Kigurunyembe, Morogoro.
Serikali imesema, Shule teule 96 za Sekondari zitaanza mwaka huu wa 2024, kufundisha masomo ya Amali, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa mitaala mipya iliyoboreshwa 2023.
Hayo yamsemwa na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dk. Franklin Rwezimula, akifungua mafunzo ya siku mbili kwa walimu wa shule teule 28 za serikali na 68 zisizo za serikali ambazo zitaanza kutoa elimu ya sekondari mkondo wa Amali katika awamu ya kwanza, yaliyoanza leo Januari 8, 2024 katika Chuo cha Ualimu Morogoro.
Dk. Rwezimula, amemshukuru Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwamba maono yake yameleta msukumo wa maboresho makubwa ya Sera ya Elimu na Mafunzo ya Mwaka 2014 Toleo la 2023.
Naibu Katibu Mkuu, amepongeza Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (NACTVET) kwa kukamilisha kazi ya ukaguzi wa shule teule, Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) kwa kuongoza maboresho ya Mitaala ya Elimu pamoja na VETA kwa kazi ya kusimamia maandalizi ya utekelezaji wa Mitaala ya Elimu ya Amali.
Nae Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) Dk. Aneth Komba, amesema Elimu ya Sekondari Hatua ya Chini itaendelea kutolewa kwa muda wa miaka minne na imegawanyika katika mikondo miwili: Mkondo wa Elimu ya Jumla na Mkondo wa Elimu ya Amali.
“Mkondo wa Elimu ya Amali umegawanyika katika michepuo ikiwemo ya fani za Kilimo na ufugaji, Umakenika, Sanaa Bunifu, michezo, Ufugaji wa nyuki na Urembo.
Pia Mwanafunzi atasoma masomo ya Hisabati, Elimu ya Biashara, Kingereza na Historia ya Tanzania na Maadili ili kupata stadi za msingi katika mawasiliano, stadi za maisha na uzalendo’’, alisema Dkt. Komba.
Kwa upande wake Katibu Mtendaji wa NACTEVET Dkt. Adolf Rutayuga amesema mitaala inayotolewa imetengenezwa na VETA na kuhakikiwa na NACTVET, hivyo amezishukuru Taasisi hizo kwa kushiriki kikamilifu kukamilisha kazi hizo kwa ufanisi.
Naibu katibu Mkuu Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia Dk. Frankilin Rwezimula, akifungua mafunzo ya Mtaala ulioboreshwa yaliyokuwa mahususi kwa walimu wa shule za sekondari za serikali na zisizo za serikali ambazo zinatekeleza mtaala wa sekondari mkondo wa Amali, katika awamu ya kwanza, yaliyofanyika katika Chuo cha Ualimu, Morogoro, leo Januari 8, 2024.
Post a Comment