Featured

    Featured Posts

RC CHALAMILA AANZA MSAKO WA NYUMBA KWA NYUMBA KUWABAINI WANAFUNZI WASIOANZA SHULE

 

Mkuu wa Mkoa wa Kagera Albert John Chalamila akizungumza na waandishi wa habari juu ya maendeleo ya Elimu Mkoani humo.
Sehemu ya waandishi wa habari wakifuatilia maelekezo ya Mkuu huyo wa Mkoa.


Na Lydia Lugakila Kagera.


Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Albert Chalamila ameagiza wakuu wa wilaya, wakurugenzi, wenyeviti wa halmashauri madiwani, walimu wakuu, waratibu elimu kata kufanya msako wa nyumba kwa nyumba kuwabaini watoto ambao hawajaripoti kuanza kidato cha kwanza mwaka 2023.


RC Chalamila ametoa agizo hilo Januari 21, 2023 katika Ofisi za Mkoa huo zilizopo Manispaa ya Bukoba wakati akizungumza na waandishi wa habari juu ya maendeleo ya elimu na hali ya uripoti wa wanafunzi wa kidato cha kwanza mwaka huu


Ametaja kukerwa  na hali ya wanafunzi ambao hawajaripoti kuanza kidato cha kwanza na kuwa wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza walikuwa ni wanafunzi 59,175 ambapo waliokwisha ripoti hadi Sasa ni 35,526 sawa na asilimia 60 pekee huku asilimia 40 wakiwa bado hawajaripoti shuleni.


"Kuanzia sasa wakuu wa wilaya kwa kushirikiana na serikali za halmashauri za kata, tarafa, vijijini kufanya masako wa nyumba kwa nyumba kabla ya mwezi huu kuisha wote waliochaguliwa wawe wamekwishafika katika shule walizochaguliwa"alisema Mkuu huyo wa Mkoa.


Ameongeza kuwa kwa mzazi atakayebainika  amemtorosha mtoto au kufanya vinginevyo atachukuliwa hatua za kisheria  huku akiwahimiza Wakuu wa Wilaya kwa kushirikiana na wakurugenzi kuhakikisha wanapokea ripoti ya kila siku ya wanafunzi walioripoti na wakuu wa shule wahakikishe wanatoa taarifa kwa viongozi hao  ili kuona wapi kuna mkwamo.


Chalamila amesema kuwa Rais Dokta Samia amewekeza kwa kiasi kikubwa katika masula ya madarasa pamoja na miundo mbinu mingine ikiwemo  maabara, vyoo vya wanafunzi, nyumba za walimu huku Mkoa wa Kagera kwa awamu ya kwanza ukiwa umepata madarasa 881, awamu ya pili madarasa 514.


 Ameongeza kuwa alitarajia kuwa kiwango cha wanafunzi waliojiunga na kidato cha kwanza kiwe kikubwa kwa sababu ya hamasa ya uboreshwaji wa miundo mbinu huku akikemea tabia iliyoanza kujitokeza kwa baadhi  wazazi kuwaficha watoto katika shughuli za kiuchumi kuwa watakaobainika watakamatwa na kisha kufikishwa katika  vyombo vya sheria.


Hata hivyo amesema kila shule iwashirikishe wazazi na kuhakikisha  kuwa inatoa chakula cha mchana kama ilivyotamkwa katika waraka no 3 wa elimu wa mwaka 2016 ili kiwe kivutio kwa wanafunzi kubaki shule na kusoma wakiwa hawana njaa.

author

Author Name

Author Description!

Get Free Email Updates to your Inbox!

Post a Comment

www.CodeNirvana.in

Magazeti Ya Leo

Copyright © Magazeti ya Leo, Habari Leo Tanzania, Mwananchi, Michuzi, mwanaspoti, nipashe, Udaku | Designed By Code Nirvana