Featured

    Featured Posts

WANAKIJIJI CHA KILANGALA MKOANI LINDI WAMSHUKURU RAIS SAMIA MBELE YA SHAKA KWA KUZIKOMBOA KIUCHUMI KAYA MASIKINI KUPITIA TASAF

Mchinga, Lindi
Wananchi wa kijiji cha Kilangala katika Jimbo la Mchinga mkoani Lindi wameishukuru Serikali ya Awamu ya sita inayongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan, kwa kuonesha kwa vitendo dhamira yake kwa vitendo katika kuzikomboa Kaya masikini kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF).

Shukurani hizo wamezitoa wakati wakizungumza mbele ya Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, Itikadi na Uenezi, Shaka Hamdu Shaka alipokuwa katika Kijiji hicho cha Kilangala akiwa katika ziara ya kikazi mkoani Lindi, jana.

Wananchi hao wamesema kupitia fedha hizo za TASAF wamenufaika kwa kuinuka kiuchumi kwa kubuni miradi mbalimbali ikiwemo kilimo cha minazi ambapo wana ekari 15 za mashamba ya zao hilo.

 Akizungumza kwa niaba ya wanufaika wenzake Mwanakijiji hicho Dalini Makwaya alisema yeye na wenzake wanaojishughulisha na mradi wa Kilimo cha mazao mbalimbali ya biashara ikiwemo minazi, wanatoa shukrani kwa Rais Samia kwa uamuzi wake wa kutoa fedha kupitia TASAF na kuwafikia moja kwa moja na hivyo kubadilisha maisha yao.

"Tunaishukuru Serikali inayoongozwa na Rais Samia kwa mpango huu wa TASAF kwa kuwa umetusaidia sisi kaya masikini, kupitia fedha hizo tumekata bima za afya, tunanunua sare za wanafunzi wetu na kubwa zaidi tunanunua chakula. Kwa hili tunasema asante sana Rais wetu," amesema Makwaya.

Kwa upande wake Afisa wa TASAF katika Halmashauri ya Manispaa ya Lindi Dativa Kisima alimueleza  Shaka kuwa pamoja na kuwawezesha wananchi kujipatia kipato kwa muda mrefu bado wamewapa ajira za muda kwa kuwalipa Sh. 3000 kila mmoja kila siku.

Akizungumza na wananchi hao, Shaka amesema kwa ushuhuda huo kuna kila sababu ya kuendelea kumshukuru Rais Samia ambaye amedhamiria kwa vitendo kuondoa umasikini kwa Watanzania kupitia TASAF kwa kushirikiana na wabia wa maendeleo huku akionesha matumaini makubwa kwa Mkoa wa Lindi akisema zinakwenda kuuinua zaidi kiuchumi.

"Rais Samia anayo dhamira ya dhati kabisa kuhakikisha kwamba anatumia kila fursa anayoipata pamoja na kushirikiana na wabia wa maendeleo anawatoa Watanzania katika dimbwi hili la umasikini.

Mkuu wa Mkoa wa Lindi kupitia maelezo yake amesema kwamba Rais Samia Suluhu Hassan ameamua kwa makusudi kuwekeza nguvu katika Mkoa huu wa Lindi ili kuleta mabadiliko, kwanza ya huduma za kijamii, lakini pili kuleta mabadiliko katika huduma hizi za kiuchumi na hilo linaonekana kwa macho kupitia miradi ya maendeleo tuliyoikagua leo," akasema Shaka.

Kwa upande wake mkuu wa Mkoa wa Lindi, Zainab Tarek, amesema Mkoa huo ni wa kimkakati ambapo mazao yanayolimwa ni ya kibiashara akitolea mfano zao la minazi na korosho.

"Mwananchi akiwa na minazi anauhakika wa kila baada ya miezi mitatu kupata fedha. Lakini pia tuna zao la korosho ambalo ni zao linauzwa kibiashara duniani na ushahidi ukifika msimu wafanyabiashara kote duniani wanakuja mkoani Lindi kwa ajili ya kupata korosho namba moja inayopatikana mikoa ya Kusini.

Kwa hiyo tulichokifanya tunaendelea kuwahamasisha wananchi wetu hawa wanaopata fedha za TASAF waingie kwenye kilimo hiki kwa sababu ukishaotesha minazi na ikaota vizuri unauhakika kabisa kwamba miaka yako yote ya maisha unauhakika wa kuvuna nazi au madafu na ukajipatia fedha," akasema Tarek.

Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, Itikadi na Uenezi Shaka Hamdu Shaka, akipata maelezo kutoka kwa Mwanakijiji Dalini Makwaya kuhusu mche wa mnazi uliomo kwenye mradi wa Kilimo cha minazi uliowezeshwa na fedha za mradi wa Kunusuru Maya Masikini unaotekelezwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii ( TASAF) katika Kijiji Cha Kilangala, Manipaa ya Lindi mkoani Lindi. (Picha na fahadi Siraji).
author

Author Name

Author Description!

Get Free Email Updates to your Inbox!

Post a Comment

www.CodeNirvana.in

Magazeti Ya Leo

Copyright © Magazeti ya Leo, Habari Leo Tanzania, Mwananchi, Michuzi, mwanaspoti, nipashe, Udaku | Designed By Code Nirvana