?

Hii inaonesha kuwa, kalenda ya Waswahili ya siku za wiki, ina siku mbili zenye jina moja lenye maana ileile japo linatamkwa na kuandikwa tofauti -Jumatano na Alhamisi, yote haya, yana maana ya –a tano (siku). Hii ni changamoto ambayo inapaswa kutafutiwa ufumbuzi maalumu.

Tatu, ndani ya kalenda hii, hakuna siku ya sita ya wiki kama ilivyo kwa kalenda za mataifa mengine, Waswahili wana siku ya kwanza hadi ya nne. Siku ya tano kimaana, ziko mbili na halafu baada ya hapo, wana siku ya saba tu, Kimaandishi, inaonekana kama kuna siku ya sita (Alhamisi), lakini kimaana ni siku ya tano, na hivyo kutokuwa na siku ya sita kwa maana ya jina.

Nne, siku ya Ijumaa inayoonekana kuwa ni siku ya Saba katika kalenda ya Waswahili, nayo ina mkanganyiko mkubwa wa kimaana. Ijumaa ni neno lenye, asili ya neno-kitenzi katika lugha ya Kiarabu – (jamaa), likiwa na maana ya kukusanyika, kukutana au kujumuika pamoja.

Waswahili walilitohoa neno 'Al-Jumu’ah' na kuliandika kama Ijumaa – (Friday) –siku ya kukusanyika, kukutana au kujumuika pamoja na aghalabu katika ibada ili kuifanya siku hiyo iwe ni siku ya mwisho wa wiki. Pamoja na kuifanya siku ya Ijumaa kuwa ni siku ya Saba kwa kufuata kalenda ya Waswahili, bado kuna mkanganyiko mkubwa kimtiririko na kimaana katika majina ya siku za wiki katika kalenda hii.

Tano, pamoja na siku za Alhamisi na Ijumaa kuwa ni siku za mapumziko katika siku za nyuma kwa mataifa mengi ya Kiislamu, hadi kufikia karne ya 21 kuna mataifa mawili tu, Irani na Afughanistani yanayoiadhimisha Alhamisi kama nusu siku ya mapumziko na Ijumaa kama siku nzima ya mapumziko.

Mataifa mengi yenye itikadi za namna hizo, yameshafuata mfumo na utaratibu wa mapumziko ya siku za mwisho wa wiki –Jumapili na Jumamosi pamoja na kwamba, Ijumaa ni siku ya makutano ya ibada kwa mataifa hayo.

Kanisa Halisi yatoa jibu
Kwa kuwa inaonyesha kuwa kalenda nyingi zilizopo zimetengezwa kulingana na mahitaji ya waliozitengeneza au tunaweza kusema ni kalenda za 'kujitungia' na siyo zinazofuata majira ya kalenda ya Mungu mwenyewe kwa kuwa Mungu ndiye aliyeweka Chimbuko la Dunia, jitihada zimeefanywa na baadhi ya watu wenye kiu ya kuona Kalenda inayotambulika ni ile itokanayo na Mungu mweneyewe.

Katika jitihada hizi, lipo Kanisa moja  ambalo, linaonekana kuwa na kiu hii ya kuona watu wanaiendea na kuitambua vema Kalenda ya Mungu mwenyewe aliyeweka chimbuko la Dunia, Kanisa hili linaitwa Kanisa Halisi la Mungu Baba, lipo jijini Dar es Salaam, likiwa na Makao yake Makuu, Tegeta Namanga.

Kiongozi Mkuu wa Kanisa hili lenye mamia ya vituo ndani na nje ya Tanzania, anayetambulika kwa jina la Baba Halisi, katika jitihada zake bila shaka kwa kufunguliwa na Mungu Baba ametoa andiko linachambua na kufafanua kwa kina ni Kalenda ipi hasa inayopaswa kufuatwa na watu wote Duniani ili kukidhi ile iliyowekwa na Mungu Baba mwenyewe.

Katika andiko hilo ambalo Kanisa Halisi italizindua rasmi Jumapili ya Januari 30, 2022 (26 KISLEU, 1) katika Ibada itakayofanyika Makao Makuu ya  Kanisa hilo, ni Majira (kalenda) ya wakati kabla ya uharibifu, ambapo katika maandiko aliyoandika Baba Halisi katika Kitabu cha uzinduzi huo, ametoa hoja mbalimbali zenye mashiko kuonyesha kuwa Majira au Kalenda yenye mfumo wa chimbuko la Mungu Baba mwenyewe inapaswa kuwaje na ni ipi.

