Featured

    Featured Posts

KIONGOZI WA MBIO ZA MWENGE AIPONGEZA RUWASA KUTEKELEZA MRADI WA MAJI NANGOMBA KWA WELEDI

 




************************

Na Muhidin Amri
Nanyumbu

KIONGOZI wa mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2022 Sahil Geraruma,ametembelea mradi wa maji safi na salama katika kijiji cha Nangomba uliojengwa na wakala wa usambazaji maji safi na usafi wa mazingira vijiji(Ruwasa)wilaya ya Nanyumbu.

Geraruma,amewapongeza Wahandisi  na watendaji mbalimbali wa Ruwasa wilayani humo, kwa kutekeleza vyema ujenzi wa mradi huo wa maji ambao umetimiza lengo la Serikali la kumtua mama ndoo kichwani.

Geraruma ametoa pongezi hizo jana,mara baada ya kutembelea mradi huo umetekelezwa kwa lengo la kumaliza changamoto ya huduma ya  maji safi na salama kwa wananchi wa vijiji viwili vya Nangomba na Mjimwema.

“Wahandisi wa Ruwasa nawapongeza sana kwa kuendelea kujenga na kusimamia mradi huu,mmefanya kazi nzuri sana,Serikali kupitia mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2022 inawapongeza”alisema.

Alisema, wataalam hao wameonyesa namna watendaji wa taasisi za umma wanavyotakiwa kutimiza wajibu wao  katika kujenga na kusimamia miradi muhimu ya maendeleo katika jamii.

Amewataka kuendelea kuchapa kazi,kutanguliza uzalendo,kuwa makini na kuhakikisha miradi yote inayojengwa ina kuwa na ubora na viwango vinavyotakiwa.

Amewataka wataalam wa taasisi nyingine za umma katika mkoa wa Mtwara,kujifunza  kwa Ruwasa  namna miradi inavyojengwa pindi wanapopewa dhamana ya kutekeleza miradi  ya maendeleo  yenye lengo la kuwaondolea wananchi kero na kuharakisha  maendeleo ya nchi.

Aidha,ameishukuru familia ya mkazi wa kijiji cha Nangomba Said Abdul kwa uzalendo wake kufuatia kutoa eneo lililojengwa mradi huo bure, na kumuagiza meneja wa Ruwasa wilaya ya Nanyumbu Mhandisi Simon Mchucha kupeleka  huduma ya maji kwa familia hiyo bila gharama yoyote.

Kwa upande wake Meneja wa Ruwasa wilayani Nanyumbu Simon Mchucha alisema,mradi huo umetekelezwa katika vijiji vya Nangomba na Mjimwema kata ya Nangomba kupitia program ya malipo kwa matokeo(PforR) kwa gharama ya Sh.196,430,118.06.

Alisema, chanzo cha mradi  ni kisima kirefu chenye uwezo wa kuzalisha lita 6,000 kwa saa  na unahudumia  zaidi ya wananchi 5,151 katika vijiji vya Nagomba na Mjimwema.

Mchucha alieleza kuwa,ujenzi wa mradi huo umehusisha vituo 11 vya kuchotea maji,ukarabati wa tenki la lita 50,000 nyumba ya mitambo, nyumba ya mlinzi,ununuzi wa pampu na Jenereta na kaya 23 zimeunganishiwa huduma ya maji.

Alitaja mafanikio  mengine ni ukusanyaji mapato yanayotokana na mauzo ya maji ambapo wastani kwa mwezi ni Sh.1,270,530 ambapo  fedha zilizokusanywa tangu mradi ulipoanza kutoa huduma Mwezi Oktoba 2021 hadi Machi 2022 kufikia Sh.8,892,285.

Mhandisi Mchucha alisema,mradi  huo unaendeshwa na wananchi kupitia Jumuiya ya watumia maji(NAMJI)ambapo chombo cha watoa huduma za maji ngazi ya jamii kimefanikiwa  kutoa ajira kwa watu 15 kati yao wanaume 2 na wawanawake 13.

Kwa mujibu wake,Ruwasa kupitia vikao na mikutano yam aji inayofanyika sehemu mbalimbali inawahamasidha wananchi kujitokeza kwa wingi kujiandikisha kwenye zoezi  maalum la sensa ya watu na makazi itakayofanyika Mwezi Agosti Mwaka huu.

Mbunge wa Jimbo la Nanyumbu Yahaya Mhata alisema,huo ni mradi mkubwa kutekelezwa na Ruwasa katika Jimbo la Nanyumbu na ameishukuru Serikali kwa kutoa fedha ambazo zimefanikilisha kujengwa kwa mradi huo.

Amewaasa wanufaika na wananchi kwa jumla,kuhakikisha wanatunza na kulinda miundombinu ya mradi huo ili iweze kudumu kwa muda mrefu kwa faida ya vizazi vya sasa na vinavyokuja.

author

Author Name

Author Description!

Get Free Email Updates to your Inbox!

Post a Comment

www.CodeNirvana.in

Magazeti Ya Leo

Copyright © Magazeti ya Leo, Habari Leo Tanzania, Mwananchi, Michuzi, mwanaspoti, nipashe, Udaku | Designed By Code Nirvana