Na Bashir Nkoromo, CCM Blog
Zikiwa zimesalia siku chache Mkutano Mkuu wa Taifa wa Chama cha Mapinduzi (CCM) ufanyike wiki hii, siku ya Ijumaa, Machi Mosi, 2022, yapo mambo kadhaa yanasubiriwa kwa hamu na Wanachama wa CCM na Watanzania wote kwa jumla.
Watanzania wanayasubiri mambo hayo kwa hamu kwa kuwa mustakabali wa maisha yao kuwa ya Ustawi na maendeleo ya Taifa katika nyanja zote hasa za Kiuchumi, Usalama na Amani ni lazima yatokane na uongozi chanya wa CCM kwa kuwa ndicho chama tawala.
Akizungumza ofisini kwake jijini Dodoma hivi karibuni Katibu Mkuu wa CCM Daniel Chongolo alisema maandalizi ya awali ya Mkutano huo utakaofanyika katika Ukumbi wa Kisasa wa Mikutano wa Jakaya Kikwete jijini Dodoma, yamekamilika.
Kwa hakika utakuwa ni mkutano mkubwa kwa kuwa unatarajiwa kuhudhuriwa na viongozi Wakuu Wastaafu wa CCM na Serikali, Wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, Wajumbe mahsusi wa Mkutano huo kutoka nchi nzima wanaokadiriwa kuwa zaidi ya 2000, na bila shaka Vingozi wa Vyama vya Siasa hapa nchini na vyama rafiki duniani watahudhuria.
Mkutano huo ambao utakaokuwa chini ya Mwenyekiti wa CCM Rais Samia Suluhu Hassan kwa mujibu wa Katiba ya CCM, baadhi ya masuala muhimu yatakayojiri ni pamoja na kutumika kuelezea utekelezaji wa Ilani ya CCM kwa kipindi cha miaka mitano, ikiwemo kuonyesha hatua zilizofikiwa katika utendaji wa Serikali.
Mbali na kuangazia yaliyojiri katika utekelezaji wa Ilani ya CCM, bila shaka Mkutano huo Mkuu utajikita katika kuitazama Katiba na Dira ya CCM, katika kuona namna zilivyoweza kuinawirisha CCM katika kipindi cha kufikia Mkutano huo Mkuu na kama kuna haja ya kupunguza, kurekebisha au kuongeza matakwa yaliyomo katika Katiba ya CCM na Dira yake.
Kwa muktadha huo, ni lazima wajumbe wa Mkutano huo Mkuu wajiandae vya kutosha, vichwa viwe vimeshiba hoja chanya, ili wafike na kushiriki Mkutano huo kila mmoja akiwa anao uwezo mkubwa wa kuchangia kwa hekima na busara mijadala mbalimbali hasa kuhusiana na Katiba ya CCM na Dira yake.
Hilo ni jambo la lazima sana kwa wajumbe kwa kuwa michango yao thabiti na chanya iliyojaa uzalendo ndiyo itaifanya CCM kuendelea kuaminiwa na Watanzania na kuwa imara zaidi katika kusikiliza shida za watu na kuzitatua.
Sasa kutokana na Umihumu wa Mkutano huo Mkuu Maalum, tunadhani ni muhimu kueleza mambo kadhaa japo kwa uchache ili kujenga uelewa kuwa Mkutano Mkuu Maalum siyo jambo dogo, bali ni jambo kubwa kwa kuwa mkutano huo Mkuu ndicho Kikao Kikubwa chenya mamlaka yoote kuhusu sura na mwelekeo wa CCM.
Katiba ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya Mwaka 1977, Toleo la Mwaka hu, Fungu la 7, Ibara ya 99 (2) imeeleza wazi kwamba Mkutano Mkuu wa Taifa wa CCM utakuwa ndio Kikao Kikuu cha CCM kupita vyote na ndicho kitakachokuwa na madaraka na maamuzi ya mwisho.
Kwa maana hiyo, Mkutano Mkuu wa CCM ndicho chombo kikuu cha maamuzi yoyote makubwa yanayoathiri Chama kizima kimuundo na Ibara ya 100 kuanzia sura ndogo (1) hadi (7) imeeleza vyema kazi za Mkutano Mkuu wa CCM kuwa ni pamoja na kusimamia siasa nzima ya CCM na kupanga na kusimamia Utekelezaji wa shughuli zote za CCM.
Kwa mujibu wa Ibara hiyo piaMkutano huo Mkuu ndiyo wenye mamlaka ya mwisho kubadili sehemu yoyote ya Katiba yake ya Chama ili kujiimarisha, kuchagua na kuthibitisha Jina la Mwanachama mmoja wa kugombea Urais wa Tanzania na Zanzibar pamoja na shughuli zingine nyingi za kuongeza ufanisi wa Chama chote.
Ibara ya 99 (7) ya Katiba ya CCM ya Mwaka 1977 inaeleza pia kwamba Mkutano huo Mkuu ndiyo kikao cha juu kabisa ndani ya CCM na chenye nguvu kubwa kuliko Kikao chochote kile na kitaongozwa na Mwenyekiti wa CCM Taifa.
Pia Ibara hiyo ya 99 (7) ya Katiba ya CCM ya Mwaka 1977 inaelekeza kwamba Mwenyekiti wa Mkutano Mkuu atakiwa Mwenyekiti wa CCM Taifa, na asipohudhuria kwa sababu yoyote, basi mmoja wa Makamu Mwenyekiti wa CCM Taifa wa Bara au Zanzibar atachukua hatamu ya kuongoza Kikao hicho.
Lakini pia Ibara hiyo imeeleza zaidi kwamba ikitokea wote watatu hawapo ama hawawezi kuhudhuria kwa sababu yoyote basi Halmashauri Kuu ya CCM Taifa itamchagua Mjumbe yeyote miongoni mwa wajumbe wa Mkutano huo kuwa Mwenyekiti wa muda wa kuongoza.
Post a Comment