Featured

    Featured Posts

KINANA APOKEA MALALAMIKO YA WAVUVI KATIKA ZIWA VICTORIA IKIWEMO UTITIRI WA KODI

Na Mwandishi Maalum, Mwanza

Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara, Kanali Mstaafu Abdulrahman Kinana amepokea malalamiko ya wavuvi katika Ziwa Victoria mkoani hapa, ikiwemo utitiri wa kodi pamoja na mateso wanayoyapata wavuvi wanapokuwa ziwani ambapo yote hayo ameahidi kuyafikisha katika mamkala husika kwa ufumbuzi.

Aidha amesema Rais Samia Suluhu Hassan amedhamiria kutatua changamoto mbalimbali zikiwemo za kisheria, hivyo changamoto zilizotolewa na wavuvi zitafanyiwa kazi kwa ajili ya kuifanya sekta ya uvuvi kuwa na tija zaidi.

Kinana ameyasema hayo jana jijini Mwanza alipozungumza na wavuvi wa Kanda ya Ziwa Victoria katika ukumbi wa BoT, akiwa katika ziara ya kukagua uhai wa Chama na utekelezaji wa Ialani ya Uchaguzi ya CCM ya 2020-2025.  

“Ndugu zangu nimekuja hapa kuwasikiliza kwa sababu mbili, kwanza Serikali hii ni ya Chama Cha Mapinduzi na pili nimekuja kuwasikiiliza, nimewasikiliza vizuri na kwa umakini, nimesikiliza risala pamoja na wasemaji wengine na yote yaliyozungumzwa na mliyosema tumeandika.

“Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lengo lake kuu ni kuwasaidia Watanzania ili kipato chao kiendelee kuongezeka wanapofanya bisahara. Tunapozungumzia sekta binafsi imara nyingi tunawafikiria wawekezaji wakubwa wa viwanda na wakati mwingine tunawafikiria hata watu kutoka nje pekee.

“Ieleweke ukiifikiria sekta binafsi ni hawa (wajasiriamali wadogo) na ndio wenye viwanda vidogo, wanajituma ili wawe na maisha bora. Serikali haiwezi kumwondolea mtu umasikini wake, lakini inaweza kutengeneza mazingira mazuri, sheria na kanuni nzuri ili iwe rahisi kwa mtu kufanya shughuli zake kwa ufanisi na kwa faida, hiyo ndio kazi ya Serikali,” alisema Kinana.

Aliongeza kuwa, wakati anasikiliza risala ya wavuvi miongoni mwa malalamiko ni uwepo wa kodi 11 ambazo ili uweze kumudu lazima uwe na kipato kikubwa huku akieleza kushangwa na uwepo wa kodi ya maegesho vyombo vya uvuvi.

“Imenifanya nicheke eti kuna kodi ya ‘parking’ yaani kodi zote wamechukua mwisho wa siku wamekuja na parking. Sasa hivi kodi nyingi kidogo, natolea mfano tu., lakini niwaambie nia ya Rais na nimemsikia Rais amezungumza juu ya malengo manne aliyonayo maana la kwanza ni kuleta maridhiano kwa Watanzania, kuleta maboresho ya serikali katika muundo, sheria, sera na kanuni ili maisha ya watu yawe bora zaidi.

“Sasa katika kuboresha mambo risala yenu hii itatizamwa namna gani tunaweza kubadili mambo yao yawe bora zaidi. Risala yenu itatazamwa namna gani tunaweza kubadilisha mambo ambayo yapo kama 14,” alisema.

Aidha, alisema baada ya miaka mingi Rais Samia ametoa fedha za ruzuku kwa ajili ya wakulima, lakini ametoa fedha za ruzuku kwa baadhi ya wavuvi ambapo ametoa fedha kwa ajili ya kutengeneza viamba na kwa mkoa wa Mwanza umepata viamba 42.

“Kwa hiyo Rais ana lengo nzuri , hawezi Rais anaweza kuwa na nia njema , malengo mazuri lakini watanzania lazima tumsaidie ili kazi na malengo yaweze kufikiwa. Risala yenu hii ni moja ya njia ya kumsaidia Rais Samia kuwasaidia Watanzania kuondokana na umasikini vile vile kuwa matajiri kupitia uvuvi,”alisema Kinana.

Hivyo amewaahidi kupitia nafasi aliyonayo vikao alivyonavyo , kwa namna anachohusika na Chama chake na Serikali yake hayo mambo yote waliyoyasema yatashughulikiwa ipasavyo.

