CCM Blog, Mara
Kampuni ya Uchimbaji Madini ya Dhahabu ya Barrick kupitia mgodi wake wa Barrick North Mara imepigwa faini ya Sh. Bilioni moja, kwa hatia ya kusababisha uchafuzi wa mazingira, Mkoani Mara.
Barrick imepigwa faini hiyo baada ya kubainika kufanya uzembe uliosababisha bomba la maji taka kupasuka na kutiririsha majitaka hayo kwenye vyanzo vya maji na makazi ya watu.
Akizungumza katika tukio hilo, Waziri wa Madini Dk. Doto Biteko, amesema Mgodi wa North Mara ambao unaomilikiwa na Kampuni ya Barrick kwa asilimia 84 na Serikali kwa asilimia 16 unapaswa kuwa mfano bora kwa kufuata na kusimamia Sheria, Taratibu na Kanuni zilizowekwa na Serikali.
"Haiwezekani bomba la maji taka lipasuke saa tatu asubuhi halafu uongozi upate taarifa saa sita mchana na isitoshe kuna walinzi wanaozunguka maeneo hayo, huu ni uzembe wa hali ya juu, sisi tunataka usalama wa watu wetu," amesema Dk. Biteko.
Kufuatia kadhia hiyo, Dk. Biteko amembadilishia majukumu Afisa Migodi Mkazi wa Mgodi wa North Mara, kwa kushindwa kusimamia majukumu yake ipasavyo katika eneo alilopangiwa.
"Kutokana na uzembe huu uliofanyika hapa mgodini naanza na Afisa wangu namuondoa hapa ataenda kupewa majukumu mengine, siwezi kukubali uzembe huu uendelee," akasema Dk. Biteko.
Sanjari na hilo, Waziri Biteko ameitaka Kampuni ya Barrick kuhakikisha inachangia katika kuleta maendeleo kwa jamii (CSR) ili wananchi wanaoishi katika maeneo yanayozunguka Migodi yaweze kunufaika na uwepo wa mgodi huo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Taifa la Uhifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), Dk. Samuel Gwamaka amesema, Kifungu cha 187 cha Sheria ya Mazingira kinampa mamlaka ya kuipiga faini Taasisi au Kampuni yenye makosa ya kuvujisha maji taka, kuanzia Sh. milioni 50 hadi Sh. Bilioni 10.
"Kampuni hii ya Barrick tumeipiga faini ya Sh. Bilioni moja ili iwe mfano kwa wengine, hivyo itambuliwe hilo ni kosa na sisi kama NEMC tutaendelea kufanya ukaguzi wa mara kwa mara ili kuhakikisha makosa kama haya hayajitokezi," akasema Dk. Gwamaka.
Naye, Mkuu wa Mkoa wa Mara Ally Happy amesema, Rais Samia Suluhu Hassan anataka kuona fedha zinazotolewa kwa ajili ya miradi zinawanufaisha wananchi ambapo ameitaka kampuni ya Barrick kutoa michango yake kwa jamii (CSR) ili kusogeza maendeleo kwa jamii.
Naye Mbunge wa Jimbo la Musoma Vijijini Mwita Waitara, amempongeza Dk. Biteko na kusema tatizo la kupasuka kwa bomba la maji taka limetokea jana lakini leo Waziri mwenye dhamana amefika eneo la tukio, hiyo inaonyesha ni kiasi gani anajali na anathamini utu wa watu.
Post a Comment