Featured

    Featured Posts

RAIS WA UJERUMANI AWAOMBA RADHI WATANZANIA KWA MADHILA YA UKOLONI, ATEMBELEA MAKUMBUSHO YA VITA VYA MAJIMAJI, SONGEA, LEO

Na CCM Blog/DW
Rais wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier amesema anaona aibu kwa yale yaliyofanywa na Wajerumani enzi ya utawala wao wa kikoloni katika iliyokuwa Tanganyika na amewa radhi Watanzania kwa yale yaliyofanywa dhidi yao wakati huo.
 

Ameeleza kusikitishwa kwake na kile alichokiita fedheha ya uhalifu uliofanywa na Ujerumani wakati ilipokuwa ikiitawala nchi hiyo ya Afrika Mashariki, enzi ya Ukoloni, "Ningependa kuomba msamaha kwa kile Wajerumani walichowafanyia wazee wenu hapa'' akasema Rais Steinmeier.

Rais Steinmeier amesema hayo leo alipotembelea makumbusho ya Vita vya Maji Maji yaliyoko katika mji wa Songea, mkoani Ruvuma, akiwa katika siku ya tatu ya ziara yake ya kikazi hapa nchini Tanzania.

Amesema anafahamu jinsi Watanzania ambavyo bado wanabeba mzigo mkubwa kwenye mioyo yao kutokana na madhila hayo huku pia akitambuwa kwamba kilichotokea ni unyama unaoendelea kuviathiri vizazi vingi pamoja na familia.

Tanzania ambayo wakati huo ilifahamika kama Tanganyika ilikuwa kile kilichoitwa Afrika Mashariki ya Ujerumani, ikizijumuisha Burundi, Rwanda,Tanganyika na sehemu ya Msumbiji, ikashuhudia moja ya vita vilivyosababisha umwagaji mkubwa wa damu katika historia ya ukoloni kati ya mwaka 1905 hadi 1907.

Rais huyo wa Ujerumani pamoja na kueleza fedheha iliyosababishwa na madhila hayo amesema nchi yake iko tayari kushirikiana na Tanzania kuelekea mchakato wa pamoja wa kuyaangalia madhila hayo ya kihistoria, huku akitilia mkazo kwamba kilichotokea ni historia ya pamoja kati ya Ujerumani na Tanzania inayowahusisha wazee waliotangulia wa pande zote mbili.

Ameahidi kuufikisha ujumbe nchini Ujerumani kwa yaliyotokea ili watu wengi zaidi nchini Ujerumani wayafahamu. Kadhalika aliwaahidi Watanzania kwamba atahakikisha kwamba Wajerumani watakuwa tayari kuyatafuta majibu kwa pamoja na Watanzania ya maswali ambayo hayajapatiwa ufumbuzi na ambayo yanawakosesha usingizi Watanzania.

Ziara yake katika makumbusho ya vita vya Majimaji imefanyika katika siku ya mwisho ya ziara yake ya siku tatu nchini Tanzania ambapo pia ametangaza kufungua milango ya kurudishwa kwa vitu vya urithi wa kale vilivyoibwa enzi ya Ukoloni. Ujerumani iko tayari kwa ushirikiano kwa ajili ya kurudishwa kwa vitu vya kale vya sanaa pamoja na mabaki ya binadamu.

Rais Frank-Walter Steinmeier baada ya kuweka shada la maua katika makumbusho ya waliouwawa katika vita vya majimaji. Picha:  Bernd von Jutrczenka/dpa/picture alliance

Rais Frank-Walter Steinmeier akitoa heshima baada ya kuweka shada la maua na mmoja wa kizazi cha mashujaa wa vita vya Maji Maji, katika Makumbusho ya vita hivyo, mjini Songea, leo. Picha: Bernd von Jutrczenka/dpa/picture alliance
author

Author Name

Author Description!

Get Free Email Updates to your Inbox!

Post a Comment

www.CodeNirvana.in

Magazeti Ya Leo

Copyright © Magazeti ya Leo, Habari Leo Tanzania, Mwananchi, Michuzi, mwanaspoti, nipashe, Udaku | Designed By Code Nirvana