Featured

    Featured Posts

MAKALA: BABA HALISI KUONGOZA MKUTANO MKUU WA KANISA HALISI UTAKAORINDIMA KESHOKUTWA JUMAPILI, MEI 7, 2023 JIJINI DAR ES SALAAM

NA BASHIR NKOROMO, CCM Blog
Uongozi wa Taasisi yoyote iwe ya Familia, Kijamii, Binafsi Serikali au ya Kimataifa ili kudhihirisha kuwa una haja ya kuijenga na kuiimarisha  taasisi hiyo, lazima uthamini kwa dhati kushirikisha Wadau wa taasisi husika ili wawe na ufahamu usio na shaka kwa taasisi yao.

Zipo njia nyigi za Uongozi kushirikisha wadau, lakini iliyo kubwa na muhimu zaidi ni Uongozi kukutana na Wadau kwa kuzingatia Katiba na Utaratibu ambao unakuwa tayari umewekwa kwa pamoja baina ya Uongozi husika na Wadau hao.

Katika kushirikisha, ndiyo taasisi huweza kuwa madhubutii kwa kuwa yaliyo mema na mazuri na hata changamoto hujadiliwa na kupatikana muafaka au ufumbuzi ulio sahihi kutokana na kukubaliana baina ya Uonhozi na kila mdau au idadi kubwa ya wadau.

Hii ni kwa sababu kutoshirikisha Wadau husababisha baadhi ya Wadau kuinung'unikia au kuijadili taasisi mabaya tu kila wanapokutana katika makutano yasiyo rasmi hali ambayo hudhoofisha taasisi husika, maana huonekana taasisi haina jema hata moja hata kama inayo mema mengi.

Kanisa Halisi la Mungu Baba, ambalo ndilo Kanisa pekee lililoanzia Tanzania na kusambaa mataifa mengine,  lenye Makao yake Makuu, Tegeta Namanga Jijini Dar es Salaam, ni miongoni mwa Taasisi ambazo nionavyo inazingatia vilivyo dhana ya ushirikishaji Wadau hasa Uzao (Waumini) wake kwa dhati na kwa uhalisia.

Naona hivyo kwa kuwa mara kadhaa nimekuwa nikishuhudia Uongozi wa Kanisa hilo ukiwashirikisha wadau na waumini unapotaka kutekeleza mambo mbalimbali kwa ajili ya kujenga afya ya Kanisa ikiwemo masuala ya maendeleo.

Katika kufanya hivyo Kiongozi Mkuu wa Kanisa Halisi ambaye jina lake kamili ni Baba Halisi na safu yote ya Uongozi amekuwa akiridhia bila hila yoyote, kufanyika tena kwa wakati Mkutano Mkuu wa Kanisa hilo kila mwaka na kutoa uhuru kwa wawakilishi halali wa Waumini kujadili kwa uwazi masuala mbalimbali yanayohusu mwenendo na maendeleo ya Kanisa.

Siyo hivyo tu, katika kuhakikisha Uwazi unatamalaki, Baba Halisi huwaalika hadi Wadau wanaolipenda tu Kanisa Halisi lakini siyo waumini, kuingia katika Mkutano Mkuu na kusikiliza kila kitu, ambapo Baba Halisi husema, huwaruhusu kuingia mkutanoni kwa kuwa Kanisa Halisi ni Taasisi ya Kijamii.

Hulka hiyo ya Baba Halisi kuwakaribisha kusikiliza kila kitu katika Mkutano Mkuu naweza kusema ni ya kipekee sana, maana, Taasisi karibu zote za kijamii zinazozijua hualika Watu wa nje kwenye Mikutano yao, lakini waalikwa hao huishia kusikiliza hotuba za ufunguzi tu, lakini kwenye mijadala hawawaruhusu kamwe!

Mwaka jana, Jumapili Mei 8, 2022, sawa na lango la 12 Abibu 1 kwa Kalenda ya Kanisa Halisi, Kanisa hilo lilifanya kwa mafanikio makubwa Mkutano Mkuu, ambao ulifanyika Makao Makuu ya Kanisa hilo, hapo hapo Tegeta Namanga, Jijini Dar es Salaam.