Baba Halisi anaadika katika Kitabu hicho kwamba kila mtu anapaswa kufahamu kuwa wiki ina siku saba (7) na mwezi una siku ishirini na nane (28), ikiwa na maana  kwamba mwaka ni lazima uwe na siku mia tatu thelathini na sita (336), kwa maana ya Miezi kumi na mbili (12) mara 28, akirejea yaliyoandikwa katika Isaya 33:6. Katika mstari huu wa Isaya 33:6; ambako kitabu kimeandika kuwa ni Majira Imara; yenye Wokovu tele na ni majira ya kumcha Muumba wa kila kitu ambaye ndiye chanzo halisi.

"Ofisi zote mjini, ziwe za umma au za sekta binafsi mshahara unaolipwa ni wa siku 28 tu. Hata likizo ni siku 28 tu. kina mama wakiwa na watoto tumboni, madaktari (gynechologists), huwa wanahesabu siku siyo miezi ili wasichanganye na nyongeza nitakayoonyesha hapo mbele kidogo.

Mwaka 1582, dunia ilianzisha majira ambayo inanyongeza ya siku tatu (3) katika mwezi, yaani siku ya 29, 30 na 31. Siku hizo tatu zinasababisha tuwe na mwezi wa kumi na tatu (13) kila mwaka badala ya miezi kumi na mbili (12) kama tunavyosoma katika Esta 3:7!", ameandika Baba Halisi katika kitabu hicho.

Sasa kwa kuwa Baba Halisi ameandika hoja nzito kwenye Kitabu hicho, haitapendeza kumtafsiri, badala yake tunakuwekea andiko lote kama lilivyotufikia kutoka kwake na bila shaka mpenzi msomaji wetu, utamuelewa, tafadhali soma andiko hilo, Hapo👇

Utangulizi.
Sisi wote TUNAFAHAMU kuwa wiki ina siku saba (7) na mwezi una siku ishirini na nane (28), hii ikiwa na maana  kwamba mwaka ni lazima uwe na siku mia tatu thelathini na sita (336), kwa maana ya Miezi kumi na mbili (12) mara 28, yaani Isaya 33:6. Katika mstari huu wa Isaya 33:6; kitabu kimeandika kuwa ni Majira Imara; yenye Wokovu tele na ni majira ya kumcha MUUMBA WA KILA KITU ambaye ndiye CHANZO HALISI.

Ofisi zote mjini, ziwe za umma au za sekta binafsi mshahara unaolipwa ni wa siku 28 tu. Hata likizo ni siku 28 tu. kina mama wakiwa na watoto tumboni, madaktari (gynechologists), huwa wanahesabu siku siyo miezi ili wasichanganye na nyongeza nitakayoonyesha hapo mbele kidogo.

Mwaka 1582, dunia ilianzisha majira ambayo inanyongeza ya siku tatu (3) katika mwezi, yaani siku ya 29, 30 na 31. Siku hizo tatu zinasababisha tuwe na mwezi wa kumi na tatu (13) kila mwaka badala ya miezi kumi na mbili (12) kama tunavyosoma katika Esta 3:7!
 
Mjini ziko ofisi ambazo hulipa mshahara wa mwezi wa kumi na tatu (13) (Thirteenth month’s salary). Ingawa Kimataifa jambo hili halijulikani kwa wengi. Matokeo yake ni kwamba, mtu akiwa na miaka 12, kumbe ana miaka 13; akiwa na miaka 24, kumbe ana miaka 26; akiwa na miaka 36 kumbe ana miaka 39, akiwa na miaka 48, kumbe ana miaka 52, na akiwa na miaka 60, kumbe ana miaka 65, nakadhalika!

Hiyo miaka ya ziada ambayo mtu haijui na haihesabu ndiyo hubeba: uzee, magonjwa. madhaifu, nakadhalika. Maana hakuna kitu kinaweza kuwepo bila majira inayokitunza na inayosababisha kitokee. Kwa hiyo, dunia na Ulimwengu ilibidi watafute majira ya kubeba madhaifu, uasi na uovu ili visiachane na mtu.

