Maelfu ya raia wa Kuwait wamefanya maandamano makubwa kulalamikia hali mbaya ya kiuchumi na kimaisha pamoja na sheria inayohusiana na uraia wa nchi hiyo.
Maandamano hayo makubwa yalifanyika jana usiku katika medani ya al-Urdah huko Kuwait, mji mkuu wa nchi hiyo. Taarifa zinasema kuwa katika maandamano hayo wananchi wametaka kufanyiwa marekebisho mitaala ya elimu, ukarabati wa hospitali, kusimamishwa kodi za serikali, kusamehewa wafungwa wa kisiasa, kuwepo uhuru wa kujieleza, kutatuliwa matatizo ya ukosefu wa ajira na kubadilishwa sheria inayohusiana na uraia. Wanaharakati wa Kuwait kupitia mtandao wa kijamii wa Twitter wametaka kufanyiwa marekebisho mfumo wa kiuchumi ambapo sambamba na kupinga tozo jipya la kodi, wametahadharisha kwamba iwapo hali mbaya itaendelea nchini humo, basi wananchi wataendeleza maandamano barabarani.
Mialiko ya maandamano nchini humo ilianza tangu siku chache zilizopita kufuatia kupoteza maisha vijana wawili wa nchi hiyo waliofahamika kwa majina ya Zared al-Assami na Badr Mirsal al-Fadhli. Vijana hao wanaotoka katika tabaka la watu wasiotambuliwa kuwa raia 'Bidun' walijiua kutokana na hali mbaya ya kimaisha. Watu wa tabaka hilo la 'Bidun' ambao serikali imekataa kuwatambua kuwa ni raia wa Kuwait kutokana na kuwa na asili isiyo ya nchi hiyo, wamekuwa wakinyimwa haki za msingi za raia au wasiokuwa raia wa taifa hilo. Mababu wa jamii ya watu hao wamekuwa wakiishi Kuwait miongo mingi iliyopita lakini hadi sasa serikali ya nchi hiyo imekataa kuwatambua kawa ni raia wa nchi hiyo.
Post a Comment