Mufti wa Tanzania Sheikh Abubakar Zubeir amesema, kwa dini ya Kiislamu, mtoto wa kike akivunja ungo anaruhusiwa kuolewa ikiwa atahitajika kufanya hivyo. Hata hivyo ameongeza kuwa, kwa maslahi ya elimu, mtoto huyo atapaswa kusubiri mpaka umri wa miaka 18 na kuendelea.
Mufti Zubeir ametoa msimamo huo baada ya kuulizwa alivyopokea uamuzi wa Mahakama ya Rufani ya Tanzania kukubaliana na hukumu ya Mahakama Kuu ya kubatilisha vifungu za Sheria ya Ndoa ya mwaka 1971 vinavyoruhusu mtoto wa chini ya miaka 18 kuolewa.
Sheikh Abubakar Zubeir amefafanua kwa kusema: "Sisi watu wa dini tuna maneno yetu tunazungumza; ikiwa mtoto anaendelea na masomo na katika kuendelea kwake na masomo atalazamika asome (basi) amalize masomo, kwa maslahi ya elimu. Lakini ikiwa hakuna jambo lolote, huwezi kumuacha akae tu mpaka afikishe miaka 18 afanye ufisadi; ikifikia suala la namna hiyo apate mume aolewe tu, sharia ya Kiislamu mtoto akibalehe anatakiwa aolewe, endapo litatokea suala la kuolewa."
Kauli hiyo ya Mufti wa Tanzania ni ya kwanza kutolewa na kiongozi wa juu wa Kiislamu tangu Mahakama ya Rufani ilipotoa hukumu yake kukubaliana na uamuzi wa mahakama ya chini kuhusu ndoa za utotoni.
Bado serikali ya nchi hiyo, ambayo sasa inatakiwa kufanya mabadiliko katika sheria hiyo ya ndoa ndani ya mwaka mmoja, haijatoa msimamo wake baada ya rufani yake ya kupinga hukumu ya Mahakama Kuu kugonga mwamba…/
Post a Comment