Featured

    Featured Posts

KANISA HALISI LAICHANGIA SERIKALI KUPUNGUZA WASIO NA AJIRA, WAUMINI WAKE ZAIDI YA 400 WAHITIMU MAFUNZO YA UJASIRIAMALI, LEO

Na Bashir Nkoromo, Tegeta
Licha ya jitihada za Serikali kutoa ajira hasa kwa Vijana, Ripoti ya ‘Tanzania in figures 2021’ inayotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) inaonyesha idadi ya ajira inaongezeka kidogo huku idadi ya watu na wahitimu ikiongezeka kwa kiasi kikubwa.

Ripoti hiyo inaonesha kuwa Idadi ya wenye ajira nchini mwaka 2019 ilikuwa milioni 22.4, kabla ya kuongezeka mwaka 2020 hadi kufika ajira milioni 23 kabla ya kuongezeka kidogo hadi milioni 23.5 mwaka 2021.

Tena ripoti hiyo hiyo ya NBS inaonesha upunguaji mdogo wa ukosefu wa ajira nchini kuanzia mwaka 2017 hadi mwaka 2021.  

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, Mwaka 2017 kiwango cha wasio na ajira kilikuwa asilimia 9.9, mwaka 2018 kilikuwa asilimia 9.7, mwaka 2019 ilikuwa asilimia 9.6 huku mwaka 2020 kikifika asilimia 9.5 kabla ya kufika asilimia tisa mwaka 2021.

Takwimu hizo za kiwango cha ukosefu wa ajira zinaonyesha kupungua kwa kiwango kidogo sana cha wasio na ajira huku wahitimu na idadi ya watu kwa ujumla nchini ikizidi kuongezeka.

Kutokana na hali hiyo, ndiyo sababu taasisi binafsi na za kijamii zinapojitokeza kupunguza changamoto ya wingi wa Idadi ya wasio na ajira kwa kuwaajiri au kuwawezesha kujiajiri hupaswa kupongezwa.

Kanisa Halisi la Mungu Baba lililoanzishwa hapa Tanzania miaka takribani miaka mitano iliyopita, ni miongoni mwa taasisi za Kijamii ambazo zimekuwa zikifanya juhudi za kupunguza Idadi ya Wananchi wasio na ajira kwa kuwajengea waumini wake uwezo wa kujiajiri.

Kwa upande wake, Kanisa hili lenye Makao yake Makuu Tegeta Namanga Dar es Salaam, uungaji mkono wake katika jitihada za kupambana na changamoto ya wasio na ajira hapa nchini, linafanya hivyo ikiwa ni sehemu ya kutimiza msimamo wa mafundisho yake ambao ni 'Ibada ni Uzalishaji'.

Katika kudhihirisha uhalisia wa msimamo wa mafundisho yake hayo ya Ibada ni Uzalishaji, Kanisa hilo limewezesha Uzao au waumini wake zaidi ya 400, kuhitimu mafunzo ya Ujasiriamali na utengenezaji wa bidhaa mbalimbali ili wapate kujiajiri na hivyo kuondokana na umasikini.

Katika mafunzo hayo ambayo yamefanyika kwa siku kumi tangu Machi 22, 2023, chini ya Walimu wabobefu wa fani ya Ujasirimali kutoka Chuo cha Elimu kwa Wote cha Tabata jijini Dar es Salaam, yamefikia tamati leo Aprili 02, 2023 kwa wahitimu wa mafunzo hayo kupewa vyeti vinavyotambulika kisheria.

Shamrashamra za kukabidhiwa vyeti na uuzaji wa bidhaa mbalimbali walizotengeneza Wahitimu, zimefanyika wakati wa Ibada ya Uzalishaji, iliyofanyika Kao Kuu la Kanisa hilo, Tegeta Namanga, Dar es Salaam, ikiongozwa na Kiongozi Mkuu wa Kanisa hilo ndani na nje ya Tanzania, Baba Halisi.

Kwa hatua hiyo bila shaka, mbali na kwamba Kanisa Halisi limetekeleza Sauti ya Chanzo Halisi (Mungu Baba) kwamba Ibada ni Uzalishaji, kwa upande mwingine, limetoa mchango wake wa kuisaidia Serikali katika kupambana na changamoto hiyo ya ukosefu wa ajira hasa kwa Vijana.

