Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Dkt Pindi Chana akisoma makadirio ya Bajeti ya wizara hiyo.
Wizara ya Maliasili na Utalii kupitia Bajeti yake ya mwaka 2022/2023 inatarajia kujenga barabara mpya zenye urefu wa kilomita 2,500 katika hifadhi za Taifa za Arusha, Burigi - Chato, Gombe, Katavi, Kilimanjaro, Kitulo, Mahale, Udzungwa, Manyara, Rubondo, Rumanyika - Karagwe, Ruaha, Mikumi, Nyerere na Serengeti.
Aidha, Wizara itajenga njia za utalii zenye urefu wa kilomita 251 na barabara za kutembea kwa miguu zenye urefu wa kilomita 342.5.
Hayo yamesemwa Jijini Dodoma na Waziri wa Maliasili na Utalii Balozi Dkt. Pindi Chana wakati akisoma Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara hiyo Bungeni jijini Dodoma leo na kuongeza kuwa itakarabati barabara zenye urefu wa kilomita 6,500 na viwanja vya ndege 17 katika hifadhi za Taifa Ruaha, Mikumi, Nyerere, Saadani, Tarangire, Mkomazi na Serengeti.
Waziri Chana ameongeza kuwa Wizara hiyo itawezesha uandaaji wa Mipango ya Matumizi Bora ya Ardhi katika vijiji 30 vinavyozunguka Hifadhi ya Taifa Nyerere na vijiji 18 vinavyozunguka Hifadhi ya Taifa Serengeti; kuchimba mabwawa mapya nane (8); na kukarabati mabwawa matano (5) kwa matumizi ya wanyamapori katika hifadhi za Taifa za Mkomazi, Tarangire, Mikumi, Katavi, Ruaha, Saadani, na Serengeti.
“Wizara itaboresha maeneo ya malisho ya wanyamapori kwa kudhibiti mimea vamizi katika eneo lenye ukubwa wa hekta 30,331 katika hifadhi za Taifa Nyerere, Saadani, Serengeti, Arusha, Ibanda-Kyerwa, Mto Ugalla, Mikumi, Mkomazi na Katavi. Vilevile, Wizara itaotesha miti ya asili 100,000 katika Hifadhi ya Taifa Kilimanjaro” alisema Waziri Balozi Dkt Chana
Katika sekta ya Utalii Waziri Balozi Dkt Chana ameeleza kuwa Wizara itakamilisha Mkakati wa Utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Utalii ya Mwaka 1999; na kuandaa Programu ya Maendeleo ya Utalii nchini. Aidha, itabainisha maeneo ya fukwe katika maziwa makuu ya Viktoria, Tanganyika na Nyasa kwa ajili ya uwekezaji na uendelezaji wa shughuli za utalii.
“Katika mwaka wa fedha 2022/2023, Wizara itatekeleza miradi ya maendeleo ambayo ni: Mradi wa Usimamizi wa Maliasili na Kuendeleza Utalii Kanda ya Kusini; Mradi wa Maboresho ya Usimamizi wa Fedha za Umma; Mradi wa Kukabiliana na Ujangili na Biashara Haramu ya Wanyamapori” Aliongeza Waziri Balozi Dkt Chana
Waziri Balozi Dkt Chana aliliomba Bunge liidhinishe jumla ya Shilingi 624,142,732,000 (Bilioni mia sita ishirini na nne, milioni mia moja arobaini na mbili, mia saba thelathini na mbili elfu) kwa ajili ya utekelezaji wa majukumu mbalimbali ya Sekta ya Maliasili na Utalii kwa mwaka ujao wa fedha.
Post a Comment