Hii ni kinyume na kilichoandikwa kuwa majira itafika watendao kwa haki lazima wawe na raha (Isaya 14:3):
1. Katika Isaya 11:7-9, iliandikwa kuwa, itakuja majira ambayo Wanyama wakali kama vile Simba na Chui watakula majani kama ng’ombe na kulisha pamoja.

Aidha, katika mistari hiyo iliandikwa kuwa mtoto atacheza na nyoka mkali hatamdhuru kwa kuwa ni majira kabla ya uharibifu kutokea. Haya yameandikwa pia katika Isaya 65:24-25 kuwa ni lazima yatokee katika MLIMA WA CHANZO HALISI. Mlima unaozungumzwa hapa siyo kama Mlima Kilimanjaro au Meru, bali ni Ufahamu mkubwa kuliko ule wa majira zilizopita.

2. Katika Isaya 2:4, iliandikwa kuwa majira itafika ambayo hakuna taifa litainuka kupigana na taifa lingine tena. Maana silaha zote zitageuka kuwa majembe ya kulimia na mundu wa kukatia majani ya kulisha ng’ombe. Majira hiyo ni hii ya kabla ya uharibifu.

3. Katika Ufunuo 21:1-3 iliandikwa kuwa dunia (Bahari) itatoweka yaani kila aina ya uharibifu kinyume utatoweka naye CHANZO HALISI atakuwa na maskani katikati ya watu na wanadamu! Hii ina maana ya utimilifu wa Isaya 57:15, ambayo inasema kuwa alitamani siku nyingi kuishi ndani ya moyo wa kila mmoja anayetenda kwa haki. Sasa imetokea. Uwe Kanisani, usiwe Kanisani, maadamu unatenda kwa Haki; CHANZO HALISI anaishi ndani ya Moyo wako na ndiye aliyeweka wazi hii majira kabla ya uharibifu.

4. Katika I korintho 15:24, 28, iliandikwa kuwa akili za mtu zitakapofika mwisho, MUNGU BABA, ambaye ndiye CHANZO HALISI, atarejeshewa: ufalme; mamlaka; utawala na nguvu ili yeye ndiye awe yote katika wote. Hiki ni kipindi cha hii majira kabla ya uharibifu.

5. Katika Isaya 65:17, iliandikwa kuwa CHANZO HALISI ataumba Mbingu Mpya na Nchi Mpya ikiwa na maana ya Mbingu Halisi na Nchi Halisi, ambayo mambo ya zamani (mabaya), hayatakumbukwa wala kuingia ndani ya moyo. Mstari huu hauna tofauti na ule wa Yeremia 50:20 ambao unasema kuwa itafika majira tutatafuta dhambi, uasi na uovu ndani ya Kanisa, jamii na taifa wala hatutaviona. Ndiyo hii majira ya kabla ya uharibifu.

KWA NINI MAJIRA HII IANZIE TANZANIA?
Kinachosumbua wengi ni kwanini majira kabla ya uharibifu ianzie Tanzania ndipo iende katika mataifa mengine! Watu wengi wanasahau kilichoandikwa katikaIKorintho 1:26, kuwa CHANZO HALISI huinua vinyonge kuaibisha vile vyenye nguvu!

Wengi wanaiona Tanzania iko chini kiuchumi na kiufahamu, ila CHANZO HALISI yeye aliikusudia iwe kama tunavyoiona ili apate mahali pa kufikia kisha aenee katika mataifa mengine.

Wengi wamechelewa kupokea ufahamu ulioanzia Tanzania kwenda katika mataifa mengine kwa kuwa walikuwa wanapenda CHANZO HALISI ashukie kule ambapo maendeleo ya kiuchumi yanaonekana kuwa juu zaidi kama vile Amerika; Ulaya na Asia. CHANZO HALISI amechagua Tanzania, Afrika kwa sababu ya kanuni ya Isaya 57:15.

Mwaka 2003, ilisikika Sauti Kuu ya Sita kule Kigoma Tanzania, Mwaka 2015 ilisikika Sauti Kuu ya Saba kule Kigoma Tanzania, Mwaka 2019 pia ilisikika Sauti Mpyakule Kigoma Tanzania ambayo ni zaidi ya zile Sauti Saba, zilizotangulia kusikika, Mwaka 2020 ilisikika Sauti ya Moyo ambayo ndiyo ilikuja kutimiza IKorintho 15:24,28.