Hiyo ni kwa kuwa, kufuatia kuhitimu mafunzo hayo yaliyoambatana na utengenezaji wa bidhaa mbalimbali zikiwemo batiki, sabuni za maji kwa ajili ya matumizi mbalimbali na mafuta ya kujipaka, Wahitimu hao sasa wataweza kujiajiri kupitia ujasiriamali hivyo kulipunguzia taifa mzigo wa Idadi ya watu wasio na ajira.

Ili kuwezesha mafunzo hayo kufanyika Kanisa Halisi chini ya Baba Halisi, liliandaa mazingira wezeshi na vifaa, kisha ndiyo walimu kutoka Chuo hicho wakaingia kuwanoa Waumini hao, na sasa leo wamehitimu wakionyesha kuwa wamefahamu vya kutosha elimu waliyopewa.

Akidhihirisha kufurahishwa kwake na namna Walimu wa Chuo hicho walivyofundisha kwa umahiri na ushirikiano mkubwa licha ya kwamba siyo waumini wa kanisa Halisi, Baba Halisi aliwapa cheti cha Kuthamini huduma waliyotoa, pia akawapa na zawadi ya fedha taslimu zaidi ya Sh. Milioni Moja.

Baba Halisi alienda mbali zaidi kwa kuwaomba Walimu hao, kwenda kufundisha waumini katika Vituo vya Kanisa hilo vilivyopo mikoani, kwa kuanzia na Kibaha mkoa wa Pwani, Arusha, Kilimanjaro, Iringa, Mwanza na kwingineko.

"Tafadhalini sana, nawasihi hawa walimu watakapokuja huko, jitokezeni kwa wingi kupata mafunzo haya na tena amuwape ushirikiano wa kutosha, ninyi watekeleza Sauti wa mikoa watakayojuka hawa, hakikisheni mnasimamia vema, na mimi nitakuwa nakuja huko", akasema Baba Halisi.

Kwa upande wake Mwalimu Kiongozi wa mafunzo hayo Saravai Rashid, aliahidi kuendelea kusaidia kutoa mafunzo mbalimbali ya ujasiriamali kwa waumini wa Kanisa Halisi mapaka atakapohakikisha wameondokana na umasikini.

Alisema, ili kutimiza lengo hilo, atatoa mafunzo kwa wahitimu ya namna ya kuweza kufundisha wengine, jambo ambalo Baba Halisi alilifurahia mno na kumwelezea mwalimu huyu kuwa ni wa kipekee na Chanzo Halisi yumo ndani yake.


Moja Halisi akimkabidhi bahasha yenye zawadi ya zaidi ya Sh. Milioni moja Mwalimu Kiongozi wa mafunzo hayo Saravai Rashid, baada ya Baba Halisi kutoa fedha hizo, wakati wa shamrashamra za tamati ya mafunzo hayo, leo.
Moja Halisi akisoma ujumbe wa Baba Halisi katika Cheti cha kuthamini mchango waliotoa walimu wa mafunzo hayo.


Kisha akamkabidhi Mwalimu Rashid cheti hicho.
Baba Halisi akizungumza wakati wa Ibada iliyoambatana na shamrashamra za kuhitimisha mafunzo ya siku kumi ya Ujasiriamali kwa waumini wa Kanisa Halisi, leo.
Baba Halisi akiwa na fulana lililotengenezwa na wanafunzi wa mafunzo hayo ya Ujasiriamali, fulana hiyo alimzawadia Uzao mmoja. 




Baadhi ya bidhaa zilizotengenezwa na Wanafunzi wa ujasiriamali wakati wa mafunzo hayo ya siku kumi.
Baadaye Baba Halisi alimpa nafasi Mama Halisi kuzungumza, akasema "Mtoto amekuwa na sasa anatembe".

Mtekeleza Sauti kutoka Rwanda naye ni miongoni mwa waliopewa nafasi na Baba Halisi kuzungumza.
 

author

Author Name

Author Description!

Get Free Email Updates to your Inbox!

Post a Comment

www.CodeNirvana.in

Magazeti Ya Leo

Copyright © Magazeti ya Leo, Habari Leo Tanzania, Mwananchi, Michuzi, mwanaspoti, nipashe, Udaku | Designed By Code Nirvana