Naweza kuandika kuwa Mkutano huo ulifana mno kwa kuwa ulihudhuriwa na maelfu ya Wajume kutoka nchi nzima na pia tofauti na mikutano mikuu ya Taasisi zingine ambazo wanaokubalika kushiriki huwa ni Wajumbe halali tu Kikatiba, Mkutano huo ulihudhuriwa pia na Wanajamii wa kawaida na kusikiliza kila kitu mwanzo hadi mwisho.

MKUTANO MKUU WA KESHOKUTWA JUMAPILI
Katika mwendelezo wa Udhati wa dhamira yake, Baba Halisi, Mwaka huu ameitisha Mkutano Mkuu mwingine wa Kanisa hilo ambao utafanyika kuanzia asubuhi, siku ya Jumapili ya keshokutwa, Mei 7, sawa na 12 Abibu Majira Halisi kwa Kalenda ya Kanisa Halisi, katika Makao Makuu ya Kanisa hilo (Tegeta Namanga Jijini Dar es Salaam.

Kwa kuwa hata katika Mtori vinyango za nyama huwa chini, bila shaka Mkutano wa mwaka huu utakuwa wa neema zaidi na kuliacha Kanisa Halisi likiwa imara na kukua zaidi, maana imeelezwa kuwa pamoja na mambo mengine, Mada Kuu itakuwa kujadili maendeleo ya Kanisa hilo, kiutendaji na Kiuchumi hasa ikizingatiwa kuwa Uzalishaji ni miongoni mwa miongozo mikuu ya Kanisa hilo.

Akizungumza katika Ibada iliyofanyika Jumapili iliyopita, Aprili 30, 2023, ambayo nilibahatika kuwepo, Baba Halisi alisema Mkutano huo wa mwaka huu tofauti na mikutano iliyofanyika majira zilizopita, utahudhuriwa na Wajumbe watano (5) kutoka kila mkoa hapa nchini, yaani Mtekeleza Sauti na Uzao (waumini) wanne (4) wa kituo husika.

Baba Halisi akikusudia kuwepo uwazi wa dhati na ushrikishwaji halisi katika mkutano huo, Baba Halisi aliagiza Uzao wanne watakaofuatana na Mtekeleza Sauti, wawe wameteuiwa na Uzao wenzao badala ya kuteuliwa na Watekeleza Sauti.

Pia Baba Halisi alisema, mbali na Wajumbe kuwa Watekeleza Sauti na Uzao wa Vituo vya Kanisa hilo hapa Nchini, Watekeleza Sauti na Uzao kutoka Vituo vilivyoko Mataifa ya Nje nao watatakiwa kuhudhuria lakini wao watakuwa wasikilizaji au mashuhuda (Obsevers), kwa kuwa kwa wakati wao Watafanya Mikutano yao mikuu huko waliko.

"Watekeleza sauti wa Vituo vyetu vya Nchi za nje nao waje kusikiliza kama 'Obsevers', maana wao watafanya mikutano yao mikuu huko, isipokuwa kila watakapofanya Moja Halisi atakuwa anakwenda. Wakifanya Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi, Msumbiji, Zambia, Marekani na kwingineko kote Moja Halisi itabidi lazima awepo na hatachoka kuwepo.", akasema Baba Halisi.

Baba Halisi alisema, kama ilivyo desturi, kwenye Mkutano huo Mkuu Mada mbalimbali zitajadiliwa hasa kuhusu mwenendo na maendeleo ya Kanisa, ikiwemo kujadili rasilimali mapato na matumizi, kwa uwazi halisi.

Alisema, moja ya jipya litakalojitokeza ni uzinduzi rasmi wa Kampuni ya One Up, ambayo imeanzishwa na Kanisa hivi karibuni, ikianza kwa kutengeneza maji ya kunywa ya One Up, ambayo baada ya uzinduzi huo mbali na maji izalisha kikamilifu bidhaa nyingine tano alizozitaja kuwa ni, Nafaka, Sabuni, Mafuta ya kujipaka na dawa za kusafisha sakafu za 'tiles'. Bidhaa hizo zimeshaanza kuzalishwa na zimeonekana kuwaa na ubora wa hali ya juu.