Hivyo, tukubali kuwa CHANZO HALISI ameshukia Tanzania na ndiye aliyeleta majira kabla ya uharibifu kupitia Tanzania.

KWANINI TUNAIZINDUA HII MAJIRA?
Hakuna kitu kinachoweza kufanyika bila majira na wakati. CHANZO HALISI, alikuja na majira yake, tuipokee na tuiishi. 12 Kisleu, 1 (16 Januari, 2022) tulimketisha kwenye Kiti cha Amani, ilikuwa ni lazima tuizindue majira yake akiwa sasa anaishi ndani yetu kwa mujibu wa Isaya 57:15.

Mtume Petro katika 1Petro 1:10-13, aliuliza kuwa mambo haya mema na mazuri yatatokea lini?Akaelezwa kuwa siyo katika kipindi chake bali ameonyeshwa tu ili kuwajulisha kwa maandishi watakaoishi kipindi hiki, wajue kuwa yatakayotokea yalishakusudiwa na CHANZO HALISI. Majira imefika sasa tunazindua majira na wakati kabla ya uharibifu.

Ukisoma Kutoka 12:1-2 na Kutoka 23:15, unagundua kuwa kabla ya Musa, kulikuwepo na Majira ambayo inampangilio tofauti na Abibu hadi Adari, kama tunavyoisoma katika Esta 3:7. Maana anasema kuwa Mwezi Abibu ambao Wana wa Israeli walitoka utumwani ndio uwe wa kwanza katika miaka yao. Hii ina maana kwamba kabla ya kutoka Misri, mpangilio wa miezi haukuwa hivyo.

Hiyo Abibu hadi Adari iliyoanza wakati wa Musa, ilipofika Mwaka 1582, iliibiwa na dunia, kwa kuwa katika majira saba hakuna chochote ulichokuwa unafanya ambacho hakikutani na mauti. Matokeo yake wanaotenda kwa haki wakabaki hawana majira sahihi.

Kwa mantiki hiyo, ilikuwa ni lazima turejee kwenye majira kabla ya uharibifu kwa kuwa majirailiyokuwepo ni ile ya Muhubiri 9:11-, ambayo inasema kuwa: siyo wenye mbio washindao kwenye michezo; siyo hodari washindao vitani; siyo stadi ambao hupata upendeleo, na kadhalika. Tumefikaje hapo; angalia:

i. Mwanzo 1:1 ndipo kulitokea kwa mara ya Kwanza, Siku ya kwanza; Wiki ya kwanza; Mwezi wa kwanza na Mwaka wa kwanza, ila miaka iliendelea kubadilika. Hiki ni kipindi ambacho CHANZO HALISI aliachilia Moyo wa Mwanzo kwa mara ya kwanza kwa ajili ya uumbaji (Methali 3:16).

ii. Mwanzo 9:1-4 kulitokea tena kwa mara ya pili, Siku ya kwanza; Wiki ya kwanza; Mwezi wa kwanza na Mwaka wa kwanza na miaka iliendelea kubadilika. Hiki ni kipindi cha baada ya gharika ya Nuhu.

iii. Mathayo 2:1-15 kulitokea kwa mara ya tatu, Siku ya kwanza; Wiki ya kwanza; Mwezi wa kwanza na Mwaka wa kwanza, miaka ikaendelea kubadilika kama nyakati zilizotangulia. Hiki ni kipindi Yesu alipozaliwa, wataalamu wa historia wakaandika Before Christ na After Christ.

iv. Isaya 41:2, 4 kulitokea kwa mara ya nne, Siku ya kwanza; Wiki ya kwanza; Mwezi wa kwanza na Mwaka wa kwanza. Hii ilikuwa 28 Februari 2012 wakati wa Eliya Adamu wa Pili aliyepokea sauti ya sita Kigoma mwaka 2003.