“Sina jibu la kutoa hapa na si vizuri nikaanza kuyajibu haya mambo kwasababu mliniita niwasilikize , nimewasiliza mmeniomba na kunitaka kama Chama kinachounda Serikali yake kitafute namna ya kutatua matatizo haya.

“Niwaahidi nitakwenda kuwahakikisha haya masuala yote yaliyotolewa humu ndani yanapata majibu na yanapata ufumbuzi .Yako yanahusu Serikali ya utekelezaji, Wizara , sera, sheria pamoja na kanuni zinazotungwa na Serikali hasa Wizara .Nitatizama namna gani nitasaidia ili na ninyi kwa yale mliyoyasema yaweze kufanikiwa,”alisema Kinana.

Awali akisoma risala ya wavuvi, Katibu wa Kamati ya Ushauri wa Wavuvi Ziwa Victoria Mayalu Kasiri, alielezea changamoto na matatizo yanayosumbua sekta ya uvuvi na kusababisha kudorora.

Ametaja changamoto hizo ni kukithiri kwa uvuvi haramu ambalo limekuwa likiitesa sekta hiyo katika Ziwa Victoria, pili biashara holela ya mabondo ya Sangara ambayo inachangia iwepo wa uvuvi haramu , uvamazi, utekeji na unyang’anyi wa samaki kwa wavuvi ziwani.

Changamoto nyingine ni muundo wa Wizara ya Uvuvi ambapo ameeleza sio mzuri kwa kuwa ina mkurugenzi mmoja ambaye ndiye anayeratibu shughuli zote za Wizara wakati yupo makao makuu ya Wizara.

“Tunaomba Serikali kuweka mfumo rasmi wa wavuvi kwani kumekuwa na matatizo mengi ya wavuvi kuhusu kukosa mitaji na zana bora za uvuvi, hivyo tunaomba Serikali yetu kuweka mfuko maalumu kwa ajili ya wavuvi tu kuliko ilivyo sasa kupitia benki ya kilimo ambayo mvuvi akienda hakopeshiki mpaka alete dhamana ya mali zao kama hati ya nyumba,”amesema.

Ametaja changamoto nyingine tozo ya ushuru wa wavuvi ambazo ziko 11 na ambapo meeleza kwa muda mrefu sasa wamekuwa na utitiri wa tozo na ushuru ambazo hulipwa na wavuvi na kufanya wabebe mzigo mzito na hatimaye washindwe kujikwamua dhidi ya umasikini.

Wakati changamoto nyingine ni ulinzi na usalama wa mali za wavuvi kwani kwa muda mrefu sasa wamekuwa wakipatwa na majanga pindi wawapo katika kazi zaa ziwani.Changamoto nyingine ni mafuta kwa ajili ya wavuvi ambayo alisema wamekuwa wakitumia nishati ya mafuta ya petrol, dizeli na mafuta ya taa ambayo bei yake kwa sasa iko juu.

Kasiri ametaja changamoto nyingine ni sheria za uvuvi na kanuni zake zilizopo sasa ni kandamizi kwa wavuvi kwani hazitoi mwanya wa mvuvi kupata haki zake kama raia wa Tanzania. Wakati nyingine ni bei kubwa ya zana za uvuvi.

Changamoto ya 10 ni mazalia ya samaki katika ziwa victoria kwani sehemu nyingi yanaharibiwa ,changamoto nyingine ni matumizi mabaya ya taa za sola ziwani ambapo kuna baadhi ya wavuvi huzibadilisha na kuzitumbukiza ziwani kuweka taa mbili kwenye Sikimai mojana zaidi ya Wati 10, kutumia betri kubwa ya uwezo wa taa na kutumia ambazo hazijafanyiwa utafiti.

Akiendelea kutaja changamoto hizo alisema iko pia fidia kwa wavuvi walioathiriwa na operesheni sangara mwaka 2018 na changamoto ya mwisho ni kutokuwepo na bodi ya uvivi ambapo wameomba iundwe ili kuratibu masuala ya uvuvi kwa ukaribu zaidi.

Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Kanali Mstaafu Abdulrahman Kinana, akizungumza na wavuvi na wadau wa Uvuvi Kanda ya Ziwa, katika ukumbi wa BoT, jijini Mwanza, akiwa katika ziara ya kukagua uhai wa Chama na utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM 2020-2025. (Picha na Fahad Siraji - CCM).
author

Author Name

Author Description!

Get Free Email Updates to your Inbox!

Post a Comment

www.CodeNirvana.in

Magazeti Ya Leo

Copyright © Magazeti ya Leo, Habari Leo Tanzania, Mwananchi, Michuzi, mwanaspoti, nipashe, Udaku | Designed By Code Nirvana