Bukoba, Kagera
Rais Samia Suluhu Hassan Alhamisi wiki hii, anatarajia kuzindua Mradi wa Maji Kyaka-Bunazi wenye thamani ya Sh. Bilioni 15.7 na kukagua Miradi ya Kiwanda cha Kagera Sugar mkoani Kagera, kuhamasisha zaidi uwekezaji katika Mkoa huo.
Akizungumza jana mjini Bukoba, Mkuu wa Mkoa wa Kagera Meja Jenerali Charles Mbuge amesema Rais anatarajia kuwasili mkoani humo keshokutwa, Jumatano Juni 8, 2022, kuanza ziara ya kikazi, na atapita Wilaya za Biharamulo, Muleba na Bukoba kwa Barabara akisalimia wananchi katika Wilaya hizo.
" Juni 9, 2022, Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan, akiwa mkoani kwetu hapa Kagera, atafika katika Wilaya ya Missenyi ambako atazindua Mradi wa Maji Kyaka-Bunazi wenye thamani ya Sh. Bilioni 15.7 na kukagua Miradi ya Kiwanda cha Kagera Sugar ili kuhamasisha zaidi uwekezaji katika Mkoa wa Kagera.
Kesho yake, Juni 10, 2022, Rais Samia anazindua Msikiti wa Jumi' Ul Istiqaama Bukoba, uliopo Mtaa wa Tupendane Manispaa ya Bukoba na kisha atazungumza na wananchi wa Mkoa wa Kagera na Taifa kwa ujumla kupitia mkutano wa hadhara utakaofanyika katika Uwanja wa michezo wa Kaitaba Manispaa hiyo", akasema Meja Jenerali Mbuge kuwaambia Waandishi wa Habari na kuongeza;
"Nawaomba Wananchi wote mjitokeze kwa wingi katika maeneo yote atakayopita Mheshimies Rais Samia ili kumpokea kwa shangwe, bashasha na nderemo.
Pia nawaomba wananchi wote kutoka maeneo mbalimbali ya Mkoa huu, mjitokeze kwa wingi sana kuanzia saa 12:00 asubuhi tarehe 10 Juni 2022, kuja kumsikiliza Rais Samia katika mkutano huu wa hadhara utakaofanyika katika uwanja wa Kaitaba Manispaa ya Bukoba".
Rais Samia Suluhu Hassan |
Post a Comment