Ikulu, leo
Rais Samia Suluhu Hassan ametuma salamu za rambirambi kwa Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Sophia Mjema kufuatia vifo vya watu 16 vilivyotokana na ajali ya magari na trekta, jana aa 4 usiku, katika Kata ya Mwakata wilaya ya Kahama.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga ACP Leonard Nyandahu jumla ya waliofariki ni wanawake wawili na wanaume 14 huku majeruhi wakiwa ni 11 ambao ni wanawake wanne na wanaume saba ambao wamepelekwa hospitali ya Kahama.
ACP Nyandahu amesema ajali hiyo imehusisha gari ndogo aina ya IST yenye namba ya usajili T 880 DUE iliyokuwa ikielekea Kahama na kuigonga kwa nyuma trekta iliyokuwa imebeba kuni yenye namba ya usajili T 719 AUP.
Watu watatu waliokuwa katika gari hiyo ya IST walifariki dunia papo hapo na dereva wa trekta kukimbia.
Aidha, basi dogo la abiria lenye namba za usajili T 350 DDX lililokuwa likitokea Kahama liligonga kwa mbele gari aina ya Scania yenye namba ya usajili T.658 DUW iliyokuwa imesimama eneo hilo la ajali na abiria 13 kufariki dunia papo hapo.
Ikulu imesema, Rais Samia amevitaka vyombo vyote vinavyosimamia usalama barabarani kuongeza juhudi za kudhibiti ajali.
Rais Samia pia anawapa pole wafiwa wote na anaungana na familia hizo katika kipindi hiki kigumu cha majonzi.
"Mungu azilaze roho za marehemu wote mahali pema peponi. Amina.", imesema taarifa hiyo ya Ikulu ikimkariri Rais Samia.
Rais Samia Suluhu Hassan
Post a Comment