Na Bashir Nkoromo, CCM Blog
Chuo Kikuu cha Mzumbe kimesema Kaimu Mkuu wa Chuo hicho Ndaki ya Dar es Salaam Prof. Prosper Ngowi ambaye amefariki dunia pamoja na dereva Innocent Mringo, kwa ajali ya gari alikuwa mhimili muhimu katika Menejimenti ya Chuo hicho.
Taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Chuo Kikuu Mzumbe Rose Joseph, imemkariri Makamu Mkuu wa Chuo hicho Prof. Lughano Kusiluka akisema Prof. Ngowi alikuwa muhimili wa Chuo hicho hususani katika usimamizi wa shughuli za kitaaluma Ndaki ya Dar es Salaam, mbunifu, na msimamizi mahiri wa miradi ya maendeleo, utafiti, machapisho na elimu kwa Umma.
"Baraza, Menejimenti, Wafanyakazi na Jumuiya nzima ya Chuo Kikuu Mzumbe, tunatoa pole kwa Familia ya Marehemu Prof. Prosper Honest Ngowi, na Innocent Gerson Mringi, Ndugu, Jamaa na Marafiki wote waliogushwa na msiba huu mzito, Daima tutawakumbuka na kuuenzi mchango wao mkubwa kwa kipindi chote cha utumishi wao katika kuendeleza Chuo Kikuu Mzumbe", imesema taarifa hiyo.
Taaarifa imethibitisha kuwa Profesa Ngowi na Dereva Mringo wamepatwa na ajali hiyo katika eneo la Mlandizi katika mkoa wa Pwani, wakiwa njiani wakitokea dar es Salaam, kwenda Kampasi Kuu ya Chuo hicho, Morogoro kwa ajili ya shughuli za kikazi.
"Mipango ya mazishi inaendelea kwa kushirikiana na familia za marehemu, na mara taratibu zitakapokamilika, Umma utajulishwa", imesema taarifa hiyo.
Taarifa hiyo imesema, Prof. Ngowi aliajiriwa na Chuo Kikuu Mzumbe mwaka 1994 kuwa Mkufunzi Msaidizi, baada ya kuhitimu Stashahada ya Juu ya Mipango ya
Uchumi.
Baadae alijiendeleza na kupata Shahada ya Kwanza, Shahada ya Umahiri katika Biashara na Uchumi, na baadae mwaka 2014 alihitimu Shahada ya Uzamivu (PhD) katika Uchumi.
Mwaka 2015 alipandishwa cheo na kuwa Profesa Mshiriki, na kuongoza Idara mbalimbali za Chuo Kikuu Mzumbe kabla ya kuteuliwa kuwa Mkuu wa Ndaki ya Dar es Salaam hadi umauti ulipomkuta, leo.
Mbali na kushika nafasi za uongozi Prof. Ngowi amekuwa Mjumbe wa Bodi mbalimbali za Taasisi za Umma na Binafsi, Bodi za Kitaaluma, Mshauri na mchambuzi wa masuala ya kiuchumi na biashara, Mtafiti, Mshauri na Mwandishi wa Makala mbalimbali za uchumi, na mtoa mada katika makongamano ya kitaifa
na kimataifa.
Kwa upande wa Dereva Innocent Gerson Mringo, taarifa imesema, aliajiriwa na Chuo Kikuu Mzumbe kuwa Dereva Daraja la Pili mwaka 2017 hadi umauti ulipomkuta leo.
Alipata mafunzo yake ya udereva na kuhitimu Chuo cha Taifa cha Usaririshaji mwaka 2016, na VETA
mwaka 2017.
|
Prof. Prosper Ngowi, enzi za uhai wake. |
|
Innocent Gerson Mringo |
Author Name
Author Description!
Get Free Email Updates to your Inbox!
Post a Comment