Aidha katika Ibada hiyo, Baba Halisi alimteua Uzao msomi Dk. Paul kuwa Mratibu Mkuu wa Miradi ya Kanisa Halisi ambapo baada ya kumuita mbele, alimpaka mafuta ya Sauti, kisha akasema, "Kama mnavyojua Kanisa letu sasa limekua na lina miradi, sasa Dk. Paul ndiye anakuwa Mratibu wa miradi yetu yote, ukiwa na jambo kuhusu miradi muone huyu. Sikumteua kwa sababu ni Mchumi, hapana, ni kwa kuwa Chanzo Halisi yumo ndani yake, naomba mmpokee".

SASA HILI NDILO KANISA HALISI
Baada ya kueleza japo kidogo habari ya Mkutano Mkuu huo wa Jumapili ya keshokutwa, na kundika Kanisa Halisi chini ya Baba Halisi kuwa ni miongoni mwa Taasisi zilizojipambanua katika kuhakikisha halifanyi jambo lolote kwa siri, bali hushirikisha Uzao na jamii kupitia mikutano, nimenijia wazo kwamba itakuwa vema pia kuwaandikia japo kidogo kuhusu Kanisa hilo lilivyoanza na sura yake ilivyo.

Kama ambavyo Kiongozi Mkuu wa Kanisa Halisi la Mungu Baba, Baba Halisi alivyoandika katika Kitabu cha Ufahamu Ulioanzia Tanzania kwenda Mataifa mengine ambacho kilizinduliwa Jijini Arusha na mimi nikabahatika kuwepo, ni kwamba Kanisa Halisi la Mungu Baba lilikuja baada ya Sauti saba kumaliza majira yake.

Kitabu hicho Baba Halisi ameandika kuwa, katika Kitabu (Biblia) kuna Mfululizo wa Sauti Kuu Saba za Mungu Baba ambazo ni 1. Kerubi (Ezekiel 28:15), 2. Adamu wa Kwanza (Mwanzo 2:15), 3. Musa (Kutoka 3:1), 4. Eliya Mtishibi (1Wafalme 17:1), 5. Yesu (Matendo ya Mitume 10:38), 6. Eliya Adamu wa Pili (Yohana 9:7) na 7. Miaka 1000 (Isaya 33:6).

Kwamba kwa mujibu wa Luka 13:6-7, Waliotumwa wote saba walifanya kazi kwa miaka mitatu peke yake. Hata Musa ambaye imeandikwa kuwa alifanya kazi kwa muda wa miaka 40, mbele za Mungu Baba ni miaka mitatu peke yake kwa maana ya tangu alipopokea torati na wakati alipopiga mwamba mara mbili. Miaka 1000, alimpisha Mungu Baba ili yeye ndiye aongoze Kanisa, baada ya kuona wote waliomtangulia waliishia njiani.

Hivyo kutokana na Kitabu Baba Halisi anafundisha kuwa Sauti Mpya ambayo ni zaidi ya hizo Saba, ni iliyosikika wakati wa Hija ya pili Mjini Kigoma, Lango la 26Thebeti,1 (25 Mei 2019), ambayo ndiyo iliyokuja kulisimamisha zaidi Kanisa Halisi na pia ndiyo iliyosimamisha Tanzania kuwa Taifa Baba na Bara la Afrika kuwa Bara la Nuru tofauti na lilivyokuwa linajulikana zamani kuwa ni Bara la giza.

Anafundisha pia kwamba, Sauti hiyo Mpya ndiyo ililivusha Kanisa Korongo la giza kwa mujibu wa 2Wakorintho 4:6. Korongo hilo liko baada ya Kitabu cha Ufunuo wa Yohana ambacho Baba Halisi anabainisha kuwa ndicho cha mwisho katika Mfululizo wa orodha ya vitabu 66 vya Biblia na kufafanua kuamba Waliotumwa wote, kama walivyoorodheshwa (katika paragrafu ya pili ya makala hii), hawakuweza kulivuka hilo Korongo na hata aliyewateka ambaye anajulikana kama Ishara ya kwanza Mbinguni kwa mujibu wa Ufunuo 12:1, hawezi kulivuka.

