Featured

    Featured Posts

MAKAMU WA RAIS WA MAREKANI KUTUA NCHINI KESHO, NI MATOKEO YA KUIMARIKA KWA DIPLOMASIA YA TANZANIA

Na Bashir Nkoromo, Blog ya Taifa ya CCM
Makamu wa Rais wa Marekani Kamala Devi Harris, anatua hapa nchini kesho Machi 29, 2023 katika ziara ambayo Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk. Stergomena Tax amesema ni uthibitisho wa uhusiano mzuri kati ya Tanzania na Marekani na matokeo ya kuimarika kwa Diplomasia ya Tanzania.

Akizungumzia ratiba ya Makamu wa Rais Kamala nchini, Dk. Tax amesema, atakapowasili hiyo kesho Kiongozi huyo atapokelewa na Makamu wa Rais Dk. Philip Isdory Mpango na akauwepo hapa Nchini hadi Machi 31, 2023.

Amesema Rais Dk. Samia Suluhu Hassan atampokea rasmi Ikulu jijini Dar es Salaam, keshokutwa Machi 30 2023, na mapokezi hayo yatafuatiwa na mazungumzo baina ya viongozi hao.

Dk. Tax amesema akiwa nchini, Makamu wa Rais Kamala ataweka shada la maua katika Makumbusho ya Taifa Jijini Dar es Salaam, kuwakumbuka walioathiriwa na mabamu yaliyolipuliwa kwenye Ubalozi wa Marekani, Dar es Salaam mwaka 1998.

 Pia atatembelea Taasisi ya Tanzania Startup Association ya Jijini Dar es Salaam, kwa ajili ya kukutana na Wajasiriamali Vijana nakushiriki Futari iliyoandaliwa kwa heshima yake na Mwenyeji wake Dk. Rais Samia.

Waziri Balozi Tax, amesema ziara ya Kamala nchini ni matokeo ya juhudi za Rais Dk. Samia za kukuza na kuimarisha ushirikiano kati ya Tanzania na Marekani, na kwamba ziara hiyo inalenga pamoja na mambo mengine, kuimarisha ushirikiano hususan kwenye maeneo ya kimkakati ya ushirikiano kama biashara, uwekezaji, utalii, elimu, afya na utunzaji wa mazingira.

Amesema uhusiano wa kidiplomasia kati ya Tanzania na Marekani ambao ulianza mwaka 1961 unaimarishwa na Program mbalimbali za ushirikiano kati ya Tanzania na nchi hiyo ambazo kwa kiasi kikubwa zimechangia juhudi za Serikali za kuboresha maisha ya wananchi.

Amefafanua kuwa Tanzania na Marekani zinashirikiana kupitia program mbalimbali ikiwemo Mfuko wa Dharura wa Rais wa Marekani wa Kupambana na UKIMWI (PEPFAR), Mpango wa Rais wa Marekani wa Kupamana na Malaria (PMI) na Feed the Future.

Dk. Tax ameeleza kuwa, Marekani kupitia Program ya PEPFAR imetangaza Bajeti ya miaka miwili ya kiasi cha Dola za 827,801,250 kwa Tanzania kwa kipindi cha kuanzia Oktoba 2024 hadi Septemba 2026.

Amesema, utekelezaji wa program hiyo hapa nchini umechangia kwa kiasi kikubwa kupunguza kuenea kwa maambukizi ya Virusi vya Ukimwi na kuwezesha asilimia 88 ya watu wanaoishi na virusi kujua hali zao, na asilimia 95 kutumia dawa za kupunguza makali ya ugonjwa huo.

Kuhusu uwekezaji wa Marekani nchini, Balozi Tax amesema nchi hiyo kwa mujibu wa takwimu za Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) imesajili jumla ya miradi 266 yenye thamani ya Dola za Marekani Milioni 4,778.6 na kutengeneza ajira zipatazo 54,584 kwa Watanzania.

Makamu wa Rais wa Marekani Kamala Devi Harris
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax akizungumza na Wahariri (hawapo pichani) kuhusu ziara ya Makamu wa Rais wa Marekani, Mhe. Kamala Devi Harris nchini. Mkutano huo umefanyika katika Ofisi Ndogo za Wizara jijini Dar es Salaam tarehe 27 Machi 2023
author

Author Name

Author Description!

Get Free Email Updates to your Inbox!

Post a Comment

www.CodeNirvana.in

Magazeti Ya Leo

Copyright © Magazeti ya Leo, Habari Leo Tanzania, Mwananchi, Michuzi, mwanaspoti, nipashe, Udaku | Designed By Code Nirvana