Featured

    Featured Posts

SERIKALI INATAFUTA NJIA ZA KUPUNGUZA GHARAMA ZA MAISHA KUFUATIA BEI YA MAFUTA KUPANDA

Serikali inatafuta njia zitakazisaidia kupunguza gharama ya maisha kwa Watanzania kutokana na kupanda kwa bei ya mafuta katika soko la dunia, ambapo kwa hapa nchini viwango vipya vya bei ya mafuta vilianza kutumika jana, baada ya kutangazwa juzi na EWURA.
 
 
Hayo yamesemwa na Waziri Mkuu Majaliwa Kassim Majaliwa  katika kikao kilichofanyika usiku wa kuamkia leo Alhamisi, Mei 5, 2022, katika  Ofisi Ndogo ya Waziri Mkuu iliyoko Oysterbay, jijini Dar es Salaam, kutathmini kupanda kwa bei ya mafuta na kuangalia namna gani Serikali inaweza kufanya ili kupunguza athari na kuleta unafuu wa gharama za maisha kwa Watanzania.
         
Waziri Mkuu amesema kikao hicho kimefanyika ikiwa ni utekelezaji wa maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan, Rais ambaye ameagiza viongozi wa sekta husika wahakikishe wanatafuta suluhisho la kupanda kwa bei ya mafuta hata kama bei hiyo inaendelea kupanda duniani.
 
"Mheshimiwa Rais ameona changamoto wanayopitia Watanzania kutokana na kupanda kwa bei ya mafuta katika soko la dunia, hivyo kikao hiki ni matokeo ya maagizo yake ya kuhakikisha sisi kama viongozi tunatafuta suluhisho la muda mfupi na la muda mrefu ili kukabiliana na changamoto hii," amesisitiza.
 
Waziri Mkuu amesema kuwa tayari Wizara ya Nishati imeanza kutafuta njia mbadala za uagizaji wa mafuta pamoja na kupunguza makato mengineyo ili kupunguza bei ya mafuta.
 
"Serikali inaangalia njia mbadala za uagizaji wa mafuta, kupitia kwa wazabuni wengine kama ambavyo imeshauriwa na wabunge na tayari mchakato huo umeanza, kwa kutathmini maombi 24 ambayo yaliwasilishwa kwa Wizara na sasa wamebaki wazabuni sita ambao wameingia hatua inayofuata. Inachokifanya Serikali hivi sasa ni kujiridhisha na uwezo wao wa kusambaza mafuta kulingana na mahitaji na taratibu zilizowekwa na Serikali,” amesema.
 
Kikao hicho kimehudhuriwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Bw. George Simbachawene, Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Mwigulu Nchemba, Waziri wa Nishati, Bw. January Makamba, Makatibu Wakuu, pamoja na watendaji wakuu wa taasisi za EWURA, TPDC na Wakala wa Uagizaji wa Mafuta kwa Pamoja (PBPA).



author

Author Name

Author Description!

Get Free Email Updates to your Inbox!

Post a Comment

www.CodeNirvana.in

Magazeti Ya Leo

Copyright © Magazeti ya Leo, Habari Leo Tanzania, Mwananchi, Michuzi, mwanaspoti, nipashe, Udaku | Designed By Code Nirvana