Nairobi, Kenya
Aliyekuwa Waziri Mkuu wa Kenya Raila Odinga amekubali uamuzi wa Mahakama ya Juu zaidi wa kuidhinisha uchaguzi wa Rais mteule William Ruto, lakini amesema kuwa hakubaliani na uamuzi huo.
Katika taarifa yake leo Jumatatu, Septemba 5, aliwataka wafuasi wake kudumisha utulivu wanapozingatia sheria.
‘Tumezingatia uamuzi wa Mahakama ya Juu kuhusu uchaguzi wa Urais uliofanyika tarehe 9 Agosti 2022. Daima tumesimama kutetea utawala wa sheria na katiba. Katika suala hili, tunaheshimu uamuzi mahakama ingawa hatukubaliani na uamuzi wao
Mawakili wetu walitoa ushahidi usiopingika na ukweli ulikuwa upande wetu, kwa bahati mbaya, majaji waliona vinginevyo. Tunaona ni ajabu kwamba majaji walitoa maamuzi dhidi yetu kwa sababu zote tisa (9) pamoja na sababu za kutumiwa kwa lugha kali kupita kiasi katika kukataa madai yetu.
Taarifa hiyo ya Odinga inaendelea kusema ; Uamuzi huu si mwisho wa harakati zetu, kwa hakika, inatutia moyo kuongeza juhudi zetu za kubadilisha nchi hii kuwa demokrasia yenye ustawi ambapo kila Mkenya anaweza kupata ukamilifu wake. Tunawashukuru wafuasi wetu na Wakenya kote nchini kwa kusimama nasi. Tutakuwa tukiwasiliana katika siku za usoni kuhusu mipango yetu ya kuendeleza mapambano ya uwazi, uwajibikaji na demokrasia.
Mahakama ya juu imeidhinisha Uchaguzi wa William Ruto kuwa rais mteule wa Kenya baada ya kesi iliowasilishwa na mpinzani wake mkuu katika uchaguzi huo Raila Odinga kukosa ushahidi wa kutosha.
Wakitoa uamuzi wao wa pamoja, majaji hao walioongozwa na jaji mkuu Martha Koome walisema kwamba ushahidi uliotolewa na mlalamishi Raila Odinga ulikuwa umejaa uvumi na porojo.
Akiangazia maswala tisa ya kesi hiyo, Jaji Martha Koome amesema kuwa mshindi wa uchaguzi huo William Ruto alifanikiwa kupita kikwazo cha kura asilimia 50 na moja ya kikatiba.
Akitangaza matokeo hayo , mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) Wafula Chebukati, alimtangaza Dkt Ruto kuwa Rais mteule baada ya kupata kura milioni 7,176,141 (asilimia 50.49) dhidi ya milioni 6,942,930 za Bw Odinga (asilimia 48.85) )Prof George Wajackoyah wa Roots Party alifanikiwa kura 61,969 (asilimia 0.44) huku David Mwaure Waihiga wa Agano Party akiibuka wa nne kwa kura 31,987 (asilimia 0.23).
Madai ya kuingiliwa kwa mfumo wa teknolojia wa IEBC
Wakiangazia suala la kuingiliwa kwa tovuti ya matokeo,majaji hao wamesema kwamba hakuna ushahidi kwamba mfumo wa matokeo uliingiliwaBi Martha , alisema kwamba hakukuwa na ushahidi kwamba mtu yeyote aliingilia mfumo wa utumaji matokeo kwa lengo la kuvuruga matokeo.
Aliongezea kwamba tume ilieleza vya kutosha jinsi mfumo ulivyonasa fomu za matokeo zilizowekwa katika tovuti yake na kwamba zote zilikuwa sawa na zile zilizowasilishwa katika kituo kikuu cha kuhesabia kura.
Majaji hawakushawishiwa na madai kwamba teknolojia hiyo ilifeli katika majaribio ya uadilifu, uthibitisho, usalama na uwazi, jaji mkuu anasema.
Mawakili wa walalamishi waliwasilisha ushahidi 'hewa '
Jaji mkuu amesema hakukuwa na ushahidi kwamba fomu za uchaguzi katika tovuti ya matokeo ya mtandaoni zilibadilishwa kutoka fomu za awali zilizochapishwa.
Jaji Koome, katika ukosoaji mkali wa baadhi ya waliowasilisha hati za kiapo, anawaonya mawakili dhidi ya kuwasilisha ushahidi wa kupotosha au kubuniwa.
Katika kesi moja anasema kwamba ushahidi umeonekana kuwa "hewa' /wongo na kupeleka korti kwenye ‘safari ndefu ya sarakasi’
Post a Comment