Na Bashir Nkoromo, Blog ya Taifa ya CCM
Kocha wa makipa wa Timu ya Soka ya Simba ambaye pia amewahi kuwa mchezaji wa timu hiyo Ramadhani Said Mohamed Sultan (40) mkazi wa Kigamboni, Dar es Salaam ni miongoni mwa watuhumiwa 9 waliokamatwa kwa tuhuma za kupatikana na dawa za kulevya aina ya Heroin katika Opresheni iliyofanywa na Mamlaka ya kudhibiti na kupambana na dawa za kulevya (DCEA).
Taarifa iliyotolewa jana Novemba 15, 2022 na Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Nchini (DCEA) Gerald Kusaya, imesema katika wahutumiwa hao 9 yumo pia Maulid Mohamed Mzungu maarufu kwa jina la Mbonde (54) mkazi wa Kamegele- Kisemvule ambaye ni ndugu yake na Kocha huyo wa Simba.
"Katika kipindi cha mwezi Oktoba na mwanzoni mwa mwezi huu wa Novemba 2022, Mamlaka ya Kuzuia na kupambana na Dawa za Kuevya (DCEA) kwa kushirikiana na vyombo vingine vya Ulinzi na Usalama vilifanya operesheni katika maeneo mbalimbali nchini na kukamata jumla ya kilo 34.89 za dawa za kuevya aina ya Heroin na 'Biskuti' 50 zilizotengenezwa kwa kutumia dawa za kelevya aina ya Bangi kama moja ya malighafi", amesema Kamishna Jenerali Kusaya.
Kamishna Jenerali Kusaya amesema, katika Operesheni hizo, jumla ya watuhumiwa 11 walikamatwa ambapo mbali na 9 waliokamatwa kwa tuhuma za kupatikana na Heroin wengine watatu (3) walikamatwa wakiwa na 'Biskuti' 50 zilizotengenezwa kwa kutumia dawa za kelevya aina ya Bangi kama moja ya malighafina na kwamba watuhumiwa hao wanaendelea kuhojiwa.
Aliwataja watuhumiwa wengine saba (7) kati ya 9 ambao wanashikiliwa kwa kukutwa na Dawa za kuevya aina ya heroine ni kuwa ni Kambi Zubeir Seif (40) ambaye mmiliki wa Kituo kinachojishughulisha na ukuzaji wa vipaji kimicheo cha Cambiasso Sports Academy kilichopo Tuangoma, Kigamboni na pia mmiliki wa Kampuni ya Safia Croup of Companies ambayo inamiliki magari ya Daladala kutoka Dar es Salaam kwenda mkoa wa Pwani.
Wengine ni John Andrew John maarufu kwa jina la Chipanda (40), mkazi wa Magore Kitunda ambaye pamoja na kuwa mfanyabiashara lakini pia ndiye ana jukumu la kutafuta vijana wenye vipaji na kuwapeleka kituo hicho cha Camboasso Sports Academy kinachomilikiwa na mtuhumiwa mwenzake, Kambi Zubeir Seif.
Said Abeid Matwiko (41) Fundi Seremala, Mkazi wa Magole A Kivule, Rajabu Mohamed Dhahabu (32) ambaye ni mfanyabiashara, mkazi wa Tabata Segerea, Seleman Matola Said (24) ambaye ni mkazi wa Temeke Wailes ambaye ni mtoto wa dada yake na mtuhumiwa Kambi Zuberi Seif, Hussein Mohammed Pazi (41) Mkazi wa Kibugumo Kigamboni na Ramadhani Rashid Chalamila (27) Mkazi wa Mzinga Kongowe.
Kamishna Jenerali Kusaya amesema, katika tukio la pili, Mamlaka ya kudhibiti na kupambana na dawa za kulevya ilimkamata Jijini Arusha Mtuhumiwa mwingine Hassan Ismail (25) mkazi wa Olasiti jijini humo anayesadikiwa kuwa ndiye mtengenezaji wa biskuti hizo zenye dawa za kulevya akiwa pia na dawa za kulevya aina ya bangi.
"Ukamataji huu umefanyika kufuatia opereshani endelevu tunazozifanya katika maeneo mbalimbali hapa nchini. Watuhumiwa hao wameshafikishwa Mahakamani jiji Arusha", amesema Kamishna Jenerali Kusaya na kutahadharisha akisema;
"Matukio ya uwepo wa bidhaa za vyakula vinavyotengenezwa kwa kutumia bangi yameanza kushamiri hapa nchini. Itakumbukwa kuwa mwaka 2020 na 2021 Mamlaka ilikamata bangi iliyosindikwa mfano wa jam keki na asali katika matukio tofauti wakati wa utekelezaji wa operesheni zake.
Hali hii inaonesha wazi kuwa tatizo hili limeanza kushamiri nchini na hasa ikizingatiwa kuwa wafanyabiashara hawa wenye nia ovu hutumia vyakula vinavyopendwa na watoto mfano pipi, keki Ice Cream na biskuti hivyo, kuwepo na uwezekano wa kuwaingiza watoto kwenye matumizi ya dawa za kulevya bila kujua na hatimaye kuwa waraibu. Hivyo natoa mwito kwa wazazi na walezi kufuatilia kwa ukaribu nyendo za watoto wao".
Post a Comment