Featured

    Featured Posts

BABA HALISI ANAPOSISITIZA IBADA NI UZALISHAJI TUMUELEWE

Tegeta, Dar es Salaam
Duniani kote mchezo wa 'Pyramid' haufanywi kabla ya wateja kuandaliwa kwanza. Lazima wateja waandaliwe kwa kutiwa hamasa hadi wafikie kiwango cha juu cha kuamini kwamba mafanikio yanaweza kuja kimiujiza, kwa sababu mtu yeyote hawezi kuamini kuwa anaweza 'kuuza' hela apate utajiri bila kwanza kuamini utajiri wa kimiujiza.

Kwa sababu hiyo, ili mtu aamini kuwa anaweza 'kuuza' hela apate utajiri au anaweza kupata hela bila kufanyakazi katika kuandaliwa aamini hivyo mtu 'huzimuliwa' kwa mbinu za kisaikolojia hadi kiwango chake cha tamaa kizidi uwezo wake wa kufikiri (His megalopsycho must exceed his reasoning capacity).

Na kadri wanavyomzimua mtu wanampima kwa anavyoshindwa kufikiri hadi anashindwa kutambua 'maigizo' hata yaliyo wazi. Anaguswa kwa ukucha anaangukia watu 10 na woote wanaanguka. Wakishaona mtu ameshaamini hivi wanajua 'amepikika akaiva'.

Kwa hapa Tanzania watu wengi hasa vijana ambao hawakuwepo miaka 2000, ukiwaambia kuhusu 'mchezo' wa UPATU ulivyowafilisi watu kutokana na tamaa za utajiri kupitia miujiza, wanadhani hilo neno UPATU ni msamiati tu wa Kiswahili, lakini kitu hicho UPATU ni kifupi cha Chama Cha Mchezo wa Pyramid ambao ulilenga Walimu.

Ilikuwa hivi; Kabla ya 'mchezo' huo kuanza palikuja manabii wake kwanza, wakazichezea akili za Walimu, baada ya kuona  Walimu 'wameiva' Manabii hao wakaongea na Chama Cha Walimu Tanzania (CWT) nao CWT  akaingia 'chaka' wakawahamasisha Walimu wajiunge na huo UPATU.

Viongozi wa CWT wakawa wakidaii "Ualimu ni wito lani wito peke yape hauleti chakula mezani", Bada ya Walimu kupikwa hadi kuiva kutokana na kaulimbiu hiyo ya 'Nabii' CWT, Waalimu takriban Laki mbili (200,000) nchi mzima wakajiunga na UPATU, wenyewe wakidai wamepata mkombozi.

Uongozi wote wa UPATU ulikuwa Manabii! Siku ya siku Walimu wakakuta Ofisi tupu! Ukazuka mgogoro wa Uongozi CWT. Baada ya  UPATA ndipo IPP nao wakaja na mchezo wao ule (kwa anayeukumbuka), kwa bahati nzuri wenyewe Serikali ikaupiga 'Stop' mapema baada ya kuonekana una mushkeli.

Baadaye mwaka 2008 kama sikosei, ukaja 'mchezo' mwingine ulioitwa kwa 'Kimombo' Development Entrepreneurship for Community Initiative (DECI). Nao ukaongozwa na 'manabii'. Pale Kipunguni B Mwakilishi alikuwa Mchungaji mmoja kutoka kabila la Watani zangu Wahaya, mjanja mjanja. Makao Makuu ya DECI Boss alikuwa pia Mchungaji lakini yeye kutoka Kenya.

"Jirani yangu mmoja alinishawishi weee, Aliweka Sh. miloni 3 akapata Sh. milioni 5! Akauza nyumba kwa Sh. milioni 40 kwa mmiliki wa Nduvini Garage, kuingiza kwenye DECI zikazama tiiii!. Akaamua kwenda zake Msongola", rafiki yangu Yahya Msangi ambaye kwa sasa naishi Nchini Togo", anasimulia.


Hatimaye mwisho wa DECI ilikuwa Viongozi wa wake Arbogast Kipilimba, Jackson Mtares, Samwel Mtares, Dominick Kigedi na Timotheo Saiguran ole Loiting’ye, kufikishwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Jijini Dar es Salaam, wakikabiliwa na mashtaka mawili ya uendeshaji wa mradi wa upatu. Lakini hatma ya wanachama 'waliowekeza' mbegu au fedha zao ili wavune utajiri hadi leo sikumbuki ikoje.

Wakati watu wanaendelea kupumbazika hadi kufikia kiwango cha kutarajia miujiza kupata utajiri, hata wahatii akili kwamba hela haiwezi kuzaa hela kirahisi mpaka iingizwe kwenye uzalishaji. yaani iliyopo itumike kununua bidhaa halafu bidhaa ikiuzwa ndiyo hela iongezeke.

Vitendo hivi vya kuwatia ujinga watu hadi 'kuwapuna' hela zao, ukitafakari kwa makini wanaovifanya ni Manabii feki au waungo.  Lakini hata ukijiuliza hivi inawezekanaje, mtu ana virusi vya ukimwi au vijidudu vya Malaria au vya ugonjwa wa maradhi yoyote, halafu akimguswa tu kichwani, ugonjwa upone! yaani virusi, vijidudu viwe ghafla vimeondoka mwilini mwa mgonjwa bila tiba!

