Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) imemhukumu kifungo cha miaka 30 jela mbabe wa zamani wa vita katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Bosco Ntaganda baada ya kumpata na hatia ya kufanya ukatili ikiwa ni pamoja na kuua, kubaka na kuwatumikisha watoto kama askari vitani.
Tarehe 18 Julai Ntaganda alipatikana na hatia ya kufanya jinai dhidi ya binadam na jinai za kivita zilizofanyika wakati alipokuwa mkuu wa kundi la wanamgambo wa Union of Congolese Patriots (UPC) huko kashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo baina ya mwaka 2002 na 2003.
Katika kikao cha leo cha kesi hiyo, Jaji Robert Fremr amesema haoni sababu ya kumpunguzia adhabu Bosco Ntaganda na ametoa hukumu ya kifungo cha miaka 30 jela ambacho ndicho kirefu zaidi kuwahi kutolewa na Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu yenye makao yake The Hague nchini Uholanzi.
Katika vita vya mashariki mwa Congo kundi la UPC linalodhibitiwa na watu wa ukoo wa Hema liliwalenga wapinzani wao wa ukoo wa Lendo kwa kuwafukuza kutoka kwenye mkoa wa Ituri wenye utajiri mkubwa wa madini. Mamia ya watu wa ukoo huo waliuawa na maelfu walilazimishwa kukimbia Makazi yao.
Orodha ya uhalifu na jinai zilizofanywa na Ntaganda inajumuisha kusajili watoto kama askari, ubakaji na utumwa wa kingono dhidi ya raia na askari watoto.
Aliyekuwa kiongozi wa Bosco Ntaganda, Thomas Lubanga, anatumikia kifungo cha miaka 14 jela baada ya mahakama ya ICC kumpata na hatia ya kusajili na kutumikisha watoto wadogo kama wapiganaji vitani.
Post a Comment