Na Bashir Nkoromo, CCM Blog
Makamu wa Rais Dk. Philip Mpango amefuta uzushi uliokuwa ukizagaa katika baadhi ya mitandao ya Kijamii na kusema kwamba alikuwa nje ya Nchi kufanya shughuli maalum kwa mwezi mmoja na ni mzima wa afya huku akiwaasa wanaotumia mitandao hiyo vibaya kuacha kwa kuwa inaumiza wengi na kusababisha vilio.
Dk. Mpango amefuta uzushi huo Jumapili, Disemba 10, 2023, alipozungumza baada ya kushiriki Ibada katika Kanisa Katoliki, Parokia ya Mwenyeheri Maria Theresa Ledochowska, Kiwanja cha Ndege mkoani Dodoma, abada ilioongozwa na Padre Dionis Paskal Safari.
"Asanteni sana kwa kuniombea, wamesema mengi na wengine bado wanasema mimi ni mzuka. Sasa wale mnaopenda kusoma biblia, labda niwakumbushe sehemu moja halafu mtamalizia. Zaburi ya 100:18 aya ya 17 inasema sitakufa nifanyeje.... Kwa hiyo mkae na amani nipo salama nilikwenda nje kufanya shughuli maalum kwa takribani mwezi mmoja sijapungua hata kidogo, si ndiyo." akasema Dk. Mpango na kuongeza,
"Mitandao ni mizuri lakini baadhi ya watu wanaitumia visivyo, mnaona kilio cha babu, inaumiza watu wengi, mnaona vijukuu vyangu vile havijaniona mwezi, vimeniona vimekimbia kuja kunifuata pale, lakini wapo watu wengi sana ambao wameumizwa na maneno ambayo hayana msingi, kwa hiyo tujitahidi sana kutumia mitandao ipasavyo kwa kumuogopa Muumba.
Kwa hiyo wale waliokuwa wanatuma picha yangu na mshumaa pembeni, siyo huu. Wengine wanasema mzee amekata moto, bado kabisa kazi ambayo Muumba alinituma sijaimaliza, wakati utakapofika nitarejea kwa Muumba wangu.
Kwa hiyo asanteni sana najua mumeniombea kweli, nimewaona Masista pale walitoa machozi na mimi nikatoa ya kwangu kwenye gari, basi Mungu awabariki sana".




Post a Comment