"Nchini Togo Serikali imekwishapicha marufuku mambo ya miujiza! Ukidai unafufua unakamatwa kisha unapelekwa 'mochwari' uthibitishe! pia michezo ya Pyramid marufuku. Matapeli ya Kinaija na Kighana hawatii mguu Togo toka 2009. Marufuku!", anasema Yahya Msangi aishiye Togo.

Hapa Tanzania lipo Kanisa moja ambalo naliona kuwa limekuwa mfano bora ambao kila anayetambua athari za kuamaini miujiza ikiwemo ya kujipatia hela za burebure, anaweza kujifunza kupitia Kanisa hilo. Maana lenyewe linakataa kwamba miujiza inaweza kumuinua mwanadamu kwa namna yoyote, linaamini katika utendaji halisi wa Mungu Baba.

Kanisa hilo ni Kanisa Halisi la Mungu Baba, Makao yake Makuu yapo Tegeta Namanga katika mkoa wa Dar es Salaam na Kiongozi wake Mkuu anaitwa Baba Halisi na Waumini wake wanaitwa Uzao Halisi.

Kabla sijaendelea kuandika kuhusu Kanisa hili, kwanza naweka wazi kuwa mimi siyo mfuasi wa Kanisa hili maana mimi ni Muislam, lakini kwa kuwa ni Kanisa rafiki kwangu, nimekuwa mfuatiliaji wa karibu wa Matukio na Ibada zake;

Nimekuwa mfuatiliaji wao kwa sababu mambo mengi ambayo huwa nikiyasikia au kuyaona kwao huniingia akilini; na ukisikia jambo linaniingia akilini ujue hilo ni la maana sana, kwa kuwa mimi ni mdadisi mno ambaye huwa silikubali jambo kirahisi bila kulipima; ndo maana sijawahi kucheza mchezo wowote wa kubahatisha tangu niishi duniani.

Yapo mengi niliyovutiwa na Kanisa Halisi, lakini kuna hili la mambo ya watu kughiribiwa akili na Manabii wa Uwongo katika baadhi ya nyumba za Ibada na mitaani, kwa kuhadaa kwamba ipo miujiza inayoweza kubadilisha maisha ya mtu akapata hela au vitu vya gharama kubwa burebure! ambalo Kanisa Halisi lina mtazao nalo ambao nauona ni Chanya.

Kiongozi Mkuu wa Kanisa Halisi, Baba Halisi katika mafundisho yake, anasema kuwa hakuna tena Ibada ya kutegemea Miujiza bali Sasa Ibada ni uzalishaji;

Baba Halisi anasema, "Wote tumezaliwa tukiwa tunajua Ibada ni kwenda kwenye nyumba za Ibada, kuimba, kutoa matunda (sadaka), na wakati mwingine kulia ili uhurumiwe na Mungu! Daudi katika kitabu cha Zaburi amefundisha hivyo katika mistari mingi kwa habari ya kumlilia Bwana. Ila ukisoma katika Mwa.1:27-28, utagundua kuwa Ibada ni uzalishaji.

Adamu akiwa bado kwenye kitanga cha mkono wa MUUMBA WA KILA KITU, aliambia akazalishe. Alipoumbwa na kuonekana kwa macho katika 'mwa.2:7-15,' alichoambiwa ni kuzalisha! Baada ya kitabu cha Mwanzo kuisha, ibada ni Uzalishaji haikuendelea. Maana hata Ibrahimu, Isaka na Yakobo ibada kwao ilikuwa ni uzalishaji shambani.

Wengi hawaamini hili lakini ni kweli, Ibada ni Uzalishaji; Mwalimu akiwa darasani akafundisha vizuri watoto bila hila, ili wafaulu, hiyo ni Ibada. dereva anayeendesha gari la abiria, akiendendesha kwa upendo abiria wakafika salama bila shida, hivyo ni Ibada. Ni tofauti na tabia ambayo ilikuwa imeshajitokeza ya kujenga nyumba za Ibada maofisini huku wengi wakiamini hiyo ndiyo Ibada. Badiliko limetokea, Ibada ni Uzalishaji, tupokee."

Baba Halisi, Kiongozi Mkuu wa Kanisa Halisi la Mungu Baba akiwa kwenye moja ya Ibada za Kanisa hilo. 

Viongozi wa (DECI) Arbogast Kipilimba, Jackson Mtares, Samwel Mtares, Dominick Kigedi na Timotheo Saiguran ole Loiting’ye, wakiwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, wakikabiliwa na mashtaka mawili ya uendeshaji wa mradi wa upatu, mwaka 2009. 👇


author

Author Name

Author Description!

Get Free Email Updates to your Inbox!

Post a Comment

www.CodeNirvana.in

Magazeti Ya Leo

Copyright © Magazeti ya Leo, Habari Leo Tanzania, Mwananchi, Michuzi, mwanaspoti, nipashe, Udaku | Designed By Code Nirvana