Baba Halisi anabainisha kuwa huyo Ishara ya kwanza ndiye aliyeanzisha ugonjwa wa UVIKO 19 (Corona) lakini kwa kuwa Taifa la Tanzania liko ng’ambo ya Korongo la giza, akashindwa kuruka kuuleta Tanzania kwa kuwa yeye mwenyewe haruhusiwi kulivuka hilo Korongo ambalo Watanzania wamevushwa kwa upendeleo wa Mungu Baba.

"Sasa kuna Sauti ya Moyo ambayo ndiyo imesababisha kutimia alichosema Yesu katika Mathayo 21:43, zaidi ya Miaka Elfu Mbili (2000) iliyopita kuwa Ufalme wa Mungu Baba utahama kutoka Mashairki ya Kati kwenda Taifa lingine ambalo wakati huo hakulitaja, lakini sasa imejulikana kuwa ni Tanzania", amefafanua Baba Halisi.

UTAMBULISHO WA KANISA HALISI
Kanisa Halisi la Mungu Baba lilitambulishwa kwa mara ya kwanza kwenye Mkutano uliofanyikia Mji mdogo wa Namanga nchini Tanzania 25 Abibu, 1 (15 Septemba, 2018) mbele ya Vituo vyote vya Kanisa hilo vya Tanzania, Kenya na Zambia, ikiwa ni mwaka mmoja baada ya Nafsi ya Baba, kwa mujibu wa Nafsi Tatu za Mungu katika 1Yohana 5:8, kuja Juu ya Nchi Mwaka 2017 kupitia Tanzania.

Hivyo, Kanisa Halisi la Mungu Baba limeanzia Tanzania kwa Sauti ya Mungu Baba Mwenyewe, ingawa kuna wanaochanganya Kanisa hilo Halisi la Mungu Baba na Siloam, bila kujua kuwa kila aliyetumwa  kwa mujibu wa Yohana 9:7 ni Siloam, ikiwa na maana ya dini na dhehebu lolote linalotokana na Kerubi, Adamu, Musa, Eliya Mtishibi, Yesu, Eliya Adamu wa Pili.

Ni Kanisa Halisi la Mungu Baba peke yake ambalo siyo Siloam kwa kuwa limeanza baada ya kukoma majira ya wote waliotumwa. Uthibitisho wa jambo hili ni jinsi Kanisa Halisi linavyofanya kazi pamoja na Taifa wakati Musa hakufanya kazi na Mfalme Farao, Eliya Mtishbi hakufanya kazi na Mfalme Ahabu na Yesu hakufanya kazi na Mfalme Herode.

Kwa mujibu wa mafundisho ya Baba Halisi Kanisa Halisi la Mungu Baba linaongozwa na Sauti ya Mungu Baba, ambayo husikika kila lango (siku) kwa aliyekusudiwa na Mungu Baba Mwenyewe hasa ikijulikana kuwa suala la kuisikia Sauti ya Mungu Baba siyo geni, maana limeandikwa katika Kitabu sehemu nyingi.

Hata hivyo, kuna dalili kwamba Dunia na ulimwengu kwa sasa wanapata shida kwa kuwa hawakudhani kama kuna Muafrika au Mtanzania anayeweza kuisikia Sauti ya Mungu Baba kila siku na kufundisha wengine kwa ufasaha alichosikia, na pia kukiandika kwenye vitabu.

Katika kudhihirisha, Ufahamu unaotokana na Sauti hiyo, Ufahamu huo ulizinduliwa rasmi 26 Eluli, Vol.1 (6 Disemba, 2020)  Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam, mbele ya Umma wa  Watanzania na Mataifa yote yaliyoizunguka Tanzania.

