Waziri Mkuu wa Sudan amewaidhinisha mawaziri 14 wa baraza lake la mawaziri; ambao ni wa kwanza kuteuliwa tangu kupinduliwa utawala wa muda mrefu wa rais wa nchi hiyo Omar al Bashir mwezi Aprili mwaka huu.
Uteuzi huo unawajumuisha Waziri wa Mambo ya Nje wa kwanza mwanamke na Mchumi wa zamani wa Benki ya Dunia ambaye ameteuliwa kuwa Waziri Mpya wa Fedha wa Sudan ambaye atakabiliana na changoto ya mgogoro wa kiuchumi ulioiathiri pakubwa nchi hiyo katika miezi ya karibuni.
Waziri Mkuu wa Sudan Abdallah Hamdok amewaidhinisha mawaziri hao wawili pamoja na wengine wapya 12. Mwanamama Asmaa Abdallah ameteuliwa kuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ibrahim El Badawi Waziri wa Fedha wa serikali hiyo ya kipindi cha mpito ya Sudan. Serikali ya mpito ya Sudan itafanya kazi chini ya usimamizi wa Baraza la Utawala wa Mpito litakaongozwa na wajumbe 11 wakiwemo sita wa kiraia na wanajeshi watano; na litaongoza kwa muda wa miaka 3 kuelekea uchaguzi mkuu. Shirika la habari la Sudan SUNA jana liliripoti kuwa, Waziri Mkuu Abdallah Hamdok anatazamia kutangaza baraza kamili la mawaziri siku mbili zijazo.
Post a Comment