Na Mashaka Mhando, Handeni
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoa wa Tanga Rajab Abdulhaman amesema watu wanaonuna kwa Rais Samia Suluhu Hassan kuambiwa anaupiga mwingi, wataendelea kukereka kwasababu kazi anazozifanya kwa Watanzania hazina kifani.
Akizungumza mwishoni mwa wiki katika mkutano wa kumnadi mgombea udiwani wa CCM katika kata ya Vibaoni wilayani hapa, Mwenyekiti huyo alisema watu hao wataendelea kununa kwasababu Watanzania wataendelea kusema maneno hayo kuunga mkono jitihada anazozifanya.
"Wapo watu wanachukia yaani ukisimama hapa ukisema Rais wetu mama Samia anaupiga mwingi, eti kuna watu wengine wananuna Rais kuambiwa anaupiga mwingi, wanataka tutumie lugha gani labda kwa haya anayoyafanya kwa Watanzania?," Alihoji Mwenyekiti huyo.
Alisema mtu husifiwa kwa mema anayoyafanya na pia hukosolewa kwa mabaya anayoyafanya lakini kwa Rais Samia mambo anayoyafanya kwa nchi hii ni mambo makubwa na mazuri yanayopaswa wananchi kumuombea kwa Mungu ili awe na afya njema aendelee kutekeleza na kusimamia miradi mikubwa yenye tija kwa nchi.
Alisema wananchi wa Tanga wataendelea kumthamini Rais na watajipanga mwaka 2025 kumpa kura nyingi ili aendelee kuongoza nchi kuendeleza yale ambayo yamepangwa katika ilani ya CCM pamoja na maono aliyokuwa nayo kama Rais.
Mwenyekiti huyo alikumbusha kwamba kipindi hiki cha mwezi Desemba, wananchi wangekuwa wakihangaika kuuza mifugo, mahindi na bidhaa zao nyingine ili kuchangia ujenzi wa vyumba vya madarasa kwa ajili ya watoto waliofaulu darasa la saba kuanza kidato cha kwanza mwakani.
Lakini Rais Samia ametafuta fedha zilizogharamia ujenzi huo nchini kote na hivyo fedha zile wananchi ambazo walikuwa wazitoe kugharamia ujenzi huo, watafanyia shughuli nyingine za maendeleo yao katika familia zao.
"Wananchi nyie mnajua kila inapofika kipindi hiki, mnauza mifugo yenu, mnauza mahindi yenu kwa ajili ya kuchangia ujenzi wa vyumba vya madarasa:
"Lakini Rais ametafuta fedha za kujenga vyumba vya kutosha vya madarasa nchini kote ikiwemo hapa Vibaoni Handeni amemsaidia Mtanzania mnyonge ambaye alikuwa anachangishwa fedha zake kwa kuuza mifugo yake pamoja na mahindi, sasa fedha zako hizo utafanyia maendeleo mengine nyumbani kwako, wewe na familia yako" alisema.
Aliwataka wananchi wa Vibaoni kumchagua mgombea wa CCM kwavile chama hicho ndicho kinachosimamia Maendeleo ya kweli ya nchi na tayari kimeunda serikali wakimchagua mgombea huyo atawawakilisha vizuri na atawaletea maendeleo kwakuwa rais na mbunge walishachaguliwa.
Aliwataka waache kujaribu kuwachagua wagombea wa vyama vya upinzani, kwasababu hawajulikani ofisi zao lakini pia hawana muundo mzuri wa uongozi katika vyama vyao kama ilivyokuwa CCM.
Katibu wa CCM mkoa wa Tanga Suleiman Mzee Suleiman, alisema wilaya za Tanga, Handeni na Lushoto zitafanya uchaguzi Desemba 17 mwaka katika uchaguzi mdogo wa marudio katika kata tatu za wilaya hizo.
Mgombea udiwani katika kata hiyo ya Vibao, Mary Mntambo aliwaomba kura wananchi wa kata hiyo akiwaeleza kwamba anao uwezo wa kusimamia maendelo katika kata hiyo.
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoa wa Tanga Rajab Abdulhaman.
Post a Comment