Na Ashrack Miraji, Same Kilimanjaro
Mbunge wa Same Magharibi, DKT David Mathayo amesema michezo huwajenga vijana kuwa na mahusiano mazuri Katika nyanja mbalimbali na kuweza kutimiza ndoto zao pia kuachana na vitendo viovu kama ukabaji na kutumia madawa ya kulevya, bangi na mirungi.
Hayo ameyasema wakati akifanya mahojiano na mwandishi maalumu katika kuelekea uzinduzi wa Dkt. Mathayo Cup Novemba 26, 2023 katika Jimbo la Same Magharibi mkoani kilimanjaro ambazo Timu 56 zitakwenda kushiriki mashindo hayo
"Dhamira yangu kwa vijana ni kubwa mno, ni kutaka kuona wanafika mbali na kutimiza ndoto zao hivyo nitakuwa nao bega kwa bega katika kuleta maendeleo chanya kwenye jimbo letu la Same Magharibi kuhakikisha nakuza vipaji vyao," alisema Dkt Mathayo.
Dkt Mathayo amesema pia Mathayo Cup hii ni jitihada za kumuunga mkono Mhe Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan katika sekta za michezo, tumeona Rais akifuatilia kwa ukaribu michezo mbalimbali na kuzipa timu zetu hamasa katika mashindano ya kimataifa na mimi kama muhimu wake katika Jimbo la Same Magharibi nitahakikisha vijana wa Same Magharibi wananufaika Katika michezo na shughuli mbalimbali za kiuchumi.
"Pia nisiwe mchoyo wa fadhira na niseme ukweli wa dhati kwa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan amenifanyia makubwa katika jimbo langu, amenijengea vituo vya afya, barabara shule namshukuru sana kwa mchango wake mkubwa hasa kwa wananchi wa jimbo la Same Magharibi hivyo niwaombe wananchi wa jimbo langu kuendelea kumuunga mkono Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anayoifanya katika kuleta maendeleo kwenye jimbo letu na Taifa."

Post a Comment