CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimetoa wiki moja kwa Wizara ya Elimu na TAMISEMI kuanzia leo Januari 20, 2023, kuhakikisha vishikwambi vilivyotolewa na serikali kwa ajili ya walimu vinawafikia walengwa.
CCM Imesema imepokea malalamiko ya kutotekelezwa kikamilifu kwa maelekezo ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kuhusu ugawaji wa vishikwambi hivyo.
Akizungumza Jijini Dar es Salaam leo, Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, Itikadi na Uenezi, Sophia Edward Mjema, alisema wakati akizundua ugawaji wa vishikwambi hivyo Novemba mwaka jana, Waziri Mkuu Majaliwa aliagiza kuhakikisha vifaa hivyo vinakwenda kwa walengwa.
"Ulitengwa muda maalumu wa kutolewa kwa vishikwambi hivyo ambao ulikuwa unaishia Januari 15, mwaka huu, lakini Chama kimepokea malalamiko kwamba hadi leo kuna baadhi ya makundi hayajapata hivyo vishikwambi. Lakini pia kuna baadhi ya wilaya hawajagawa kabisa vishikwambi hivyo.
"Kuna maeneo mengine unakuta walimu wako 10 na wote wanahitaji na wanastahili kupata, lakini unakuta vishikwambi vinatoka vinane wawili wanaachwa.
"Chama kinatoa maelekezo, kinaielekeza wizara husika (Wizara ya Elimu na TAMISEMI) kuhakikisha zoezi hili linakamilika na walengwa wote wanaostahili kuhakikisha wamevipata vishikwambi hivyo, lakini sio hivyo tu bali pia wahakikishe malalamiko haya hayapo na wasimamie zoezi kuona makundi yaliyopaswa kupewa yanafikiwa na wale ambao hawajapata wapate. Baada ya wiki moja tupate taarifa zoezi hili limekwendaje," amesema.
Post a Comment