Rais Erdogan amekiambia chama chake tawala kuwa Uturuki haitosita kuanzisha operesheni zake iwapo wapiganaji wa Kikurdi hawatokuwa wameondoka kilomita 30 kutoka eneo la kaskazini au iwapo kundi hilo litaanzisha mashambulizi dhidi ya vikosi vya Uturuki. Amesema Uturuki itatoa majibu makali kwa shambulizi la aina yoyote litakalofanywa dhidi yake huku akisema watapanua eneo lao salama.
Uturuki imetangaza kuanzisha doria ya pamoja na Urusi siku ya Ijumaa kaskazini mashariki mwa Syria, kufuatia makubaliano ya kusimamisha mapigano yaliosimamiwa na Urusi yaliotaka wapiganaji wa Kikurdi kuondoka na kuelekea upande wa kusini ili kulifanya eneo la kaskazini kuwa eneo salama.
Hilo linatokea wakati kukiarifiwa mapigano makali kati ya vikosi vya Syria na Uturuki katika mji wa mpakani wa Ras al Ain ambako Uturuki inalenga kulifanya eneo lake salama. Uturuki ilianzisha operesheni za kijeshi kaskazini mashariki mwa Syria mapema mwezi huu kwa nia ya kuwaondoa wapiganaji wa Kikurdi wa Syria kutoka eneo hilo. Uturuki inaliona kundi hilo kama kundi la kigaidi linalofungamana na waasi waliopo nchini mwake.
Kando na hayo hii leo pia Rais Erdogan amepuuzilia mbali hatua ya baraza la wawakilishi nchini Marekani kutambua mauaji ya halaiki ya Waarmenia akisema ni jambo lililokosa thamani na tusi kubwa kwa watu wa Uturuki.
Waziri wa mambo ya kigeni wa Uturuki Mevlut Cavusoglu amesema uamuzi huo uliofanywa hapo jana ni wa kulipiza kisasi hatua ya Uturuki nchini Syria. Uturuki inakanusha vikali madai ya mauaji ya halaiki kwa watu wa Armenia na kusema maelfu kwa maelfu ya Waarmenia na Waturuki waliuwawa kutokana na Vita vya Kwanza vya Dunia.
Ujumbe wa Syria wakutana Geneva
Huku hayo yakiarifiwa mjini Geneva ujumbe kutoka serikali ya Syria, upinzani na mashirika ya kiraia wamekutana kwa mara ya kwanza hii leo kujadili kuunda katiba ya nchi hiyo hatua iliyotajwa na mpatanishi wa Umoja wa Mataifa kwa Syria Geir Pedersen kuwa jukumu muhimu linaloweza kuiondoa nchi hiyo katika mgogoro wa takriban miaka 9.
Pedersen amezitolea mwito pande zote mbili kuwa wavumilifu na kuendelea kutaka kutafuta suluhu ya matatizo yao huku akionya kuhusu mambo kama mashambulizi ya kigaidi na mapigano yanayoweza kuchelewesha mazungumzo yaliochukua miezi mingi kuyapanga. Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres ameyataja mazungumzo hayo kuwa hatua muhimu ya kutengeneza mazingira ya kuwepo kwa suluhu ya kisiasa. Mataifa kama Iran, Urusi, Uturuki na Marekani wanayafuatilia kwa karibu mazungumzo hayo.
Katika mkutano wa amani ya Syria ulioandaliwa na Urusi mwaka 2018, makubaliano yalifikiwa ya kuunda kamati ya watu 150 ya kuunda katiba mpya ya taifa hilo linalokumbwa na vita, itakayokuwa muhimu kuandaa uchaguzi na suluhu ya kisiasa kwa mgogoro uliosababisha mauaji ya zaidi ya watu 400,000.
afp,ap,reuters
Post a Comment