Featured

    Featured Posts

AG DK. FELESHI AWATAKA MAWAKILI WA SERIKALI VIJANA KWENDA NA WAKATI

Na Mwandishi Maalum, Dodoma
3/28/2022

Kasi ya mabadiliko ya  kiuchumi, kijamii na kisiasa  inayoikabili Tanzania na Dunia kwa ujumla inawataka Mawakili wa Serikali na hususani walio vijana, kuwa tayari kwa kujiendeleza, kujijengea uwezo na umahili katika maeneo mbalimbali ili kukabiliana na kasi hiyo.

Hayo yameelezwa leo Jumatatu, Machi 28, 2022 na Mwanasheria Mkuu wa Serikali Jaji Dk. Eliezer  Feleshi  alipokutana na kufanya mazungumzo na Mawakili wa Serikali Vijana takribani 27 kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Ofisi ya Taifa ya Mashtaka Kanda ya Dodoma.

AG Dk. Feleshi amewaambia Mawakili hao wa Serikali kwamba, ni kwa kujiendeleza na kujiongezea maarifa ndipo watakapoweza kuishauri vyema na kwa weledi Serikali na kuedesha mashauri na mashtaka kwa  ubora  na viwango vya hali ya juu kama Mawakili wa Serikali.

“Kwa muda mrefu nimekuwa nikitamani sana kukutana nanyi Mawakili wa Serikali Vijana, na leo imewezekana.  Na kubwa ambalo nimependa  tubadilishane mawazo ni   hili  la kujengeana uwezo na maarifa katika sehemu zetu za kazi ili kupitia maarifa hayo muweze  kutekeleza majukumu yenu  na katika viwango vinavyokubalika” akasema AG Feleshi.

Amebainisha kwamba  yeye binafsi  ni muumini mzuri sana  wa dhana ya   kujiendeleza na kujiengea maarifa na umahili mahali pa kazi.  

“Nimelisimamia hili katika maeneo mbalimbali niliyofanya kazi baada ya kuona changamoto mbalimbali  katika utekelezaji wa majukumu nikiwa Mwendesha Mashtaka wa Serikali  na pia nikiwa Jaji kiongozi kwa sababu, niliona haja na umuhimu  wa suala hilo na nimeona  matokeo  chanya ya dhana hiyo”. akasema AG Dk. Feleshi

Katika mazungumzo hayo na ambayo  yamefanyika katika ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu  Mtumba, Dodoma,  AG Dk. Feleshi amesema uwezeshwaji wa Mawakili wa Serikali  waliopo katika Ofisi ya  Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Mataifa ya Mashtaka kunaweza kufanyika kwa kuweka utaratibu mzuri wa Mawakili Waandamizi wenye uzoefu na waliobobea kuwafundisha  na kuwaelekeza Mawakili wa Serikali vijana ili nao waweze kuboresha utendaji wao  wa kazi.

“Tutambue wazi kwamba, dunia inabadilika kwa kasi sana,  nasi lazima tuenende na kasi hiyo, nitawapa  mfano mdogo, vita vinayoendelea hivi sasa kati  ya Urusi na Ukraini italeta changamoto  nyingi na kubwa, mnasoma huko Ulaya wanavyojadiliana  kuangalia  namna na hatua za kukabiliana  na changamoto zitakazotokana na vita hiyo zikiwamo za masuala ya gesi na mafuta.  Kwa hiyo tunaweza kujikuta  tunapokea wawekezaji wengi katika maeneo hayo je  kama  mawakili wa Serikali  tunajipangaje” akaeleza AG Dk. Feleshi.

Akawataka  Mawakili  hao wa Serikali kutambua kwamba leo wao ni vijana lakini kesho watakuwa viongozi  na huwezi kuwa kiongozi pasipo kuwa na  nia, hamu, utashi na uthubutu wa kujiendeleza na kujijengea  maarifa. Nyinyi mmesoma katika mazingira mazuri na bora kuliko sisi wa huko zamani,  rai yangu kwenu zitumieni  fursa hizi vizuri”.

Amebainisha  kuwa  ni lazima na muhimu  kwa wakili wa serikali kuwa na  ujuzi na maarifa mtambuka na kuweza kutekeleza majukumu mbalimbali kwa wakati mmoja.

“Usiridhike kwamba wewe ni  mwendesha mashtaka basi ukaishia hapo, au wewe ni Muandishi wa Sheria ukaridhika hivyo au wewe ni Mpekuzi wa Mikataba ukaridhika na hali hiyo. Kama  ni mwendesha mashtaka basi uwena uelewa pia wa kuedesha kesi za madai,  ujue pia kuandika sheria,  ujue pia kupekua mikataba, na hivyo hivyo kwa  muandishi wa sheria,  ama mpekuzi wa mikataba, uwe tayari kufanya kazi sehemu au katika taasisi  yoyote”, akasema AG Dk. Feleshi.

Akitilia mkazo  juu ya  umuhimu wa Mawakili wa Serikali kujiendelea  na kujengea uwezao na umahili sehemu za kazi, Mwanasheria Mkuu Dk. Feleshi alisema hatamuelewa wakili yeyote wa serikali wakiwemo viongozi watakaofanyia mzaha  jambo hilo na kwamba watakuwa kama wahujumu  wa maendeleo yao binafsi ya na Taifa.

Vile vile amewahimiza  Mawakili wote wa Serikali, kujiamini,  kujithamini na kujipambanua kwa sababu nafasi yao kama Mawakili wa Serikali ni kubwa na ya heshima sana.

Kwa upande wao  Mawakili hao wa serikali pamoja na kumshukuru Mwanasheria Mkuu huyo kwa kukutana  nao na kubadilishana nao mawazo wameahidi kuzingatia ushauri wake na pia wameomba kuandaliwa utaratibu wa namna ya kubadilishana uzoefu ikimo namna ya kwenda mahakamani kuendesha.

“Mhe. Tunakushuru kwa kukutana nasi,  tutayazingatia haya na tunaomba  utaratibu uaandaliwe ili tuweze kubadilishana uzoefu na kujifunza na  pia kwenda mahakamani”. Akasema  Dk. Dalfina Ndumbalo Wakili wa Serikali kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Mwanasheria Mkuu wa Serikali Jaji Dk. Eliezer Feleshi  akiwa katika picha ya kumbukumbu na  Mawakili wa Serikali Vijana kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Ofisi ya Taifa ya Mashtaka Kanda ya Dodoma, baada ya kukutana nao na kubadilishana mawazo, Ofisini kwakei, jijini Dodoma, leo. Mwenye suti ya bluu kulia kwa AG ni Seth Henry Mkemwa Wakili wa Serikali Mkuu na Kaimu  Mkurugenzi Sehemu ya  Makosa ya Udanganyifu na utakatishaji Fedha.
Mawakili wa Serikali  kutoka Ofisi ya  Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Ofisi ya Taifa ya Mashtaka Kanda ya Dodoma, wakimkiliza Mwanasheria Mkuu wa Serikali Jaji  Dk. Eliezer  Feleshi (Hayupo Pichani), alipokutana nao kwa ajili ya kubadilishana mawazo, leo  Jijini Dodoma. (Picha zote na Ofisi ya AG).
author

Author Name

Author Description!

Get Free Email Updates to your Inbox!

Post a Comment

www.CodeNirvana.in

Magazeti Ya Leo

Copyright © Magazeti ya Leo, Habari Leo Tanzania, Mwananchi, Michuzi, mwanaspoti, nipashe, Udaku | Designed By Code Nirvana