DIRA YA KANISA HALISI
Kwa mujibu wa Baba Halisi, baada ya aliyepokea Sauti ya Saba, kumpisha Mungu Baba, Dira ya Kanisa anayo Mungu Baba mwenyewe, maana kwa mujibu wa Isaya 57:15 sasa Mungu Baba anaishi ndani ya Moyo wa kila mmoja anayemkubali.

Baba Halisi anasema, hili linathibitishwa na Sauti inayofundishwa kila siku inayoonyesha wazi kuwa Mungu Baba alikusudia asiwepo maskini hata mmoja. Ndiyo maana Kauli Mbiu ya Kanisa Halisi la Mungu Baba ni; 1. Utawala wa Amani (Isaya 2:4), 2. Upendo Usiobagua (1Wakorintho 13:13,  na 3. Kuzalisha kwa kuanza na ulichonacho (Mwanzo 2:15).

VITUO VYA KANISA HALISI
Kanisa hadi sasa lina vituo takriban 300 ambavyo vipo kila mkoa nchini Tanzania na za zaidi ya hapo Kanisa lina Vituo katika Mataifa yote yaliyoizunguka Tanzania na pia lina vituo Marekani na Ujerumani, huku kukiwa na mamilioni ya Wafuasi wanaofuatilia masomo kwenye Youtube na Whatsapp kila siku.

"Msisitizo siyo watu kuwa kwenye majengo, bali ni kukubali msamaha bure wa Mungu Baba (Isaya 43:25) ili wawe uzao wake. Mfano Tanzania wamefikia zaidi ya 1,000,000, Kenya zaidi ya 30,000, Marekani zaidi ya 10,000, ila hawako ndani ya majengo. Wafuasi wa aina hii wako katika mataifa karibu 130. Wanatafsiri Kiswahili kwa lugha zao kwa kuwa wanapenda kujua unawezaje kuisikia Sauti ya Mungu Baba na kuifundisha kwa wengine", anasema Baba Halisi.

MWELEKEO WA KANISA HALISI
Kila Mwezi Mataifa yaliyopokea Ufahamu huo huwa wanafika mara moja Makao Makuu ya Kanisa Halisi la Mungu Baba, Tegeta Namanga jijini Dar es Salaam, Tanzania, kuhudhuria Ibada kwa mujibu wa Isaya 66:23.  Aidha, Kila Mwaka wafuasi ndani na nje ya Tanzania wanakwenda Hija Mkoani Kigoma, kwenye Chanzo cha Sauti.  na kwa mujibu wa takwimu za mitandao ya kijamii hasa YouTube, Mafundisho yanafika katika mabara yote saba Duniani.

Katika hali inayoonyesha kuwa Kanisa Halisi la Mungu Baba linazidi kutanuka licha ya kuwa na umri wa miaka mitano tu, sasa kadri kila taifa linavyoendelea kujua Kiswahili Kanisa hilo hufungua vituo vyake, Hapa nataka nikukumbushe kuwa kwa mujibu wa Baba Halisi Ibada zote za Kanisa hilo huendeshwa kwa Lugha ya Kiswahili katika Mataifa yote.

Hata hivyo Baba Halisi anasisitiza kuwa Uzao wa Mungu Baba siyo lazima wawe ndani ya Kanisa Halisi la Mungu Baba, kama ambavyo Watanzania wote wamejikuta ni chanzo cha Baraka, ingawa si wote wako ndani ya Kanisa hilo.

Kiongozi Mkuu wa Kanisa Halisi la Mungu Baba Ndani na Nje ya Tanzania, Baba Halisi, akiendesha Ibada, Makao Makuu ya Kanisa hilo, Tegeta Namanga Jijini Dar es Salaam, Jumapili iliyopita ya Aprili 30, 2023, na kutangaza kwa furaha kufanyika Mkutano Mkuu wa Kanisa hilo.
author

Author Name

Author Description!

Get Free Email Updates to your Inbox!

Post a Comment

www.CodeNirvana.in

Magazeti Ya Leo

Copyright © Magazeti ya Leo, Habari Leo Tanzania, Mwananchi, Michuzi, mwanaspoti, nipashe, Udaku | Designed By Code Nirvana