Hii ilikuwa kurejesha Majira ya Mungu wa majira saba iliyoibiwa na dunia mwaka 1582. Mpaka inarejeshwa mwaka 2012 ilikuwa ni miaka 430, pamoja na hayo miaka iliendelea kubadilika.

v. Isaya 59:20 kulitokea kwa mara ya tano, Siku ya kwanza; Wiki ya kwanza; Mwezi wa kwanza na Mwaka wa kwanza. Kipindi ambacho mkombozi alikuja Sayuni kwa walioacha maasi mwaka 2018. Tofauti ya majira iliyopatikana Mwaka 2012 na mwaka 2018 ni kwamba wakati wa 2012 ilirejea Abibu mpaka Adari (Esta 3:7) kama Musa alivyokuwa amepewa kwa mujibu wa Kutoka 23:15.

Lakini wakati wa 2018 mkombozi alikuja mwezi Kisleu ambao kwa Musa ilikuwa ni Mwezi wa tisa, lakini kwa Mkombozi Halisi ni Mwezi wa kwanza; maana kwa mujibu wa Kutoka 12:1-2, mwezi ambao Mkombozi amewakuta ndio unakuwa mwezi wa kwanza kwenu mliokombolewa.

Wote tuelewe kuwa hata wakati wa Musa, Abibu haikuwa mwezi wa kwanza kwao, ila ni kwa kuwa Mkombozi kipindi kile aliwatoa utumwani Misri, ndio ikaamriwa Abibu uwe mwezi wa Kwanza kwao. Jambo kubwa hapa ni kwamba bado miaka iliendelea kubadilika.

vi. Isaya 65:17; Isaya 66:22; Ufunuo 21:1-3 na 2 Petro 3:13 kulitokea kwa mara ya sita Siku ya kwanza; Wiki ya kwanza; Mwezi wa kwanza na Mwaka wa kwanza na safari hii miaka haitabadilika tena itakuwa moja tu (Zekaria 14:9).

Hii ina maana tumeupata Utimilifu wa Mduara wa Majira Moja Halisi ndani ya Mbingu Halisi na Nchi Halisi. Kama unavyofahamu namba sita ni uumbaji kwa maana ya Mwanzo 1:31 hivyo kila kitu kimekuwa chema. Kwa kuwa huu mwaka wa Kanisa umeanzia hapa Tanzania ina maana Moyo ule unaomjua Aliyeumba kila kitu (Kanisa la Kweli) uko hapa. Kumbuka mara zingine zote zilizopita, hawakuupata huu mwaka wa Kanisa ambao haubadiliki, mara hii ya sita ndio umepatikana.

HITIMISHO
Kwa kuhitimisha, majira inayozinduliwa: Kisleu ni 1; Thebeti ni 2; Shebati ni 3; Adari ni 4; Abibu ni 5; Zivu ni 6; Siwani ni 7; Tamuzi ni 8; Abu ni 9; Eluli ni 10; Ethanimu ni 11; na Buli ni 12. Mpangilio huu ni kutokana na Mkombozi Halisi kuja Sayuni Mwezi Kisleu kwa Mujibu wa Isaya 59:20.Kama nilivyotangulia kufafanua, Tofauti ya majira iliyopatikana Mwaka 2012 na mwaka 2018 ni kwamba wakati wa 2012 ilirejea Abibu mpaka Adari kama tunavyosoma katika Esta 3:7(kama Musa alivyokuwa amepewa kwa mujibu wa Kutoka 23:15).

Lakini wakati wa 2018 mkombozi alikuja mwezi Kisleu ambao kwa Musa ilikuwa ni Mwezi wa tisa. Kwa Mkombozi Halisi, Mwezi huo wa Kisleu ukawa wa kwanza; maana kwa mujibu wa Kutoka 12:1-2, mwezi ambao Mkombozi amewakomboa ndiyo unakuwa mwezi wa kwanza kwenu. Wote tuelewe kuwa hata wakati wa Musa, Abibu haikuwa mwezi wa kwanza kwao, ila ni kwa kuwa Mkombozi kipindi kile aliwatoa utumwani Misri mwezi huo wa Abibu, ndio ikaamriwa Abibu uwe mwezi wa Kwanza kwao.
author

Author Name

Author Description!

Get Free Email Updates to your Inbox!

Post a Comment

www.CodeNirvana.in

Magazeti Ya Leo

Copyright © Magazeti ya Leo, Habari Leo Tanzania, Mwananchi, Michuzi, mwanaspoti, nipashe, Udaku | Designed By Code Nirvana